Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu!

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi anaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Baba mlishi wa Yesu. - ANSA

18/03/2017 17:09

Kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Lakini kutokana na Siku kuu hii kuangukia Jumapili, Kanisa linaadhimisha Siku kuu hii, Jumatatu tarehe 20 Machi 2017. Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, ameiadhimisha Siku kuu hii, Ijumaa tarehe 17 Machi 2017 ili kuwapatia waamini nafasi ya kumtafakari kwa kina na mapana Mtakatifu Yosefu aliyeonesha na kushuhudia unyenyekevu na hekima ya hali ya juu kwani kama binadamu, watu wanategemezana na kukamilishana.

Huu ni mwaliko pia kwa waamini kujinyenyekesha mbele ya Mwenyezi Mungu, kinyume kabisa cha mwelekeo wa jamii mamboleo, ambamo watu wanataka daima kupewa kipaumbele cha kwanza hata katika vyombo vya upashanaji habari. Hawa ni watu ambao ndani mwao wanaficha wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko, hali ambayo wakati mwingine imekuwa ni chanzo cha majanga ya kijamii. Unyenyekevu na heshima inayofumbatwa katika maisha ya Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu unaonesha umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano yanayofumbata: ukweli, ustawi na maendeleo ya wote.

Hii ni changamoto ya kutafuta suluhu ya matatizo yanayojitokeza katika maisha pasi na kukata tamaa kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu. Wazazi na walezi wanapaswa kutekeleza wajibu na dhamana yao katika maisha, malezi na makuzi ya watoto wao: kiroho na kimwili sanjari na kuhakikisha kwamba, familia inapata mahitaji yake msingi. Kardinali Bagnasco anasikitika kusema, kutokana na athari za kiuchumi, kuna watu wengi ambao hawana fursa za ajira, kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya jumuiya hata kama wanazo sifa zinazohitajika katika mchakato wa uzalishaji na huduma.

Kardinali Bagnasco anasikitika kusema kuwa kutokana na  athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, vijana wengi wanakimbia kutoka nchini Italia ili kutafuta maisha bora zaidi nje ya Italia, jambo ambalo linasikitisha sana. Hawa ni vijana walioandaliwa barabara na taifa, lakini hawana fursa za ajira. Italia ina historia ya wananchi wake wengi kukimbilia uhamishoni ili kutafuta maisha bora zaidi. Historia iendelee kuwa mwalimu kwa wananchi wa Italia kutambua, kuthamini na kuwasaidia wakimbizi wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora nchini Italia. Kuna idadi kubwa ya wananchi wa Italia ambayo inanyemelewa na umaskini wa hali na kipato.

Takwimu kutoka Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Italia, zinaonesha kwamba, idadi ya wananchi wanaohudumiwa kwa chakula cha usiku inaendelea kuongezeka maradufu. Kardinali Bagnasco anawataka wananchi wa Italia kujenga utamaduni wa kujadiliana katika ukweli, uwazi na heshima ili kuweka hadharani matatizo na changamoto za maisha, tayari kuzipatia ufumbuzi wa kutosha. Utamaduni wa kujibizana kwa njia ya vyombo vya habari hausaidii katika kuleta ukomavu wa kisiasa, kidemokrasia na kiuchumi. Watu wajenge madaraja ya kukutana na kujadiliana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

18/03/2017 17:09