2017-03-15 07:03:00

Ratiba elekezi ya Liturujia zinazoadhimishwa na Papa Francisko


Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada na Liturujia zinazoadhimishwa na Baba Mtakatifu Fracisko ametoa ratiba elekezi ya ibada na matukio makuu yakayoongozwa na Baba Mtakatifu kuanzia tarehe 17 Machi hadi tarehe 16 Aprili 2017, Kanisa litakapokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Pasaka kilele cha imani na matumaini ya Kikristo! Baba Mtakatifu Ijumaa, tarehe 17 Machi 2017 majira ya 11:00 za Jioni anatarajiwa kuongoza Ibada ya Kitubio kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Jumamosi tarehe 25 Machi 2017, Kanisa litaaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko atafanya ziara ya kitume ya Siku moja, Jimbo kuu la Milano, lililoko Kaskazini mwa Italia. Jumapili tarehe 2 Aprili, Domenika ya V ya Kipindi cha Kwaresima, Baba Mtakatifu Francisko atafanya hija ya kichungaji Jimboni Carpi na Mirandola, Kusini mwa Italia ili kuonesha upendo na mshikamano na wananchi walioathirika kwa kiasi kikubwa na tetemeko ka ardhi lililotokea katika maeneo haya kunako mwaka 2012.

Akiwa Jimboni humo, atabariki Jiwe la Msingi la Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Agatha, Nyumba ya Mafungo ya kiroho ya Mtakatifu Antonio. Baada ya Sala ya Malaika wa Bwana na Chakula cha Mchana kwenye Makao makuu ya Askofu wa Carpi, Baba Mtakatifu atakutana na wakleri, watawa na majandokasisi wakiwa wameongozana na Askofu Fracesco Cavina. Atatembelea Kanisa kuu la Jimbo la Carpi ambalo bado halitumiki kutokana na kuathiriwa na tetemeko la Mwaka 2012. Papa Francisko atazungumza na familia ya Mungu Jimboni humo na baadaye atakwenda kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbu kumbu ya watu waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi la mwaka 2012, mnara ambao uko kwenye Parokia Mtakatifu Giacomo Roncole, baadaye jioni atarejea tena mjini Vatican.

Tarehe 9 Aprili 2017 itakuwa ni Jumapili ya Matawi, Kanisa linapokumbuka Siku ile Yesu alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kubwa, huku watoto wa Wayahudi wakitandaza nguo zao kumshangalia. Huu utakuwa ni mwanzo wa Juma kuu na Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Kubariki Matawi na baadaye kufuatia maandamano ya matawi na mwishowe, kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, hii pia ni Siku ya Vijana Kijimbo kama sehemu ya maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani, itakayoadhimishwa huko Panamà kunako mwaka 2019. Ibada ya Misa Takatifu itaanza saa 4:00 kwa saa za Ulaya.

Tarehe 13 Aprili 2017, Alhamisi kuu, Majira ya Saa 3:30 Asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Haya ni mafuta yanayotumiwa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa: Mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka Wakatekumeni, waamini wanapoimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara; wanapokuwa wagonjwa na kwa wale wanaopewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Tarehe 14 Aprili 2017 ni Ijumaa Kuu! Majira ya Saa 11: 00 Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Neno la Mungu, Ibada ya Kuabudu Msalaba na hatimaye, waamini watapokea Ekaristi Takatifu. Saa 3:15 Usiku, Baba Mtakatifu ataongoza Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo. Jumamosi Kuu tarehe 15 Aprili 2017 Majira ya Saa 2:30 za Usiku, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza mkesha wa Siku kuu ya Pasaka. Jumapili tarehe 16 Aprili 2017, Siku kuu ya Pasaka, Kanisa linapokumbuka ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu; Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye atatoa Salam na Baraka za Pasaka kwa Mji wa Roma na Ulimwengu kwa ujumla kama zinavyofahamika kwa Lugha ya Kilatini “Urbi et Orbi”.

Ndugu msikilizaji, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa tayari kukushirikisha matukio yote haya katika taarifa zake. Lakini kwa wale wenye haraka zao wanaweza kutembelea tovuti ya Radio Vatican kwa anuani ifuatayo: www.radiovaticana.va Fungua Lugha ya Kiswahili, hapo utakuwa umefika, ili kukata kiu ya hamu yako ya matukio yote haya awamu kwa awamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.