2017-03-29 16:01:00

Yesu ni njia, ukweli, uzima na ufufuo kwa wale wanaomwamini!


Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima tulialikwa kumchagua Mungu kama mwanga wa maisha yetu, Mungu anayeganga, anayeponya na anayejitambulisha kuwa mimi ndiye. Tukiwa pamoja na Mungu tunaweza kuona vizuri uwepo wake na kumwabudu. Liturujia ya Neno la Mungu ya leo yatualika tutafakari ukuu wa Mungu juu ya uzima wa milele. Yesu anasema – waniaminio hawatakufa kamwe. Somo la kwanza la leo laongea kuhusu mwisho wa utumwa na kuanza kwa kipindi kipya kwa Israeli. Nabii Ezekieli anaona taifa la Israeli kama watu ambao walikata tamaa, wakabaki kama mifupa. Nabii anawakumbusha kuwa ahadi ya Mungu iko pale pale – nitawatoa katika makaburi yenu na kuwapa roho mpya. Hapa kuna mwaliko wa ufufuko si tu wa mwili bali pia wa moyo. Anaongea uwepo wa matumaini. Pale taifa teule lilipoanza kuamini tena, basi safari ya ukombozi iliendelea. Hii ndiyo roho mpya kama asemavyo mtume Paulo katika somo la pili anapongea juu ya roho anayeishi ndani yetu na kwa huyo roho sisi tunakuwa watu wake.

Ndugu zangu, hatuna budi kukumbuka kuwa tunaweza kuwa wafu hata kabla hatujafa. Kifo si tu kile cha mwili au dhambi bali hali yo yote ile inayoondoa uhai – kama kupoteza nguvu, hamu, matumaini na cho chote kile ambacho kinaondoa uzima ndani yetu. Mfano Waisraeli walipoteza matumaini, wakabaki kama mifupa mitupu. Katika Injili – tunamwona Yesu akitoa uhai na tunaona kuwa hakuna tena kifo kama tukiamini. Yesu analeta ufufuko dhidi ya majonzi na anajitambulisha wazi akisema mimi ndiye ufufuko na uzima. Habari ya Lazaro imeandikwa kutuonesha kuwa kuna ufufuko wa mwili na pia ufufuko wa moyo. Katika nyumba ya Martha na Maria walikuwepo watu wengi waliokuja kuwafariji lakini haikusaidia kumrudishia yule maiti uhai wake. Walitakiwa kumwita Yesu kama walivyofanya dada zake Lazaro. Hii inasema wazi kuwa peke yetu bila Yesu hatuna uhai wa kimungu, tutakufa kimwili na kiroho.

Katika hali ya kawaida ya kibinadamu, tunapokuwa katika taabu au tukizama katika dhambi tunashindwa kufanya cho chote chema hata kumwita Yesu na matokeo yake ni kubaki kama Lazaro kaburini. Ni hapa tunaona haja ya kumwita Yesu na hitaji la uwepo wa wengine ili kufanya kitu kwa ajili yetu. Tunaweza kusema nitafanya nini katika hali ngumu na ya kifo? Katika Mt. 10:8 tunaambiwa – ponyeni wagonjwa, fufueni wafu. Hii amri ni kwetu sote wafuasi. Tuna wajibu wa kuzika wafu, lakini pia tunafahamu kuwa tunatakiwa kufufua wafu. Dada zake Lazaro watupe changamoto kubwa. Wao walichukua hatua, hawakuona kama yote yameisha, walitambua uwepo wa Bwana, wakamwita. Swali. Inakuwaje mafundisho haya yako wazi lakini hatuayaelewi au hatuyaweki katika matendo? Shida ni nini?

Wito unatolewa wa kusoma maandiko matakatifu kila siku na kwa hali mpya na tutoe nafasi kwa Neno ili liingie akilini na moyoni mwetu, ili tuwe hilo neno watu waone waje kwetu. Hatuna budi kujiuliza kama makutano yetu na Yesu yameleta mabadiliko katika maisha yangu na wale ninaokaa nao. Je, matumaini yetu yakoje? Huwezi kutoa usichokuwa nacho. Maisha yetu hayana budi kuwa ni ushududa endelevu. Ushuhuda kama wa Yesu  - mimi ni mwanga Yoh: 9:39-41 , mimi ni mlango – Yoh. 10:7. Mimi ni mchugaji mwema Yoh. 10:11, mimi ni tawi - Yoh. 15:1

