2017-03-14 14:40:00

Papa Francisko: Jifunzeni kutenda mema!


Nabii Isaya anawahamasisha waamini kujiosha na kujitakasa; kuondokana na uovu wa matendo yao ili usiwe mbele ya Mwenyezi Mungu; waache kutenda mabaya na kuanza kujifunza kutenda mema; kwa kutoa hukumu ya haki, kwa kuwasaidia walionewa, kwa kumpatia yatima haki yake na kumtetea mjane. Hivi ndivyo Neno la Mungu linavyopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini kwani maneno matupu kamwe hayawezi kuvunja mfupa! Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa takatifu, Jumanne, tarehe14 Machi 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki cha Kwaresima. Watakatifu ambao kimsingi ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu walitenda dhambi, lakini daima walikimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaondokana na tabia ya kuishi katika dhambi za mazoea. Waamini wajifunze kutenda mema na kwamba, huuu ni mchakato wa kila siku katika maisha ya waamini kama ilivyo kwa watoto wadogo. Kujifunza kutenda mema ni sheria na kanuni ya toba na wongofu wa ndani, safari ndefu katika maisha.

Waamini wajitahidi kukimbia dhambi na nafasi zake kwa kujifunza kutenda mema si tu kwa maneno, bali maneno yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mtu! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma, upendo na mshikamano; mambo yanayomwilishwa katika maisha ya watu! Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa wao wanasema lakini hawatendi jambo ambalo ni vigumu sana kupata wongofu wa ndani. Yesu anawaalika watu kuzungumza na kujadiliana naye kama alivyofanya kwa yule kiwete aliyekuwa hawezi, mtoto wa Yairo na Mtoto wa yule mama wa Naini.

Mwenyezi Mungu anashika mkono waje wake na kuwanyanyua juu kama mlingoti wa bendera. Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kumsaidia mwamini kuongoka, muujiza unaofanyika katika hija ya maisha ya mwamini! Kumbe, mambo makuu yanayopaswa kupewa mkazo katika mchakato wa wongofu wa ndani ni kukimbia dhambi na nafasi zake sanjari na kuanza kujifunza kutenda mema! Waamini wawe na ujasiri wa kujadiliana na Kristo Yesu katika maisha yao, licha ya mapungufu na udhaifu wao wa kibinadamu, kwani hata kama dhambi zao ni nyekundu kiasi gani, zitaweza kusafishwa na kuwa nyeupe kuliko theluji.

Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo safari ya toba na wongofu wa ndani wakati huu wa Kwaresima kwani Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake kutoka katika undani wa maisha yao. Huyu ni Mungu anayewatakia mema watoto wake kwa kuwasindikiza katika safari ya toba na wongofu wa ndani, changamoto kwa waamini ni kujivika fadhila ya unyenyekevu, ili aweze kuwanyanyua juu kama tai shingoni! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kusema hii ndiyo hija ya toba na wongofu wa ndani katika kipindi hiki cha Kwaresima, ili kupata msamaha na maondoleo ya dhambi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.