2017-03-29 13:42:00

Ibrahimu ni baba wa imani na matumaini, mfano bora wa kuigwa!


Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Warumi anasema kwamba, Mwenyezi Mungu alimweka Ibrahimu kuwa ni baba wa mataifa mengi kwani aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi. Imani ya Ibrahimu inamfanya kuwa ni baba wa imani na matumaini hata kwa Wakristo wa nyakati hizi. Kwa njia yake, waamini wanaweza kupokea tangazo la Fumbo la Ufufuko na maisha mapya yanayoshinda ubaya na kifo! Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 29 Machi 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Ibrahimu alimwamini Mwenyezi Mungu mwenye uwezo wa kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Alikuwa ni mtu ambaye hakuwa dhaifu wa imani, alifikiri juu ya mwili wake ambao ulikuwa umekwisha kufa! Haya ndiyo matumaini ambayo hata Wakristo wa nyakati hizi wanahamasishwa kuyamwilisha katika maisha yao. Mwenyezi Mungu alijifunua kwa Ibrahimu kuwa ni Mungu anayeokoa, anayewawezesha waja wake kutoka katika hali ya kukata tamaa na mauti, ili kukumbatia maisha.

Baba Mtakatifu anasema, huu ndio utenzi wa sifa na unabii unaoshuhudiwa katika maisha ya Ibrahimu, baba wa imani na matumaini na kupata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Hata Wakristo wanahamasishwa kutoka katika kifo ili kuambata maisha na kwa njia hii, Ibrahimu anakuwa kweli ni baba wa mataifa mengi anayetangaza ubinadamu mpya  ambao umekombolewa kutoka katika dhambi na mauti ili kuweza kuukumbatia upendo wa Mungu.

Mtakatifu Paulo, Mtume anawasaidia waamini kuona uhusiano uliopo kati ya imani na matumaini kwani Ibrahimu aliamini kwa kutarajia yasiyowezekana, hali inayojionesha kwa namna ya pekee, katika maisha yake kwa kukiona kifo kinamkodolea macho sanjari na maisha ya Sara aliyekuwa mgumba, kiasi kwamba, hawakutarajia kupata tena mtoto, lakini Ibrahamu akajiaminisha kwa Neno la Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kufuata mfano wa Ibrahimu, baba wa imani na matumaini.

Alijua kwa hakika kwamba, Mwenyezi Mungu aweza kufanya yote alioahidi, kwani Mungu anawatakia watu wake mema na kwamba, atatekeleza ahadi yake kwa wakati muafaka. Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu ni kwa waamini kufungua sakafu ya mioyo yao ili matumaini yaweze kuingia na kuchipuka. Mwenyezi Mungu ameahidi ushindi dhidi ya kifo na mauti kwa njia ya Fumbo la Ufufuko kwani Mungu ni ufufuko na uzima. Waamini wajitahidi kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie neema ya matumaini inayobubujika kutoka kwenye ahadi zake kama watoto wa Mzee Ibrahimu. Kwa njia ya ufufuko atawawezesha waamini wote kuwa wamoja katika Yeye na kwamba, Neno lake linadumu milele yote.

Hiki ndicho kiini cha matumaini kinachowawezesha waamini kudumu katika maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia mahujaji wote  furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Waendelee kuboresha imani na matumaini yao kwa njia ya Tafakari ya Neno la Mungu, Sala na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kipindi cha Kwaresima ni muda muafaka wa kupyaisha imani. Bikira Maria aliyejiaminisha kwa Neno la Mungu kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, awasaidie na kuwaenzi waamini katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, daima wakijitahidi kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.