2017-03-06 07:29:00

Ushauri wa Ibilisi na Majibu makini ya Yesu Jangwani!


Mara nyingi picha ya Ibilisi ni ya kutisha, kuchukiza na wala haina mvuto wala mashiko, lakini cha kushangaza bado watu wanajaribiwa na kuburuzwa na Ibilisi huyu! Mbaya zaidi katika Biblia kitabu cha mwanzo Ibilisi anaoneshwa kuwa ni nyoka mwenye sumu ya kufisha. Kama Ibilisi angekuwa hivyo kweli, basi watu wasingemfuata. Ndugu zangu, Ibilisi anavutia sana, ni kama rafiki anayekutakia mema, anakupa ushauri na anataka kukusaidia ili ufanikiwe katika maisha. Katika mapokeo ya zamani nyoka aliwakilisha mambo mawili. Mosi, alikuwa alama ya kifo kutokana na sumu yake inayofisha. Pili, alikuwa ni alama ya uzima usio na mwisho, kutokana na ukimya wake na hali yake ya kujichubua magamba na kuonekana daima mpya na mwenye uhai. Leo hii wangesema, nyoka daima anaonekana kama “baby”. 

Picha hizi mbili za nyoka ndizo zilizochukuliwa katika sura ya tatu ya kitabu cha mwanzo cha biblia. Kwa upande mmoja nyoka anaonesha kuwa ni maisha yanayodumu daima, tena maisha mazuri na ya furaha na ya kujitosheleza mwenyewe. Mitolojia hiyo ya nyoka mwenye uzima inaaminika hadi leo, hasa ukimkumbuka caduceo de asculapio yaani ile fimbo iliyozungushiwa nyoka alama ya uchumi, biashara, na uzima. Ndiyo maana katika maduka ya dawa (farmacy) kuna alama ya nyoka aliyetundikwa katika kijiti. Hiyo ni alama ya uponyanji, ya uhai na ya furaha. Binadamu wa kwanza alipambana na Ibilisi huyo, akapendekezewa masuala mazuri, naye akayakubali na mapato yake ni uchungu wa kifo.

Kumbe, nyoka ni kweli nduma kuwili, anakuahidi maisha kumbe kwa sumu yake kali anakuua. Hizi ndizo alama mbili za nyoka zinazokanganya tunazoziona katika kitabu cha mwanzo. Hali hizi za unyoka ziko katika kila binadamu. Leo Yesu anawekana kitimoto na Ibilisi na kwa pamoja wanajadiliana masuala mazito ya maisha. Ibilisi mwenye mang’amuzi ya muda mrefu ya kuishi hapa ulimwenguni, anajaribu kumpa Yesu ushauri wa bure ili aweze kufanikiwa katika maisha yake hapa duniani. Yesu aliupanguana ushauri wa Ibilisi na akaibuka mshindi. Yesu peke yake alitimiza unabii wa biblia kuwa atakikanyaga kichwa cha nyoka huyo mwenye sumu ya kufisha.

Kwa hiyo katika kipindi hiki cha Kwaresima tunaalikwa kutafakari ushauri wa Ibilisi pamoja na majibu ya Yesu kwani huo ni uhalisia wa maisha tunaouishi. Tuone kwanza mandhali ya majadiliano. “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi.” Angalia vizuri hapa, inatamkwa kuwa ni Roho wa Yesu yaani hadhi yake ya kufanana kabisa na Mungu hasahasa ule umwana wa Mungu, ndiyo inayomwongoza jangwani. Kwa Myahudi linapotamkwa jangwa au nyika mara moja akili yake inamrudisha uhamishoni Misri alikopewa ushauri na Ibilisi. Wakalogwa kukubali ushauri wake na mapato yake wakagongwa na kufishwa na sumu yake. Wayahudi walisafiri Jangwani kwa miaka arobaini kabla ya kuingia nchi ya ahadi. Yesu alikuwa huko jangwani kwa siku arobaini. Namba hii arobaini inamaanisha maisha yote ya mtu hapa duniani. Kwa hiyo, sisi tuko jangwani ulimwenguni kama wasafiri na bondeni kwenye machozi. Jangwani Yesu alijaribiwa. 

