2017-03-20 10:29:00

Kampeni ya Kwaresima nchini Kenya kwa Mwaka 2017: Uchaguzi mkuu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya hivi karibuni limezindua kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2017 inayoongozwa na kauli mbiu “Uchaguzi wa amani na unaoaminika… Viongozi waadilifu” kwa maandamano makubwa na hatimaye, Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Nairobi, Kenya na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu nchini Kenya. Kampeni ya Kwaresima kwa mwaka huu nchini Kenya inagusa kwa namna ya pekee kabisa uhalisia wa maisha ya wananchi wa Kenya hasa wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya mchakato mzima wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 8 Agosti 2017.

Itakumbukwa kwamba, chaguzi nchini Kenya kwa miaka ya hivi karibuni, zimekuwa ni chanzo kikuu cha mpasuko wa kijamii na maafa makubwa kwa wananchi na mali zao; Umoja na mshikamano wa kitaifa. Kumbe, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka wananchi pamoja na viongozi wanaohusika na mchakato mzima wa uchaguzi kuhakikisha kwamba, kweli uchaguzi wa Mwaka 2017 unakuwa huru na wa haki; uchaguzi unakubalika na wengi. Wananchi wanatakiwa kuwajibika barabara na hatima ya nchi yao, ili kuwapata viongozi waadilifu, wachapakazi na wapenda amani, watu  watakaokuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa Kenya kwa ari na moyo mkuu!

Kampeni ya Kwaresima inajikita katika mambo nyeti ya usalama; vijana na jamii inayowazunguka, ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; uchaguzi mkuu kwa kukataa ukabila, udini na umajimbo mambo ambayo hayana tija, mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Kenya. Kampeni ya Kwaresima imefafanuliwa kwa kina na mapana na Askofu Cornelius Arap Korir, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.

Askofu Cornelius Arap Korir anasema, kilio cha wananchi wa Kenya kwa miaka kadhaa iliyopita ni kuhusu uwajibikaji na maadili ya viongozi waliopewa dhamana na wananchi wa Kenya ili kuwaonesha dira na njia katika maisha yao. Kwa bahati mbaya, kuna umati mkubwa wa viongozi ambao umefikishwa mahakamani kutokana na rushwa, ufisafi na ubadhilifu wa mali ya umma; ukabila, udini na umajimbo. Umefika wakati kwa familia ya Mungu nchini Kenya kufanya maamuzi machungu kwa kuwachagua viongozi waadilifu, wachapakazi na wanaopania ustawi na maendeleo ya watu!

Viongozi wasichaguliwe kwa dhana ya ukabila, udini au mahali anapotoka mtu. Kanisa Katoliki kwa kuongozwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa, linatawaka wananchi wa Kenya wasikubali kutoa wala kupokea rushwa wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi, bali waongozwe na dhamiri nyofu na wala si kutaka kuganga njaa kwa siku moja na hatimaye, kulitumbukiza taifa katika majanga makubwa! Familia ya Mungu nchini Kenya, ijenge na kudumisha utamaduni wa upendo, haki, amani na utawala wa sheria. Chuki, uhasama na kutaka kulipizana kisasi ni mambo ambayo ni kinyume kabisa cha tunu msingi za Kiinjili. Usalama ni changamoto kubwa ambao familia ya Mungu nchini Kenya imetafakari wakati wa Juma la kwanza la Kwaresima kwa Mwaka 2017. Usalama ni dhana inayogusa medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Kenya; ni dhana inayotaka kujenga na kuimarisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; ngono na picha chafu zinazosambazwa na vyombo na mitandao ya kijamii; nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo pamoja na sheria za usalama na mazingira bora kazini.

Kampeni ya Kwaresima, Juma la pili inajikita katika ustawi na maendeleo ya vijana wa Kenya, ili kweli waweze kuendelezwa kwa hali na mali; kwa kuwapatia majiundo makini na endelevu, ili waweze kupata ukomavu katika tunu msingi za maisha ya Kikristo pamoja na kuwa na burudani zinazozingatia maadili na utu wema. Juma la tatu la Kampeni ya Kwaresima, Kanisa Katoliki nchini Kenya, linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote!

Hii inatokana na ukweli kwamba, kwa miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wanaofariki dunia nchini Kenya kutoka na ugonjwa wa Saratani. Haya ni matokeo ya uchafuzi wa mazingira, vyanzo vya maji sanjari na matumizi mabaya ya mbolea mashambani. Kumekuwepo na tabia ya kutojali kutunza mazingira kwa kutupa taka ovyo! Matokeo yake ni madhara kwa afya ya binadamu na mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kusababisha athari kubwa kwa watu na mali zao.

Kampeni ya Kwaresima Juma la Nne inajikita kwa namna ya pekee kabisa katika Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Kenya hapo tarehe 8 Agosti 2017 na kwamba, hadi wakati huu, homa ya uchaguzi mkuu inaendelea kupanda na kushuka, lakini familia ya Mungu nchini Kenya inapaswa kupiga kura inayowajibisha, kwanza kabisa kwa wananchi wengi kujitokeza ili kutekeleza haki yao ya Kikatiba kwa kupiga kura makini, kwa hekima na busara ili kuwapata viongozi waadilifu. Wanasiasa wanaowania madaraka wawe pia tayari kupokea matokeo halali ya uchaguzi mkuu, kwani mara nyingi patashika nguo kuchanika huanza kwa baadhi ya wanasiasa kugomea matokeo na hatimaye kuanza kushambuliana kwa maneno na matendo, hali ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imepelekea machafuko makubwa ya kisiasa nchini Kenya.

Maaskofu wanasema, mwaka huu, wananchi wanataka uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Serikali iliyoko madarakani pamoja na vyama vya upinzani, kila upande ukitekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Vyama vya upinzani vinapowajibika vyema, vimekuwa ni msaada mkubwa wa kuidhibiti pamoja na kuiwajibisha Serikali ili iweze kutekeleza dhamana na wajibu wake mbele ya umma wa wanachi wa Kenya, ili kucharuka katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linakaza kusema, ukabila usiokuwa na mashiko wala mvuto ni tema itakayochambuliwa wakati wa Juma la Tano la Kampeni ya Kwaresima. Uwepo wa makabila mengi nchini Kenya ni ukweli usiofumbiwa macho na kamwe usiwe ni sababu ya chokochoko na mipasuko ya kijamii. Familia ya Mungu nchini Kenya inapaswa kufurahia utofauti wake na hatimaye, kutajirishana kwa amana na urithi huu mkubwa; ukabila unaosababisha chuki, kinzani na misigano ya kijamii ni kinyume kabisa cha tunu msingi za Kiinjili, kwani binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya lina waalika waamini kufunga na kusali ili kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kuwajibika barabara katika mchakato wa uchaguzi mkuu, kwa kudumisha misingi ya haki, amani tayari kupiga kura kwa kuwajibika. Wananchi waoneshe utulivu wakati na baada ya uchaguzi mkuu kwa kuepuka kinzani anasema Askofu Cornelius Arap Korir, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.