2017-03-08 15:57:00

Mashuhuda wa ukuu na utukufu wa Mungu!


Ndugu yangu! Kipepeo kinapitia mabadiliko makubwa kutoka umbo la kiwavi kisha kifukofuko kinachoonekana kutokuwa na umbo zuri wala uhai ndipo kinabadilika kuwa kipepeo kizuri kinachoruka angani. Mabadiliko anayopitia kipepeo yanaitwa metamorphothe kutokana na maneno mawili ya Kigiriki meta ni mabadiliko  na morphe ni umbo. Kwa kiingereza yanaitwa metamorphoses. Injili ya dominika ya leo ya kwaresima ni ya Kungara sura Bwana wetu Yesu Kristo. Hapa limetumika neno metamorphose yaani kubadilika. Ili kuelewa vyema metamorphoses au mabadiliko hayo aliyopitia Yesu tuone kwanza mazingira yake.

Injili ya leo inaanza hivi: “Na baada ya siku sita.” Kumbe, kabla ya hizi siku hizo Yesu alikuwa Kaisaria-Filipi alikowauliza wanafunzi wake: “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Simoni Petro akajibu: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Baada ya jibu hilo, Yesu “akawatonya” kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi na kuuawa, lakini atafufuka siku ya tatu!. Hapo Petro akamchukua Yesu kando na kumkemea asilogwe wala kuthubutu kufanya hivyo. Ndipo Yesu alipomgeukia Petro na kumwambia: “Nenda nyuma yangu, Ibilisi.” Petro anaitwa Ibilisi kwa sababu hafikiri kadiri ya Mungu bali kadiri ya fikra za ulimwengu alinusa kuanguka kwa nafasi yake kama mwamba!. Kwa hiyo katika siku hizi sita, Yesu alijionesha kuwa ameshindwa, alikuwa kama kifukofuko tu.

Injili ya leo inaendelea kusema: “Yesu akawatwaa Petro na Yakobo, na Yohane ndugu yake, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani.”  Wanafunzi wanapelekwa faraghani. Mlima huo siyo wa kihistoria (Tabor) bali ni mlima wa kitaalimungu. Lengo lake ni kutuletea mang’amuzi ya mabadiliko metamorphose ya imani waliyoanza kuyaona wanafunzi baada ya kuishi na Yesu kwa kina. Wanafunzi hawahawa tutawakuta tena Getsemani walikomshuhudia Yesu anavyoona uchungu mkali na kuogopa, alikoonekana kama kifukofuko kiasi hata cha kutoka jasho la damu!. Huko faraghani “Yesu aligeuka sura mbele yao,” Kadhalika kama sisi tunataka kuona mabadiliko metamorphose hiyo yatubidi tujitenge na ulimwengu na kumfuata Yesu faraghani.

Yesu wa Nazareti, mwenye umbo la kibinadamu sasa anabadilika. Sisi pia ni binadamu tulio na mwili unaonja magumu, shida na hatimaye mwili unaokufa. Lakini mwili huu ni pia pazia linalotuzuia kuiona hali halisi ya hadhi yetu ya uwana wa Mungu inayojidhihirisha katika matendo ya huruma na upendo wa Mungu kwetu sisi binadamu. Metamorphose inayotokea kwa Yesu ni kwamba, ubinadamu wake uliokuwa wa utumwa na utumishi, ulibadilka kabisa machoni pa Mungu. Kwa hiyo mng’aro au metamorphose ni kufunua pazia ili kuona hadhi na mng’aro halisi ya mwana wa Mungu, yaani kuuona ukuu na utakatifu wa Mungu kwa macho makavu!. Wanafunzi wakaanza kuona uso wa Yesu “uking’aa kama jua na mavazi yake meupe kama nuru.” Jua ni alama ya utukufu wa Mungu ni jua la haki. 

Nuru ni picha ya Umungu. Kila binadamu anao mwanga na nuru ya umungu ndani mwake, lakini pia kuna pazia linalotuzuia kuona uhalisia wa mwanga huo. Injili ya Yesu inatualika daima kufanya metamorphose au mabadiliko hayo. Mathalani, maingilio ya Injili ya Yohane yanasema: “Nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama Mwana wa pekee atokaye kwa Baba amejaa neema na kweli.” (Yoh1:14). Haya ni mang’amuzi ya metamorphose kwa yule aliyeonekana ameshindwa kumbe wameona ushindi yaani utukufu. Kadhalika Paulo anasema: “mwanga unang’ara gizani, unaingia katika mioyo yetu ili kufanya uangaze utukufu wa Mungu, inayong’ara katika uso wa Kristu.” (II Wakor. 4) Hayo ni mang’amuzi ya Paulo ambaye mwanzoni alimwona Yesu kama kifukofuko na mzushi, aliyeshindwa kumbe baadaye akaona mabadiliko (metamorphose) yaani uso wa mtumishi halisi na wa Mwana kweli wa Mungu.

