2017-03-27 13:52:00

Kanisa kuendeleza mapambano dhidi ya nyanyaso kwa watoto wadogo


Tume ya Kipapa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia katika mkutano wake wa nane uliofanyika kuanzia tarehe 24- 26 Machi 2017; imeamua kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo. Wajumbe wanampongeza na kumshukuru Mama Marie Collins aliyekuwa mjumbe wa Tume hii kwa mchango wake katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo.

Ni matumaini ya Tume hii kwamba, waathirika wa nyanyaso za kijinsia wataweza kupata majibu ya haraka kutoka Vatican pale wanapowaandikia, kama kielelezo cha ukweli, uwazi na uwajibikaji katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ambazo kimsingi zimelichafua sana Kanisa kwa miaka ya hivi karibuni! Ni matumaini ya Tume kwamba, Mama Marie Collins ataendelea kutoa ushirikiano wa dhati hata akiwa nje ya Kamati, ili kusaidia kuwanoa wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Maaskofu wapya katika masuala haya ya nyanyaso za kijinsia.

Wajumbe kwa pamoja wameamua kushirikiana kufanya kazi na waathirika wa nyanyaso za kijinsia, ili mchango wao uweze kumsaidia Baba Mtakatifu kutoa dira na mwelekeo sahihi katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo. Wajumbe wameamua kutuma mapendekezo zaidi kwa Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuyapima na hatimaye, kuyafanyia kazi. Baba Mtakatifu anaendelea kuwatia shime wajumbe kutekeleza wajibu wao bila ya kukata tamaa, ili kuyasaidia Makanisa Mahalia kuwajibika barabara katika kuwalinda watoto wadogo ili wasitumbukizwe kwenye nyanyaso za kijinsia.

Tume pia inaendelea kuzungumza na wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia wakati wanapofanya hija ya kitume mjini Vatican. Mwongozo wa Tume hii ni muhimu sana na kwamba, wataendelea kushirikiana na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ili kuhakikisha kwamba, Mwongozo huu unayafikia Mabaraza ya Maaskofu Katoliki. Kwa viongozi wa Kanisa na watu wenye mapenzi mema wanaotaka, wanaweza kutembelea katika tovuti ya Tume kwa anuani ifuatayo: (www.protectionofminors.va). Wajumbe wa Tume pia walipata nafasi ya kushiriki katika mafunzo yaliyotolewa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani kuhusu ulinzi wa watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia majumbani. Walengwa wakuu walikuwa ni wale kutoka nchi za Amerika ya Kusini ambazo kwa kiasi kikubwa zina mtandao wa shule za Kikatoliki. Viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican wamehudhuria pia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.