Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Jimbo kuu la Milano liko tayari kumpokea Papa Francisko 25 Machi 2017

tarehe 25 Machi 2017 itaacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za wananchi wa Jimbo kuu la Milano.

20/03/2017 07:00

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Machi 2017 anatarajiwa kutembelea Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia. Akiwa Jimboni humo, Baba Mtakatifu akiwa ameambatana na Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano atatembelea Parokia ya Mtakatifu Galdino na hapo kama Baba wa maskini, atapata nafasi ya kutembelea familia mbili ili kujionea hali halisi ya maisha ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Milano. Atapata nafasi ya kusalimiana na wawakilishi wa familia za makundi ya wahamiaji na wakimbizi; waamini wa dini ya Kiislam pamoja na familia za maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Majira ya saa 4:00 asubuhi, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea Kanisa kuu la Jimbo kuu la Milano na huko atashuka chini kwenye Kikanisa kilichojengwa kunako mwaka 1606 na Francesco Maria Richini kinachohifadhi masalia ya Mtakatifu Charles Borromeo. Baba Mtakatifu atasali kwa kitambo kidogo mbele ya Sakramenti kuu pamoja na kutoa heshima zake kwa masalia ya Mtakatifu Charles Borromeo. Atakutana na kuzungumza na wakleri na watawa pamoja na kujibu maswali na dukuduku zitakazotolewa na wakleri. Baba Mtakatifu baadaye, atazungumza na waamini watakaokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Milano pamoja na kusali nao Sala ya Malaika wa Bwana.

Baba Mtakatifu akiwa Jimbo kuu la Milano atapata nafasi ya kutembelea Gereza kuu la “San Vittore” na kuzungumza na viongozi pamoja na askari magereza; atazungumza na wafungwa na baadaye kutembelea baadhi ya vyumba vya gereza hilo ili kujionea mwenyewe hali halisi ya wafungwa magerezani nchini Italia. Baadaye, Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana na wafungwa 100 gerezani hapo. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa na upendeleo wa pekee kwa wafungwa na daima katika ziara zake za kichungaji amekuwa walau akipata nafasi ya kutembelea na kuzungumza na wafungwa.

Baba Mtakatifu majira ya saa 9:00 Alasiri kwa Saa za Ulaya, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, lakini kabla ya Misa, atazungumza kidogo na Maaskofu pamoja kamati ya maandalizi ya Ujio wa Baba Mtakatifu Jimbo kuu la Milano. Ibada hii ya Misa Takatifu itaadhimishwa kwenye Uwanja wa Monza. Baada ya Misa Baba Mtakatifu majira ya saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya kwenye Uwanja wa michezo wa “San Siro” atakutana na kuzungumza na wazazi, walezi na watoto wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara. Atatumia fursa hii kujibu maswali kadhaa yatakayoulizwa na watoto hawa. Baadaye, Baba Mtakatifu atakuwa anahitimisha safari yake ya kichungaji Jimbo kuu la Milano na kuanza kurejea tena mjini Vatican ili kuendelea na utume na maisha yake kama kawaida!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

20/03/2017 07:00