2017-03-09 15:00:00

Kwaresima ni safari ya imani na matumaini kuelekea utukufu wa Mungu


Kipindi cha Kwaresima ni safari ya kiroho yenye dhamira ya kuturudisha kwa Mungu. Ni fursa nyeti kwetu ambayo inatugutusha na kutuwezesha kuona kwamba tupo nje ya mstari. Hivyo tunapewa nafasi hii muhimu sana kwa ajili ya kuitikia sauti ya Mungu ambayo hutuita tena kupitia njia mbalimbali za kichungaji ambazo hulenga kuifufua dhamira ya mtu na kulitambua kusudio ya kuumbwa kwake, yaani kuelekea katika: ukuu, utakatifu na utukufu wa Mungu. Mungu anapotuita ananuia kutupatia ujumbe wake, mwitikio wetu kwa sauti yake utufikisha katika kuuonja utukufu wake.

Dominika ya pili ya majira ya Kwaresima inatufunulia utukufu wa Mungu ambamo sote tunaalikwa kuchuchumilia na kuufikia. Neno la Mungu linatuwekea mbele yetu safari hiyo ya kiroho kupitia wahusika wawili: Abraham Baba yetu wa imani katika somo la kwanza na Kristo katika somo la Injili. Abraham anaitwa kuifanya safari hiyo ya kiroho: “toka wewe katika nchi yako ... mpaka nchi nitakayokuonesha”. Kwa imani kama Waraka kwa Waebrania unavyomdadavua anaanza safari hiyo kuielekea ahadi ya Mungu.

Abraham anaitwa kutoka katika nchi yake, anaelekezwa kuacha yote hata ndugu zake na kwenda mahali atakapoelekezwa na Mungu. Kwaresima inaanza kwa kutupatia mwaliko wa kutoka katika nchi yetu. Nchi yako au nchi yangu ni mahali panaponitambulisha, ni mahali palipo na yale niliyoyazoea, ni mahali ambapo wapo wapendwa wengi ambao tumezoeana na kushibana, ni mahali ambapo zipo taratibu nyingi ambazo zimekwisha kuwa sehemu ya maisha yangu. Katika safari hii ya Kwaresima ninaitwa kwa kuambiwa toka mahali huko na kwenda mahali ambapo Mungu atakuonesha.

Nchi yangu yaweza kutamalakiwa na maadui watatu tuliotafakari juma lililopita na kutufanya kumweka Mungu pembeni. Kwa kujikumbusha maadui hao ni mahitaji muhimu ya kimwili, ulinzi na usalama wangu na mali na madaraka ya dunia. Ninaweza kubobea katika himaya za maadui hawa na kufungwa kabisa kiasi ambacho nikajijenga katika ubinafsi na kujijali mwenyewe bila kuthubutu kufungua macho na kuwangalia wengine. Nchi yangu imejaliwa na starehe nyingi tamutamu, mali nyingi zinazofurahisha mwili na akili, madaraka na heshima kedekede ambazo zinanifanya nijione naelea katika ulimwengu wa raha na starehe hata nisitamani kuguswa mithili ya “teja” aliyepata dozi kidogo ya dawa za kulevya. Au mlevi aliyebugia viroba!

Katika jamii ya leo mwanadamu amejifungia zaidi katika ulimwengu wake na kutokuwa tayari kujipatanisha na wengine. Hakuna mahusiano mazuri katika familia zetu na hata katika jamii kubwa ya mwanadamu. Neno msamaha na upatanisho kati yetu ni aghalabu kuonekana. Twajifungia na kujidanganya kwa mafanikio bandia tunayoyapata. Hii nayo tunaweza kuitambua kama nchi yetu ambayo tupo, nchi ambayo tunaalikwa tutoke na kujipatanisha na wengine. Utu wa mtu umesulubishwa vya kutosha sababu ya ubinafsi wetu na kutokuwa tayari kujifunua kwa wengine. Mimi kwanza, mahitaji yangu kwanza na usalama wangu kwanza. Sipo tayari kupatana na yule anayeniingilia anga zangu. Ama zake au ama zangu.

