2017-03-18 07:59:00

Papa Francisko aongoza Ibada ya Toba na kutoa huruma ya Mungu!


Mama Kanisa anafundisha kwamba, Yesu Kristo ni mganga wa roho na mwili; anayesamehe dhambi za wenye kupooza; ndiye anayemrudishia mwamini afya ya mwili na kulitaka Kanisa liendeleze kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, kazi yake ya uponyaji na ya wokovu, hata miongoni mwa viungo vyake. Kwa waamini waliojiandaa vyema na ambao wako tayari kukimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho hupokea kutoka humo huruma ya Mungu na maondoleo ya dhambi sanjari na kupatanishwa na Kanisa ambalo dhambi yao imelijeruhi; Kanisa ambalo kwa upendo na mfano wa sala huangaikia wongofu wa watoto wake.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni, tarehe 17 Machi 2017 ameongoza Ibada ya Kitubio kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, kitubio humdai mdhambi kupokea kwa hiari moyoni mwake: majuto; kinywani mwake maungano; katika matendo yake unyenyekevu kamili na malipizi yanayozaa matunda ya wongofu wa ndani. Ibada ya kitubio ilijikita katika hatua kuu nne yaani: kutubu dhambi kwa kuchunguza dhamiri kwa mwanga wa Neno la Mungu. Hatua ya pili ilikuwa ni kuungama dhambi. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaungamisha waamini saba waliokuwa wamejiandaa kwa ajili ya kupokea huruma ya Mungu.

Kwa vile dhambi husababisha madhara makubwa kwa Mungu na jirani, kumbe, kuna haja ya kufanya malipizi ya dhambi kama njia ya kujipatia afya kamili ya maisha ya kiroho. Baadaye kilifuatia kitubio ambacho kila mwamini atatekeleza kadiri ya mazingira yake. Kitubio kinaweza kuwa ni kwa njia ya sala, matoleo, matendo ya huruma: kiroho na kimwili sanjari na huduma makini kwa jirani. Waamini wanakumbushwa kwamba, malipizi wanayoyafanya ni kwa njia tu ya Kristo Yesu anayewatia nguvu na kuwawezesha, kwa hiyo mtu hana cha kujisifia, bali kujisia kote ni katika Kristo ambaye ndani mwake wanafanya malipizi ya dhambi zao na kutoa matunda yapatanayo na toba ambayo hupata nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Msamaha wa dhambi huleta upatanisho na Mungu, jirani na Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.