Tunaalikwa kutambua kuwa ufufuko huo ni kwa jili yetu. Kwamba maisha ya ufufuko yanaazia hapa hapa kinyume na tamko la Martha – ufufuko ni siku ya mwisho. Uongofu wetu, toba yetu n.k. hutegemea upendo wa Mungu kwetu, imani yetu n.k. Tusiwe kama Abunuwasi ambaye daima anatumia ujanjaujanja na hila kudhulumu wengine. Anashinda lakini anaumiza wengine. Sisi tuna uhakika toka kwake Yesu kwamba anayeamini hatakufa milele. Tunataka nini zaidi? Hatuna budi kumshukuru Mungu aliyetujalia maisha, maisha ya imani, ule uhusiano na Utatu Mtakatifu, hivyo hata tukifa bado tutaishi. Utukufu huo unaanza hapa hapa. Kile anachosema Mtume Paulo katika somo la pili – tunakuwa warithi wa utukufu huo kituimarishe. Mafundisho ya Biblia ni dhahiri – imani yahitajika – katika Kum. 5:26 – tunasikia habari ya Mungu aliye hai na katika Lk. 20:38 – tunaambiwa kuwa Mungu ni Mungu wa walio hai. Sisi tuitikie upendo huo na uhai huo.

Ndiyo maana Yesu anamwuliza kwanza Martha kama anaamini, halafu kinachofuata ni kumrudishia uhai yule maiti. Imani ya kina Martha kwa Yesu inamrudishia uhai yule aliyekuwa amekufa. Tunaona hilo katika somo la kwanza – uhai wa taifa la Israeli unatangulia na matumaini mapya. Nabii Ezekieli anasimama kati ya Mungu na watu na anaongea habari ya matumaini mapya. Katika injili Yesu anasema nimekuja ili wawe na uhai Yoh. 10:10. Sisi je tunawapatia matumaini gani wale waliokufa, wale ambao hawana uhai tena wa kimwili wala wa kiroho? Mtakatifu Francisko wa Assisi katika sala yake anasema ‘Ee Bwana unifanye chombo cha amani yako ....ili nilete matumaini pale yalipopotea”

Ndugu zangu, Waisraeli waliamini kuwa mtu akishafariki dunia roho iliachana kabisa na mwili siku ya tatu baada ya kifo. Baada ya hapo mwili huanza kuoza. Ona Martha alivyomwambia Bwana – ana siku ya nne, ananuka – Yoh. 11:39. Huu muujiza wa ufufuo wa Lazaro waonesha kuwa mbele ya Mungu hakuna kifo au kukata tamaa. Yahitajika ushirikiano na Mungu. Yahitajika imani hai na thabiti. Yahitajika imani tiifu na inayofanya kazi kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Kadiri ya mhubiri maarufu Padre Munachi, habari ya ufufuko wa Lazaro inatutafakarisha na kutuwajibisha katika mambo makuu matatu ambayo  mfuasi/wafuasi anatakiwa kuyafanya ili kupata uhai au kurudisha uhai uliopotea. Mambo haya yanagusa uhalisia wa maisha yetu ya kila siku na kama tukiyafanya kwa imani basi tutabaki salama. Mambo haya matatu yanajionesha katika lile tendo la kumfufua Lazaro. 

  1. Imani kwa Yesu. Yesu anawaambia watu waondoe jiwe – mstari 39-41. Wale watu waliweka mbali kile walichokuwa wanakiamini, kwamba amekwisha kufa. Ushiriki wa mtu unahitajika hapa.Wakashika imani mpya. Utii uliwasukuma. Yesu angeweza kuamuru jiwe liondoke bila kuwasumbua watu. Kinachooneka hapa ni kuwa Mungu anamtumia mwanadamu kutimiliza muujiza wake. C. S. Lewis anasema – Mungu hafanyi muujiza kile ambacho mwanadamu anaweza kufanya kwa utii.
  2. Amri kwa maiti. Mstari 43-44 – Lazaro toka nje. Hata maiti inamtii Yesu. Hata uozo unamtii Yesu. Mbele ya Mungu hakuna linaloshindikana. Hapa tunaona haja ya kufanya kitu hata kama tunajisikia au tunadhani kuwa tumekufa au kusongwa mno na dhambi zetu.
  3. Tena tunaona ushiriki wa mtu – mstari 44. Pamoja na kutoka nje, yule maiti hakuweza kujifungua vifungo vyake. Alihitaji jamii ifanye hivyo na iweze kumpokea. Twaona kuwa kumbe bado tuna nafasi kama jamii kuwasaidia wengine ambao tunadhani kuwa wamekufa au kukata tamaa.

Hakika tukifanya haya tutakuwa tumeshiriki kikamilifu kuishi yale mapenzi ya Yesu, mimi nimekuja ili wawe na uzima.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.