2017-03-25 11:42:00

Hotuba ya Papa Francisko kwa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya


Umoja na mshikamano wa dhati; utu, heshima na zawadi ya maisha; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; tunu msingi za Kikristo, ajira na vijana; ukarimu na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji ni kati ya mambo mazito ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyagusia kwenye hotuba yake alipokutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Jumuiya ya Ulaya pamoja na wawakilishi mbali mbali, Ijumaa, tarehe 24 Machi 2017 kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Ulaya. 

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewarejesha tena viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na waasisi wao hapo tarehe 25 Machi 1957, ili kujiwekea sera na mikakati ya kukabiliana na changamoto mamboleo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, lakini hasa kwa kuwekeza katika ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu: kwa kulinda na kudumisha maisha, udugu na haki, kama chachu muhimu sana ya mabadiliko Barani Ulaya, baada ya patashika nguo kuchanika wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Waasisi wa Umoja wa Ulaya walikazia kwa namna ya pekee zawadi ya maisha ya binadamu na haki zake msingi sanjari na umuhimu wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano unaosimikwa katika: ukweli na haki; msingi wa sera za kisiasa, kisheria na kijamii Barani Ulaya. Jumuiya ya Uchumi Barani Ulaya itaweza kudumu na kushamiri, ikiwa kama itaendelea kujikita katika uaminifu kwa mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Ulaya. Hii ilikuwa ni changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengenano, ili kuokoa maisha ya familia zilizokuwa zinaogelea katika dimbwi la umaskini, vita na mipasuko ya kijamii, inayoendelea kushuhudiwa hata leo hii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna umati mkubwa wa watu wanaokimbia nchi zao kutokana na vita, njaa na umaskini; hawa ni watu wanaopaswa kuoneshwa mshikamano wa upendo ili kuandika tena ukurasa wa matumaini kwa ajili yao wenyewe pamoja na familia zao. Kumbe, wote wanapaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa amani unaotoa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hizi ni tunu msingi zilizobainishwa na waasisi wa Umoja wa Ulaya, lakini ikumbukwe kwamba, mizizi ya tunu hizi ni utamaduni na Mapokeo ya Kikristo yanayozingatia kwa namna ya pekee kabisa: utu wa binadamu, uhuru na haki.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, ikiwa kama Umoja wa Ulaya bado unaendelea kushamiri ni kwa sababu umesimikwa katika mapokeo ya pamoja yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiutu zinazotoa kipaumbele cha pekee kwa: utu na heshima ya binadamum, haki, uhuru, bidii ya kazi, juhudi na maarifa; upendo kwa zawadi ya maisha ya familia: maridhiano kati ya watu, shauku ya ushirikiano na amani. Hizi ni tunu ambazo zitaendelea kumwilishwa katika maisha ya watu ili kujenga jamii ya watu wanaoheshimiana na kuthaminiana licha ya tofauti zao.

Baba Mtakatifu Francisko amezungumzia kuhusu mustakabali wa Umoja wa Ulaya unaopaswa kukabiliana na changamoto mamboleo kwa kufanya upembuzi yakinifu, kwa kuendelea kuwa macho na makini kwa kuamua na kutenda. Kumbe, kipindi cha changamoto ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati ili hatimaye, kufanya mang’amuzi ya kina ili kutengeneza njia ya matumaini itakayo zaa matunda kwa wakati wake.

Bara la Ulaya litaweza kuwa na matumaini ikiwa kama binadamu atapewa kipaumbele cha kwanza katika taasisi zake; kwa kumsikiliza kwa makini; kwa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia; kwa kuheshimu na kuthamini umoja katika tofauti; kwa kushirikiana na kushikamana katika kutumia na kugawana rasilimali fedha, vitu na akili; kwani wote wanaunda Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Umoja wa Ulaya utakuwa na matumaini kwa kuambata mshikamano wakati wa raha na shida kama ambavyo imejionesha wakati Uingereza ilipokumbwa na kitendo cha kigaidi hivi karibuni. Mshikamano ni dawa ya mchunguti dhidi ya ubinafsi na umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kwa maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; ni watu wanaotaka kujijenga kisiasa. Mshikamano unatoa nafasi ya kusaidiana, kwa wenye nguvu kuwashika na kuwasindikiza wanyonge katika safari yao, ili wote kwa pamoja waweze kufikia lengo linalokusudiwa.

Bara la Ulaya litaweza kuwa na matumaini  kwa kuondokana na woga pamoja na tabiaya kujifungia katika ubinafsi wake, kama kielelezo cha usalama wa watu wake. Lakini, ikumbukwe kwamba, historia ya Bara la Ulaya inasimikwa katika mchakato wa mwingiliano wa watu na kwamba, utambulisho wake ni ule wa watu kutoka katika tamaduni mbali mbali mambo ambayo yamechangia utajiri wa Ulaya katika maisha ya kiroho; utajiri ambao unapaswa kupyaishwa kila wakati ili kuondokana na utupu wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu, vinginevyo watajenga mazingira ya watu wenye misimamo mikali, hatari sana katika jamii.

Bara la Ulaya litaweza kupata matumaini kwa kuwekeza katika mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na amani, kwani amani ni jina jipya la maendeleo ya watu! Pasi na amani, maeneo ya pembezoni mwa jamii yataendelea kuwa ni vituo vya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; mahali pa fujo na vurugu za kijamii. Matumaini ya Bara la Ulaya anasema Baba Mtakatifu yanajikita kwa kuwa wazi kwa mambo yanayokuja mbeleni; kwa kuwajengea watu uwezo wa kuanzisha na kuendeleza familia; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utakatifu wa maisha ya binadamu. Miaka 60 ya Umoja wa Ulaya iwe ni fursa ya kuganga na kutibu mapungufu yaliyojitokeza huko nyuma; kwa kushirikiana na kushikamana kwa pamoja; kwa kuamua na kutenda kwa ujasiri. Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema, Vatican na Kanisa katika ujumla wake, litaendelea kuonesha ushirikiano na Umoja wa Ulaya kwani Bara la Ulaya kwa hakika linahitaji kujengwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.