2017-03-16 15:09:00

Papa Francisko: Msimezwe na malimwengu na kushindwa kuwasaidia maskini


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 16 Machi 2017 amewataka waamini kuwa makini ili dhambi isiwatumbukize katika rushwa na hatimaye, kushindwa kuona, kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao kama ilivyotokea kwa Maskini Lazaro na Tajiri asiyejali wala kuguswa na mateso ya watu wengine. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kuchunguza dhamiri zao, ili hatimaye, waweze kutembea katika njia ya haki, ukweli na uzima kwa kumtegemea na kumtumainia Mwenyezi Mungu katika maisha yao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa mtu anayejiamini kupita kiasi mara nyingi ni yule ambaye amemezwa na malimwengu yaani: kiburi na utajiri wa mali na fedha; mambo ambayo mara nyingi yanamfanya mwanadamu kutumbukia katika anasa kiasi hata cha kushindwa kuona na kuguswa na mahangaiko ya jirani zake. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Maskini Lazaro na Tajiri anayesimuliwa na Mwinjili Luka aliyekuwa anajipamba kupindukia, akala, akashiba na kusaza, bila hata kumwangalia Lazaro maskini aliyekuwa anatamani kupata hata makombo yaliyokuwa yanaanguka mezani pake. Alimtambua hata kwa jina, lakini hakuthubutu kumsaidia. Katika maisha yake alifunikwa na ubinafsi, uchoyo na ulafi wa fedha na mali, kiasi hata cha kushindwa kutubu na kumwongokea Mungu. Dhambi ilikwisha haribu maisha ya huyu tajiri kiasi kwamba hasingeweza tena kurejea nyuma! Aliona umaskini na maskini waliokuwa wanateseka mitaani pake, lakini yote haya akayapatia kisogo! Baada ya kifo anaomba huruma kwa Ibrahimu, Baba wa imani. Amelaaniwa mwanadamu anayejiamini kupita kiasi, huu ni ugonjwa unaompelekea mtu mahali pabaya.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, hata leo hii kuna watu wanaolala barabarani pasi na makazi; kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu ha hatarishi, daima wako mitaani, lakini wanapigwa mawe utadhani mbwa koko! Kuna watu ni watanashati, lakini hawana fedha ya kulipia pango la nyumba, na wala hawana mahali pa kupata mahitaji yao msingi. Haya ndiyo mazingira ambamo watu wengi wanaendelea kuishi kana kwamba, ni sehemu ya maisha ya kawaida! Baba Mtakatifu anasema hapa kuna hatari kubwa ya kutumbukia katika dhambi ya mazoea, mwaliko ni kujinyima ili kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Mdhambi anaweza kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza safari ya maisha yake ya kiroho! Lakini kwa mtu anayejiaminisha katika mali na utajiri wake, kamwe hataweza kuguswa na hali ngumu ya maisha ya maskini kama ilivyotokea kwa Lazaro. Baba Mtakatifu anawataka waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awapatie ujasiri wa kuchunguza dhamiri zao ili kuona kama wamepotoka, tayari kutubu na kumwongokea Mungu ili kuanza upya safari ya maisha ya kiroho. Hii iwe ni sala ya siku ya Alhamisi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.