2017-03-23 08:30:00

Hali ya kisiasa mkoani Dar Es Salaam kwa sasa ni tete!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 23 Machi, 2017 amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri. Katika Mabadiliko hayo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Palamagamba Aidan John Mwaluko Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amemteua Dkt. Harrison George Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Uteuzi huu unaanza mara moja. Wateule wote wataapishwa tarehe 24 Machi, 2017 Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Wachunguzi wa mambo wanasema, mabadiliko haya ni matokeo ya aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye kusema kwenye vyombo vya habari kwamba endapo atashindwa kusimamia uhuru wa habari na vyombo vya habari nchini Tanzania atakuwa hafai kubaki kwenye nafasi hiyo kwa kuwa atakuwa ameshindwa majukumu yake katika nchi huru. Nape ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akizungumzia na kulaani kitendo kinachodaiwa kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, cha kuvamia chombo cha habari cha Clouds, akiwa na askari wenye silaha na kukifananisha kitendo hicho na kuinajisi taaluma ya habari.

Waziri huyo alisema amezoea kuona matukio kama hayo yanatokea kwenye nchi ambazo zimepinduliwa kwa bunduki lakini kwa nchi yetu si jambo jema kwenda kwenye vyombo vya habari na mabunduki mkononi. "Tumezoea kuona matukio haya yanatokea kwenye nchi ambazo zimepinduliwa kwenda kwenye vyombo vya habari na mabunduki si sawa, kwa jambo hili tunataka kutenda haki tumsikilize Mkuu wa Mkoa ili tujue kwanini amefanya jambo hili". Alisema Nape

Kufuatia tukio hilo Waziri Nape aliunda tume yenye wajumbe takribani watano itakayoenda kumhoji Makonda na kutoa mrejesho wa kazi hiyo ndani ya masaa 24 ikiwa imeeleza sababu maalum kutokea kwa tatizo hilo. Huu ni mfululizo wa matukio ambayo yameutikisa mkoa wa Dar es Salaam kwa siku za hivi karibuni baada ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza majina ya watuhumiwa wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya; orodha iliyogusa “vigogo” kadhaa mkoani Dar es Salaam. Baadaye likaibuka sakata la kugushi vyeti ambalo kwa namna ya pekee lilimgusa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda. Kutokana na matukio yote haya wachunguzi wa mambo wanasema, Dar es Salaam, hali ya kisiasa kwa sasa ni tete!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.