Kisha tunasikia: “Akatokea Musa na Eliya wakizungumza na Yesu” Hapa tunaona Metamorphoses nyingine. Katika agano la kale Wayahudi walimsubiri Masiha aliyeandikwa katika sheria ya Musa na katika unabii wa Eliya mashuhuda wa ufunuo wa kweli wa Mungu. Musa alitaka kuona uso wa Mungu, lakini akaambiwa hataweza kufunuliwa utukufu wa Mungu bali atakapopita atamfunika Musa uso kwa mkono. Baada ya kupita angetoa mkono na kuufunua uso wake naye Musa angeona mabega tu ya Mungu. Kumbe Mungu anaudhihirisha utukufu wake baada ya kupita, yaani baada ya kuonesha matendo aliyofanya ndipo mmoja unaweza kugundua utukufu wake. Kadhalika Eliya hakuweza kuuona uso wa Mungu katika mtetemeko na radi kule mlimani Horebu bali katika sauti tulivu sana. Hii ndiyo maana ya watu hawa wawili wanaojitokeza wakizungumza na Yesu yaani maandalizi ya mabadiliko metamorphose ya kumwona binadamu aliyeandaliwa na Agano la kale. Wanafunzi hawa watatu wa Yesu ndiyo wanaanza kuona mabadiliko metamorphose ya ufunuo huo.

Kisha Petro anasema:“Bwana! ni vizuri sisi kuwapo hapa, ukitaka nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa na kimoja cha Eliya.” Petro hakujua kwamba amepata fursa ile ya kukwea mlimani ili awe na mang’amuzi ya metamorphose mabadiliko ya Mwana wa Mungu, halafu ashuke bondeni waliko wengine na akayaishi mang’amuzi yale ulimwenguni. Kadhalika yabidi ikumbukwe kwamba hakuchukuliwa mtu mmoja faraghani bali walikuwa wanafunzi watatu, kumaanisha jumuiya. Mang’amuzi haya ya jumuiya ni sawa na yale tunayopata tunapokuwa pamoja Kanisani wakati wa Misa takatifu. Tunakutana na wengi na tunapata mang’amuzi ya mabadiliko (metamorphose) ya kimungu. Baada ya kupata mang’amuzi ya iwana wa Mungu katika sala ya liturjia inabidi turudi ulimwengu kuendelea kuishi vizuri.

Kumbe, Petro anapoendelea kuweweseka: “Tazama wingu jeupe likawatia uvuli.”  Hii ni tungo tata, eti wingu jeupe halafu linatia kivuli.  Kulikoni? Kwa sababu kama kuna wingu basi ni giza, kumbe hilo ni wingu jeupe linalong’aa. Hapa inaonesha kuwa huwezi kuelewa kikamilifu Fumbo hili la mabadiliko yaani metamorphose.  Kumbe huwezi kuuelewa kabisa ulimwengu wa Mungu. Daima unabaki upande wa giza na uvuli usioonekana waziwazi. Wingu ni ulimwengu wa Mungu ndiyo maana kunasikika sauti inayotuonesha huyo Yesu wa Nazareti: “Huyo ni mwanangu mpendwa wangu ninayependezwa naye.” Sauti hii imesikika mara mbili. Mosi, wakati wa Ubatizo wake Yohane alipokataa kumbatiza Yesu, akiwa na uhakika kwamba Mwana wa Mungu hawezi kuwa pamoja na wadhambi yaani kifukofuko. Kumbe kutokana na unyenyekevu wake  na ukifukofuko wake wa kujiweka pamoja na wadhambi unapata mabadiliko metamorphose yaani anang’ara na anakuwa mwana mpendwa wa Baba. Mara ya pili ni fasuli ya leo. Mungu ayeonekana katika Yesu anatualika: “Msikilizeni yeye.” Kumsikiliza Yesu maana yake kupokea mapendekezo yake ya maisha na kuanza kuyamwilisha kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Kuona mabadiliko yanayotokana na Msalaba kunadai kuwa na imani na moyo mkuu. Kadhalika binadamu unapopata pendekezo hilo la Yesu wa Nazareti juu ya mateso na kifo unaogopa. Mapato yake “wanafunzi walianguka kifulifuli na wakaogopa sana.” Lakini Yesu anawakaribia na kuwagusa akiwaambia “amkeni msiogope.” Lakini “Wanafunzi walipoinua macho yao hawakumwona yeyote isipokuwa Yesu peke yake.” Musa na Eliya walikuwa na kazi moja ya kuandaa ujio wa mwanga. Sasa baada ya kuja mwanga huo anabaki Yesu wa Nazareti peke yake. Wanafunzi wanatambua hilo baada ya kuinua macho yao. Tendo la “kuinua macho” linatokea mara nyingi katika Biblia. Mmoja anapoinua macho yake anaona kitu kizuri. Kwa mfano Abrahamu alipoinua macho kuangalia nyota angani akapata ahadi ya uzao usio na mwisho. Kadhalika Musa anakwenda mlima Pisgar ili kutafakari nchi atakayotoa Mungu kwa ajili ya watu wake.

Katika Injili Yesu anainua macho angani na kumponya kipofu. Aidha anainua macho na kumwona Zakeo mtini. Nasi tunaalikwa kuinua macho yetu mbinguni ili kuona mabadili ya mambo kama vile amani na upendo ulimwenguni. Kisha wanafunzi na Yesu walirudi na kuanza tena maisha ya kawaida baada ya kuwa na mang’amuzi haya ya metamorphosi (mabadiliko) pamoja na Yesu faraghani. Mabadiliko hayo yabidi hata sisi kuyafanya baada ya kugundua hadhi ya kweli ya Yesu wa Nazareti, iliyofunikwa na pazia la ubinadamu na baadaye turudi kwa ndugu zetu tukaakisi mwanga uleule tuliotafakari juu uso wa Yesu. Kama sisi tukiwa watumishi wa wenzetu hivi hata wao wataweza kupokea mwanga wa metamorphosi ya mtu halisi aliyejifanya mtumishi na kuwa Mwana wa Mungu aliye hai.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.