Dhambi hutuwekea utamu na kutokuwa na ujasiri kama wa Abraham wa kuamua kutoka. Tunashindwa kuisikiliza sauti ya Mungu kwa kuwa tunaona na kujiaminisha kwamba, mambo haya ya ulimwengu yametung’arisha vilivyo. Ndiyo! Ni kweli! Maana kila mmoja anashuhudia tunavyoshamiri na kukua katika biashara zetu; tunavyoendelea kula “bata hadi kuku wakitushangaa”. Katika mazingira haya unataka tutafute utukufu gani tena? Tung’arishwe na nini tena? Kipindi cha Kwaresima kinatukumbusha kuwa huko tulipo si kwetu na utukufu wake ni wa kupita. Tunarudishwa nyuma na kutafakari juu ya wale waliong’aa na kutamba kidunia lakini wakaishia kuangamia. Tunaalikwa kuutafuta utukufu mkuu wa Mungu, utukufu ambao hautatuadaa.

Kwa imani Baba yetu wa imani Ibrahim alitoka katika nchi yake na kuifikia nchi ambayo Mungu alimwonesha. Safari yake hiyo ilikuwa inatuandaa sisi wanadamu kusafiri kwa pamoja huku tukiongozwa na Mungu na kuufikia utukufu wa kweli wa Mungu ambao kilele chake ni maisha ya kipasaka. Kristo anaufunua utukufu huo leo hii kwa kung’ara sura. Tukio hilo linamtambulisha kama Mwana mpendwa wa Mungu: “Huyu ni mwanangu mpendwa wangu, msikieni yeye”. Hili ndilo lengo la safari hii ya kiroho wakati wa majira haya ya Kwaresima, yaani kuifikia sikukuu ya Pasaka ambayo kwayo tutaipokea hadhi ya kuwa wana wa Mungu na kung’aa katika utukufu wa kweli.

Kristo anaifunua ahadi ya Mungu kwa Abraham na kuuonesha utukufu wake; kupanda juu mlimani ni udhihirisho wa kiuinuliwa kwa hadhi yetu kutoka katika ardhi chini na kufanywa yenye utukufu mkuu; kufanyika kuwa watoto wa Mungu. Imani na matumaini kwa Mungu vinaonekana pia hapa. Kwa hakika tendo hilo la kupanda juu mlimani linadokeza kufanyika kwa jitihada fulani. Tendo la kupanda mlima si lele mama. Tendo hili linachosha na kukera lakini mwisho wake ni furaha kwani aliye kileleni anayo nafasi ya kupata mwanga na nuru zaidi na wakati mwingine hewa nzuri. Ndivyo nasi tutakapoitikia wito wa Mungu kipindi hiki cha Kwaresima na kupanda pamoja na Kristo hakika tutaufikia utukufu wake na kuuonja.

Jibu kwa shahuku ya mtume Petro linatupatia fundisho muhimu. Baada ya kuuonja furaha ya utukufu wa kweli Petro alitamani kujenga vibanda mahali pale kuashiria nia ya kubaki katika hali hiyo ya utukufu. Nia hiyo ni njema. Petro na wenzake wakiwa katika shahuku hiyo sauti ilisikika ikiwaambia: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye”. Hapa tunaambiwa kwa namna nyingine kwamba utukufu huu si wa kuupokea tu burebure bali unahitaji ufuasi: “msikieni yeye”. Uaminifu wetu katika ufuasi, yaani katika kulisikia Neno la Mungu ambalo Kristo ni kilele cha ufunuo wake ndiyo hakika kwetu kuupata utukufu wa Mungu. Ndiyo namna ya kutuondoa katika njia yetu na kwenda mahali pale tulipoandaliwa. Ndiyo namna ya kutuinua hadhi yetu.

Kristo anatambua wazi kuwa sifa hiyo ya kuwa Mwana mpendwa wa Mungu itajidhihirisha wazi katika ukamilifu wa fumbo la Pasaka na ndiyo maana anawakataza kwa kuwaambia: “msimwambie mtu yeyote habari ya maono haya, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu”. Kwa fumbo la Pasaka Kristo anaturudishia hadhi yetu ya kuwa wana wa Mungu ambayo ilijeruiwa na dhambi. Dhambi inatuondoa katika utukufu huo na hivyo mwaliko wa kutubu wakati wa kipindi hiki cha Kwaresima ni dhahiri mwaliko wa kurudi tena katika utukufu wa Mungu. Mtume Paulo anauonesha wito huo  kuwa ni “mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa makusudi yake Mungu na neema yake”.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.