2017-03-13 11:42:00

Papa Francisko: Sikilizeni kilio cha watoto wanaonyanyasika duniani!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 12 Machi 2017 aliyaelekeza mawazo yake nchini Guatemala ili kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wananchi hao ambao kwa sasa wanaomboleza baada ya nyumba ya “Refugio Virgen de la Asunción” kushika moto na kusababisha vijana kadhaa kupoteza maisha na wengine wengi kupata majeraha makubwa. Baba Mtakatifu anaziombea roho za wale wote waliofariki dunia katika ajali hii na anapenda kuzifariji familia zote zilizotikiswa na msiba huu mzito nchini Guatemala.

Baba Mtakatifu amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye kwa sala ili kuwakumbuka vijana ambao wamekuwa ni wahanga wa: vita, vitendo vya makosa ya jinai, vurugu, nyanyaso na unyonyaji. Hili ni donda kubwa dhidi ya ubinadamu; ni kilio ambacho kinapaswa kusikilizwa kwa makini na kukipatia jibu muafaka na kamwe watu hawawezi kuziba masikio yao na kujifanya kana kwamba, hawaoni wala kusikia kile kinachotendeka mbele yao! Umefika wakati wa kukataa katu katu utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine!

Taarifa kutoka Guatemala zinasema kwamba, moto huu pengine ulisababishwa na baadhi ya wasichana 52 waliokuwa wamefungiwa darasani na kupewa magodoro ili wayatumie wakati wa usiku. Kati ya wasichana hawa, 40 wanasadikiwa kwamba, wamefariki dunia baada ya kuunguzwa na moto na wengine waliobakia wamepata majeraha makubwa na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Roosevelt. Serikali nchini Guatemala imetangaza kufanya marekebisho makubwa katika huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Wasichana hawa walikuwa wanatunzwa kwenye Kituo cha “Refugio Virgen de la Asunción”, makazi kwa watoto ambao wamekumbana na nyanyaso za kijinsia; watoto wanaotoka katika familia maskini na wakati mwingine ni watoto ambao wanatunzwa hapo kwa amri ya Polisi. Wananchi wanaoishi katika maeneo haya wanasema, watoto hawa wanaishi katika mazingira ambayo ni kinyume kabisa cha haki msingi, utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.