Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha: imani, matumaini na mapendo

Yesu aliwaimarisha mitume wake katika imani ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Fumbo la Msalaba, kielelezo cha hali ya juu cha huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu!

23/03/2017 15:14

Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican,  ni wakati mwingine tena wa kuendelea  kupata  tafakari  ya kiroho   na hasa wakati huu wa kwaresima. Kwani katika kipindi hiki cha Kwaresima  Mama Kanisa anatualika kwa namna ya pekee kufanya tathimini ya maisha yetu ya kiroho, ili tathmini hiyo  ipate kutuletea mabadiliko katika maisha yetu na mwenendo mzima wa maisha yetuHivyo Pamoja na  manufaa mbalimbali ambayo kila mmoja atajichotea katika kipindi hiki cha kwaresima, tuendelee kuimarisha imani yetu katika utukufu ujao.

Kumbe, Yesu  tangu mwanzo kabisa mwa kazi yake ya ukombozi alijua kuwa atapata mateso makali na atauawa ili Maandiko yapate kutimia.  Lakini alitaka kazi yake ya kueneza habari njema ya ufalme wa Mungu na kutangaza ukombozi isikome na kifo chake, bali iendelee hata baada ya kifo chake. Hivi Yesu kwa kulifahamu hili aliwachagua mitume wake kumi na wawili ili aweze kuandika ujumbe wake mioyoni mwao na kwa kupitia hao ujumbe wake uenee kwa vizazi vyote duniani. Hao Mitume aliowachagua alifuatana nao na kuwafundisha kwa maneno na matendo yake ya kila siku.

Baada ya Yesu kukaa na hawa mitume wake takribani  miaka mitatu, ndipo alipowauliza swali kuwa Yeye ni nani? Na swali hili likiwa   ni kupima ukomavu wao katika kumwelewa Yeye kuwa ni nani. Petro akiwawakilisha wenzake anajibu swali hili  kwa komwonesha Yesu kuwa ni “Mwana wa Mungu na Masiha.”  Petro kwa kujibu swali hili, Yesu anatambua kwamba sasa ni muda muafaka wa kuwapatia mitume wake “fundisho la kukomaa” kwa kuwaambia bayana lengo la ujio wake na lile ambalo alikuwa anasubiri kulikabili. Yesu anatoboa siri yake kuwa imempasa mwana wa Adamu, kama walivyomkiri, kupata mateso mengi na kukataliwa na wakuu wa makuhani na wazee na waandishi na kuuawa (kifo cha Msalaba). Ila hapa, Petro kwa mara nyingine anajitokeza na  kupinga kuwa haiwezekani kwa mtu mkubwa na maarufu na muhimu kama Masiya wa Bwana, kukataliwa, kuteswa na hata kuuwawa.

Hivyo mpaka hapa, Yesu anagundua kuwa mitume wake hawajamwelewa  vya kutosha. Imani yao bado ni changa sana. Sasa kwa watu ambao hawajakomaa kiimani kifo cha Yesu hapa ni kikwazo! Hivi Yesu anatambua wazi kwamba inabidi awaimarishe katika imani ili waweze kustahimili yote yatakayomkuta hapo baadaye, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji kwa watu wa mataifa!

Kwa kulitazama hilo ndipo, Yesu akawachukua Petro, Yohane na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, na mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Na watu wawili walikuwa wakizungumza naye. Nao ni Musa na Eliya; walionekana katika utukufu wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu. Ila ukumbukwe, ukweli wenyewe kuhusu Yesu ni kwamba, Yesu ni Masiha atakayeteswa, kufa na kufufuka kwa wafu tumaini la utukufu ujao. Kashfa ya Msalaba ilikuwa ni nzito sana katika maisha ya Mitume wa Yesu. Kipindi cha Kwaresima kitusaidie kuimarisha imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake, daima tukijitahidi kudumisha ile neema ya utakaso tuliyopokea wakati wa Sakramenti ya Ubatizo. Changamoto kubwa ni kuwa kweli mashuhuda na vyombo vya ushuhuda wa ukuu, utakatifu na utukufu wa Mungu katika maisha ya watu!

Na Padre Agapiti Amani ALCP/OSS.

23/03/2017 15:14