2017-03-08 14:01:00

Jimbo kuu la Dar lazindua Jubilei ya Miaka 100 ya B. Maria wa Fatima


Baba Mtakatifu Francisko anasema Kanisa katika ulimwengu mamboleo ni Kanisa la mashuhuda ambalo linaendelea kujengwa kutokana na damu ya watoto wake inayomwagika sehemu mbali mbali za dunia. Kuna watu wanauwawa, wanayanyaswa na kudhulumiwa kutokana na chuki za kidini. Huu ndio ukweli uliokuwa umefumbatwa katika ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, yaani Francis, Lucia na Yacinta hawa wakawa ni vyombo na mashuhuda wa “Siri ya Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima”. Kumbe, Bikira Maria ni alama ya matumaini kwa sasa na kwa siku za baadaye! Ni Siri inayogusa matukio ya kihistoria, maisha na utume wa Kanisa.

Mwaka 2017 Kanisa linaadhimisha kilele cha miaka 100 tangu Bikira Maria wa Fatima alipowatokea Watoto wa Fatima Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki na Serikali ya Ureno kutembelea nchini humo, kuanzia tarehe 12- 13 Mei 2017 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Karne Moja, tangu Bikira Maria wa Fatima alipowatokea watoto watatu wa Fatima. Papa Francisko anaendelea kukaza akisema hata leo hii, Kanisa linaendelea kujaribiwa, kwa baadhi ya watu kutaka kujenga hisia za chuki na uhasama dhidi ya Kanisa sanjari na kupandikiza mbegu ya kifo. Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima, aliwapatia Siri kuu tatu ambazo zote zimekwisha fafanuliwa na viongozi wa Kanisa kwa wakati wake. Ni siri ambazo zimejikita katika mwono wa vita, majanga, kinzani na migawanyiko kati ya watu. Siri zote hizi ziliandikwa na Sr. Lucia.

Mtakatifu Yohane Paulo II baada ya jaribio la kutaka kumuua kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro hapo tarehe 13 Mei 1981 aliamuru kwamba, siri ya tatu ifunuliwe na kuwekwa hadharani. Tafsiri ya siri hii ilitolewa na Kardinali Joseph Ratzinger, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, na alisema kwamba, siri ya tatu ya Fatima ilikuwa ni mwaliko kwa Wakristo kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa njia ya ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake!

Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, hivi karibuni amezindua maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, changamoto kwa wakati huu anasema ni kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini wawe tayari kumwachia Mwenyezi Mungu awaguse kwa na neema yake na hivyo kumwachia nafasi ya kuweza kuwaletea mabadiliko katika maisha yao.

Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano bora wa kuigwa katika: imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Waamini wajifunze kumfahamu Kristo Yesu kwa njia ya shule ya Bikira Maria ili kuachana na dhambi pamoja na nafasi zake, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, aliye njia, ukweli na uzima. Bikira Maria ni Mama aliyeguswa na mahangaiko ya watu, akawawa tayari kuyawasilisha mbele ya Yesu ili kuyapatia majibu muafaka, waamini wawe na ujasiri wa kujivika unyenyekevu, bidii na uaminifu wanapotoa huduma kwa jirani zao. Katika shida, mahangaiko na magumu ya maisha, waamini wawe tayari kuyatafakari yote haya na kuyahifadhi katika sakafu ya mioyo yao kwa imani na matumaini kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria hata mbele ya mateso na kifo cha Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo! Waamini wajitaabishe kumkimbilia Bikira Maria katika maisha yao, ili aweze kuwaonesha njia inayokwenda kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia.

Kumbe, Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima iwe ni fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu; wakati muafaka wa kushuhudia imani yenye mvuto na mashiko kwa Kristo na Kanisa lake ni wakati uliokubalika wa kumwilisha imani katika matendo kwa njia ya unyenyekevu na moyo mkuu anasema Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Na Pascal Mwanache, Dar es Salaam.

Na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.