2017-03-13 11:26:00

Ukuu na utukufu wa Yesu unafumbatwa katika Fumbo la Msalaba!


Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya pili ya Kipindi cha Kwaresima inasimulia jinsi ambavyo Yesu alivyowachukua mitume wake watatu yaani: Petro, Yakobo na Yohane wakajitenga na hapo akang’ara sura mbele, kiasi cha kuwafunulia ukuu, utukufu na utakatifu wake ambao walipaswa kuupokea kwa njia ya imani, mahubiri pamoja na miujiza mbali mbali aliyotenda katika maisha yake. Tukio la kung’ara kwa Yesu linasindikizwa na uwepo wa Musa na Eliya waliokuwa wanazungumza na Yesu, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii. Mwanga angavu uliokuwa kiini cha tukio hili ni kielelezo cha mwanga unaopaswa kuangaza akili na mioyo ya Mitume wa Yesu ili waweze kumfahamu Bwana wao. Ni mwanga unaoangaza Fumbo la maisha ya Yesu na hivyo, kufunua maisha na utume wake wote!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 12 Machi 2017 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Yesu aling’ara sura yake mbele ya Mitume wake, wakati alipokuwa anajiandaa kupanda kwenda Yerusalemu, ambako angehukumiwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani. Yesu alitumia fursa hii kuwaandaa kuipokea kashfa ya Msalaba iliyokuwa na nguvu kubwa sana kiasi hata cha kutikisa msingi wa imani yao, ili hatimaye, kuwatangazia ufufuko wake na hivyo kuonesha kuwa kweli alikuwa ni Masiha, Mwana wa Mungu aliye hai.

Yesu aliwaandaa mitume wake kikamilifu kwa ajili ya kulipokea Fumbo la Msalaba, kwa kujionesha kuwa ni Masiha ambaye alikuwa ni Mtumishi mnyenyekevu na asiye na nguvu kinyume cha matarajio yao ya kuwa na Masiha: mtawala na mwenye nguvu; mtu wa kawaida asiyekuwa na utajiri ambao kimsingi ilikuwa ni alama ya baraka ya Mungu, bali mtu wa kawaida asiyekuwa hata na mahali pa kulaza kichwa chake; Mseja asiyekuwa na nyumba wala kiota; ufunuo wa Mungu uliowaacha watu wengi wakiwa wamepigwa na bumbuwazi na hasa zaidi kwa kashfa ya Msalaba.

Lakini, Baba Mtakatifu anasema, ni kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu ataweza kufikia kilele cha ufunuo wa: ukuu, utukufu na utakatifu wake ambao utadumu milele yote kwa njia ya Fumbo la Ufufuko wake. Yesu kwa kung’ara uso wake pale juu mlimani Tabor amewafunulia wafuasi wake utukufu wake unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, ili kuwaonesha Njia ya Msalaba inayowapeleka kwenye utukufu wake. Anayekufa na Kristo, huyo atafufuta pia pamoja na Kristo; anayeshikamana na Kristo katika mapambano, huyo atashinda pamoja na Kristo.

Baba Mtakatifu anafafanua zaidi kwa kusema, huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Waamini watambue ukuu wa Msalaba na wala si tu kama kito cha thamani wanachovaa shingoni au kupamba nyumbani kwao, bali ni dira na mwaliko wa kuutafakari upendo wa Yesu aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwaresima iwasaidie waamini kutambua na kuthamini ukuu wa Msalaba, madhara ya dhambi na thamani ya mateso ya Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa watu wote. Baba Mtakatifu anahitimisha tafakari yake kwa kusema, Bikira Maria aliyetafakari utukufu wa Yesu uliokuwa umefumbatwa katika ubinadamu wake, awasaidie waamini kukaa pamoja na Yesu katika sala kwa kumpatia nafasi ili aweze kuangaza giza la mioyo yao ili hatimaye, waweze kuutafakari ukuu, utukufu na utakatifu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.