2017-03-11 11:00:00

Je, mnawakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaodhulumiwa?


Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Machi 2017, anauliza swali la msingi, Je, ni wangapi kati yenu wanaokumbuka kusali kwa ajili ya kuwaombea  Wakristo wanaoteswa na kunyanyaswa sehemu mbali mbali za dunia? Nia hii ya Baba Mtakatifu husambazwa na mtandao wa utume wa sala, unaowahamasisha waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuungana na Baba Mtakatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kusali kwa ajili ya Wakristo wanaodhulumiwa na kuteswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni watu wanaopaswa kusaidiwa na Makanisa na Jumuiya za Waamini kwa hali na mali.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tema anayozungumzia kwa Mwezi Machi ni tete sana kwani kuna maelfu ya watu wanaodhulumiwa, kuteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa. Watu wanalazimika kuyakimbia makazi yao; maeneo ya ibada pamoja na kuwapatia kisogo wapendwa na wajuani wao na hatimaye kutokomea mahali wasikojua hatima ya maisha yao. Watu hawa wanateswa na baadaye kuuwawa kikatili kwa vile tu ni wafuasi wa Kristo Yesu, yaani hawa ni Wakristo!

Baba Mtakatifu asema huu ndio uekumene wa damu, kwani wale wanaowadhulumu hawatofautishi Makanaisa wala madhehebu yao: kwamba, hawa ni: Wakatoliki, Waorthodox, Waanglikani, Waluteri au waamini wa Makanisa ya Kipentekoste. Wote hawa wanatambulikana kuwa ni Wakristo! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaoteswa na kunyanyaswa sehemu mbali mbali za dunia. Nia hii ya Baba Mtakatifu inasindikizwa na picha za Makanisa yaliyochomwa moto na watu wanaotendewa unyama, ili kuvuta hisia kwa Jumuiya ya Kimataifa iweze kuona na kutenda, kwa ajili ya kuwasaidia maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.