2017-03-15 15:03:00

Hospitali ya Mt. Gaspari, Itigi, Oasisi ya huruma na upendo wa Mungu


Katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii nchini Tanzania (CSSC), yaliyofanyika hivi karibuni Jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Mtakatifu Gaspari, Itigi, Manyoni, Tanzania ilipewa tuzo ya kuwa ni kati ya hospitali tano bora nchini Tanzania kati ya 190 hospitali zinazosimamiwa na kuratibiwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii nchini Tanzania. Hii ni hospitali ambayo imetoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto wagonjwa kwa kujizatiti ili waweze kupata huduma na lishe bora kwa njia ya mradi wa elimu ya lishe bora unaotolewa hospitalini hapo. Huduma bora na makini; ut una heshima ya binadamu; huruma na upendo ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuipambanua hospitali ya Mtakatifu Gaspari kwa huduma makini.

Uchunguzi wa magonjwa ni katika huduma bora sana zinazotolewa na Hospitali ya Mtakatifu Gaspari, Itigi. Ili kuweza kukabiliana na changamoto za wahudumu, hospitali kunako mwaka 2006 ilianzisha Chuo cha Uuguzi cha Mtakatifu Gaspari ambacho pia kimekuwa kikifanya vyema katika taaluma pamoja na kuchangia weledi katika huduma kwa wagonjwa wanaohudumiwa hospitalini hapo! Chuo kimekuwa kikitoa cheti na diploma na kwamba, kwa sasa uwezo wa chuo ni kutoa mafunzo kwa wanafunzi 250. Taarifa zinaonesha kwamba, hiki ni kati ya vyuo vya uuguzi vinavyoendelea kucharuka nchini Tanzania kwa ubora!

Itakumbukwa kwamba, hii ni hospitali inayoendeshwa na kumilikiwa na Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania kwa lengo la kujibu kilio cha maskini kwa kutambua kwamba, Damu Azizi ya Kristo ni ufunuo na huruma ya Mungu kwa watu wake; ni damu inayoinua utu na heshima ya binadamu aliyedhohofishwa kwa dhambi; ni damu ambayo ni chemchemi ya haki na upendo wa Mungu kwa binadamu aliwahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II. Uamuzi wa kujenga hospitali hii anasema Padre Chesco Peter Msaga, Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu ni kutaka kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, ndiyo maana ikajengwa Itigi takribani miaka 30 iliyopita!

Padre Serafini Lesiriam, Mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspari hivi karibuni alisikika akisema, hospitali hii ina jumla ya wafanyakazi 296 kati yao kuna madaktari 11, wauguzi 90 na wengine waliobaki ni wafanyakazi katika vitengo mbali mbali vya huduma. Ni hospitali yenye changamoto zake, lakini bado inaendelea kutoa huduma makini kwa wagonjwa ndani na nje ya Kanda ya Kati nchini Tanzania. Dira ya hospitali hii ni kwamba, kitovu cha ufanisi wa huduma bora za afya na mafunzo kwa kuzingatia kanuni za Kanisa, zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Dhima ni kutoa huduma za hali ya juu za tiba, elimu na utafiti ulio makini kwa jamii zilizoko pembezoni kulingana na kanuni za Kanisa Katoliki. Licha ya mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatika katika hospitali ya Mtakatifu Gaspari, Itigi, bado kuna changamoto nyingi zinazopaswa kuvaliwa njuga na Shirika katika ujumla wake kwa kusaidiana na Serikali ili kuweza kupata madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto; kodi kubwa kwa serikali, gharama za umeme, dawa na vifaa tiba; fedha kwa ajili ya ukarabati pamoja na mishahara inayokidhi mahitaji msingi ya watumishi wa hospitali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.