2017-03-14 09:48:00

Waanglikani wasali masifu ya jioni kwenye Kanisa kuu la Mt. Petro!


Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Uekumene wa sala unaowapatia nafasi Wakristo kuweza kusali pamoja  kama njia ya kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili siku moja waweze kuwa wamoja kadiri ya mapenzi ya Kristo Yesu. Jumatatu tarehe 13 Machi 2017 kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki, Waamini wa Kanisa Anglikani mjini Roma wameadhimisha Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Askofu mkuu David Moxon, Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Kianglikani mjini Roma.

Tukio hili limekuwa na umuhimu wa pekee sana kwani hizi ni jitihada za Makanisa haya mawili kutaka kukoleza majadiliano ya kiekumene na kama kumbu kumbu ya miezi mitano tangu Baba Mtakatifu Francisko aliposali masifu ya jioni kwa kuungana na Askofu mkuu Justin Welby, Mkuu wa Kanisa Anglikani. Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti za Kanisa ndiye aliyetoa mahubiri katika tukio hili la kihistoria kuwahi kuadhimishwa kwenye kaburi la Mtakatifu Petro, mwamba wa imani. Hapa ni mahali muhimu sana kwa imani, maisha na utume wa Kanisa Katoliki; eneo takatifu linalotumika kwa Ibada inayowawezesha waamini kuonesha unyenyekevu na upendo wao kwa Mwenyezi Mungu.

Askofu mkuu Arthur Roche anakaza kusema unyenyekevu ni utambulisho wa Wakristo. Mtakatifu Gregory mkuu ni kati ya Mapapa wanaokumbukwa sana na Mama Kanisa kwa kuacha urithi mkubwa katika maisha na utume wake. Ni kiongozi aliyetumia karama na mapaji yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Alikuwa ni mtu wa sala, tafakari, mtii na mnyofu katika huduma. Alijipambanua kuwa ni kiongozi mahiri wa Kanisa katika masuala ya sheria yanayofumbatwa kwa namna ya pekee katika hekima na busara, daima akipania kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa: watumwa, maskini, wafungwa, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji. Tunu hizi zikamwezesha kupeta katika maisha ya kiroho na kisiasa.

Askofu mkuu Arthur Roche anasema, Papa Gregory mkuu alijipambanua kuwa ni mhimili mkuu katika mchakato wa uekumene kwa kutambua kwamba, Ukuu wa Mtakatifu Petro ulikuwa unafumbatwa katika huduma, kwani kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alikuwa ni “Servus servorum Dei” yaani, mtumishi wa watumishi wa Mungu, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kujitahidi kuwa ni watumishi wa huduma kwa jirani zao, daima wakiendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo watambue kwamba, wao ni watumwa wasio na faida; wanafanya yale tu wanayopaswa kufanya! Lengo ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha Imani ya Kanisa.

Askofu mkuu Arthur Roche anaendelea kusema kwamba, Papa Gregory mkuu alijipambanua kuwa na ari na mwamko wa kimissionari, kiasi cha kuthubutu kuwatuma Mapadre kama Mtakatifu Augostino wa Canteburry kwenda kutangaza na kushuhudia Imani; chachu ya Injili ikazaa matunda ya toba na wongofu wa ndani kwa Ulaya ya Kaskazini kuongoka na kumwambata Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu. Kanisa limeanzishwa ili kutoka tayari kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Uinjilishaji huu ulitekelezwa hata kwa njia ya muziki mtakatifu.

Kristo Yesu ni kiini cha imani ya Wakristo wanaohamasishwa kushikamana tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wakristo wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe, tayari kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza na kuwatia shime ili kuvuka vikwazo vinavyoendelea kukwamisha mchakato mzima wa Uekumene. Jitihada hizi zifanywe katika hali ya unyenyekevu mkuu pasi na haraka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.