2017-03-25 15:23:00

Fungueni macho yenu ya imani ili kumwona Yesu Mwanga wa Mataifa!


Katika kipindi cha Kwaresima, Mama Kanisa anatukumbusha kwa namna ya pekee kusali na kukazia maisha ya Kisakaramenti, kulitafakari Neno la Mungu na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yetu kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji! Ni kipindi cha kutekeleza matendo ya huruma, ili kuwasaidia wengine kuona na kuonja mwanga wa imani, matumaini na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Leo Kanisa linaadhimisha Jumapili ya nne ya Kipindi cha Kwaresima, maarufu kama Jumapili ya furaha, Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini wote kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Furaha ya Injili, kwa kushiriki kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili; kwa kuendelea kulipyaisha Kanisa katika maisha na utume wake; kwa kuwakumbatia na kuwaenzi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha; kwa kusimamia misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano, ili kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi!

Kwa namna ya pekee kabisa, leo Mama Kanisa anapenda kuturejesha tena kwenye zawadi ya imani ambayo tumekirimiwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, inayomwezesha mwamini kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, tayari kushiriki katika maisha ya uzima wa milele. Kwa njia ya Ubatizo, mwamini hushiriki mauti ya Kristo, huzikwa na kufufuka pamoja naye, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima ilimwonesha Yesu akizima kiu ya imani ya Mwanamke Msamaria na hivyo kumwashia moto wa upendo kwa Mungu na jirani, pale walipokutana na kuzungumza kisimani! Kijiwe cha wapendanao!

Leo Yesu anawataka wafuasi wake kufuata nyayo zake kwani Yeye ni Mwanga wa Mataifa, chemchemi ya maisha ya uzima wa milele. Mwinjili Yohane anasimulia kwa ufundi mkubwa tukio la Yesu kumponya huyu kipofu asiye na jina! Hapa kila mwamini anachangamotishwa kujisikia kuwa yuko Mahakamani, ili kuweza kujipima ikiwa kama ile neema ya utakaso aliyoipokea wakati wa Ubatizo bado iko hai na ikiwa kama anatembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka kwa kuifia dhambi na makandokando yake kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume kwamba, mtu akiwa katika dhambi anatembea gizani na huko anaweza kujikwaa.

Kumbe, Imani inapaswa kulindwa kwa njia ya tunu msingi za Kiinjili; inapaswa kuendelezwa kwa kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Imani inaboreshwa kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na malezi ya dhamiri nyofu. Imani inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kusimamia haki, amani na ustawi wa wengi! Paulo Mtume, anatualika waamini kutembea katika upya wa maisha kwa kumwambata Kristo Yesu anayezima kiu ya imani yetu na kuwasha moto wa upendo na matumaini. Imani iwe ni dira na mwongozo wa maisha yetu katika medani mbali mbali za maisha; wakati wa shida na raha; wakati wa magumu na hali ya kukata tamaa kutokana na changamoto za maisha. Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya imani na kwamba, imani si vazi la sherehe au jumapili bali ni utambulisho na mwanga unaofukuzia mbali giza na upofu wa maisha, kwa kujikita katika uaminifu, ukweli na uadilifu kama watoto wateule wa Mungu.

Neno kuu katika tafakari yetu ni imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka! Imani inayopaswa kushuhudiwa. Neno la Pili ni Efata! Funguka! Yesu katika maisha na utume wake, aliwaondolewa watu dhambi zao, akawagusa na kuwaponya kutoka katika shida na mahangaiko yao, changamoto kubwa kwa waamini ni kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia ile furaha ya kuona matendo makuu ya Mungu katika maisha. Leo tunaalikwa kufunga ili kusikiliza kwa makini Neno la Mungu linalotangazwa na kushuhudiwa kwetu!

Funguka, ili uweze kusikiliza na kuona shida, mateso na mahangaiko ya jirani zako! Funguka ili uweze kumshuhudia kwa maneno na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwamba, Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu, Mwanga wa Mataifa na Uso wa huruma ya Baba wa milele! Funguka ili kuondokana na matendo ya giza yanayokwamisha uhusiano wako na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zako. Mtakatifu Paulo anakaza kusema, tunda la nuru ni katika wema wote, haki na ukweli na kwamba, matendo ya giza ni kielelezo cha kifo!

Mwenyezi Mungu humchagua mtu awaye yote kwa ajili ya kazi na utume maalum kama ilivyokuwa kwa Daudi aliyefungua historia mpya ya kazi ya wokovu. Ndiye aliyepakwa mafuta, kwani Mwenyezi Mungu anaangalia yale yaliyofichika kwenye sakafu ya moyo wa mwanadamu; anamtakasa na kumtuma, ili aweze kuwa ni shuhuda na chombo cha Habari Njema ya Wokovu. Bwana Yesu aliwafanya viziwi wasikie na bubu waseme, atujalie tuweze kusikia kwa masikio Neno lake; na kuungama kwa midomo yetu imani yetu kwa Kristo, kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba. Basi ndugu yangu, tumwombe Mwenyezi Mungu afungue macho yetu kwa mwanga wa Roho Mtakatifu ili tuweze kumwona Yesu mwanga wa mataifa, ili kumwamini na kumshuhudia mbele ya watu kama alivyofanya yule kipofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.