2017-03-18 16:16:00

TANZIA: Kardinali Miloslav Vlk amefariki dunia!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Miloslav Vlk, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Prague, nchini Czech aliyefariki dunia tarehe 18 Machi 2017 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi kwa Kardinali Dominic Duka wa Jimbo kuu la Prague anapenda kumshukuru Mungu kwa kumwezesha Kardinali Vlk kuweza kuvumilia mateso na mahangaiko yake ya ugonjwa kwa imani na matumaini, sasa anapenda kumwombea mtumishi wake mwaminifu na jasiri aweze kupumzika katika usingizi wa amani.

Baba Mtakatifu anapenda kuungana kiroho na wale wote wana omboleza msiba huu mzito. Anamkumbuka kwa namna ya pekee, kutokana na ujasiri, uaminifu na udumifu wake wa imani kwa Kristo na Kanisa lake wakati wa nyanyaso na madhulumu dhidi ya Kanisa. Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya huduma mbali mbali kwa familia ya Mungu nchini Czech ili iweze kupeta: kiroho na kimwili kama ushuhuda wa Injili ya furaha. Alijizatiti kikamilifu ili kulipyaisha Kanisa la Kristo, daima akionesha unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito!

Marehemu Kardinali Vlk alizaliwa tarehe 17 Mei 1932, Kusini mwa Bohemia. Ni kiongozi ambaye aliteseka sana chini ya utawala wa Kikomunisti. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi katika shida na majaribu makubwa akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 23 Juni 1968. Tarehe 14 Februari 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 31 Machi 1990. Kutokana na ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, kunako tarehe 27 Machi 1991, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Prague, Jamhuri ya Watu wa Czech. Tarehe 26 Novemba 1994 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Kardinali. Kwa muda mrefu amekuwa akiugua na ilipofika tarehe 18 Machi 2017 akafariki dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.