Neno la Kigiriki peirasthenai limefasiriwa vizuri katika Kiswahili, kwani katika maisha tunajaribiwa, kama vile “kutikisa kiberiti” ili kuona kama kuna njiti au la. Aidha anatajwa mjaribu kuwa ni Ibilisi. Ibilisi kwa Kiingereza ni devil kwa Kigiriki ni diabolou, kutokana na maneno mawili ya kigiriki: dia ni mkingamo na balei ni kuingilia kati. Hivi Ibilisi au devil ni yule anayeweka mikingamo au kupinganisha, kuingilia mambo au hasa kuingilia upendo wa watu wawili. Mfano Ibilisi ni yule anayeingilia kati na kuwaonea wivu wapendanao. Katika maisha ya mahusiano yetu na Mungu, kunaweza kuwa Ibilisi au devil anayeingilia kati na kuweka mikingamo. Ibilisi huyo anaweza kuwa mtu, au jamii, au shirika, yaani chochote kinachoingilia k mahusiano ya mapendo kati yako na Mungu. Ibilisi huyo anaweza kujimwilisha na kutujia kama rafiki. Katika Injili kulikuwa na Ibilisi aliyeingilia kati mahusiano ya Yesu na Mungu, hata Yesu akamwita Ibilisi, naye ni Petro. Yesu alimwita Ibilisi kwa sababu kuweka mikingamo katika barabara aliyoagizwa Baba yake wa mbinguni kuipita. Petro anajionesha kama rafiki mzuri anayemshauri Yesu asiendelee kupita njia ya inayoelekea Yerusalemu kuteswa kumbe ni Ibilisi.

Aidha yasemwa kuwa Yesu alibaki jangwani mchana na usiku bila kula wala kunywa. Hiyo ilikuwa nafasi pekee kwake ya kutafakari hadhi yake na mahusiano yake ya upendo na Mungu kabla ya kuiwakilisha sura ya Mungu kwa taifa. Hivi ndivyo tunavyoalikwa nasi kutafakari juu ya hadhi ya maisha yetu na mahusiano yetu na Mungu na jirani. Jaribio la kwanza na la pili linahusu mahusiano na Mungu mbele ya uhalisia wa ulimwengu tunamoishi. Tutaona tofauti illiyoko kati ya mapendekezo ya Mungu na yale ya Ibilisi.

Jaribio la kwanza: “Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.” Ibilisi anamtambua Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu, hivi anampa ushauri kwamba inambidi afanane na Baba yake. Hivi anamdokezea jinsi anavyoweza kufanana na Baba yake katika masuala ya hapa duniani. Lakini kama kawaida yake Ibilisi hawakilishi sura halisi ya Baba wa mbinguni, bali analeta picha ya miungu wanaofuatwa na wale wanaoongozwa na thamani za ulimwengu huu. Angalia Ibilisi anavyomwambia Yesu: Wewe ni Mwana wa Mungu, mtu wa hadhi ya juu sana, kutokana na maendeleo ya kisayansi na teknolojia unaweza kuwa Mungu mwenye kila kitu, hawa ndio wale wanaoitwa “Genius” “Google”. Unaweza kutumia maweza yako ili kubadili ulimwengu huu na kuutawala. Hivi hapa kuna picha halisi ya Mungu wa Yesu, na picha feki ya mungu wa ulimwengu huu. Yesu anajibu: “Imeandikwa: Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” Yaonekana hata Mungu anaafiki chakula cha kimwili, kwani katika biblia neno chakula linajitokeza mara 910. Ni vigumu kuridhika na chakula. Kumbe jibu la Yesu ni kwamba kuna maisha bora zaidi aliyotuzawadia Mungu. Hayo maisha yanatakiwa kulishwa na chakula cha kimbingu.

Jaribio la pili: Kisha Ibilisi akamchukua mpaka ji mtakatifu, kamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini.” Hapa tena Ibilisi anamkumbusha Yesu kuwa yu Mwana wa Mungu na amefanana naye kabisa hivi asijiangushe. Ibilisi anamwambia unaweza kuhakikisha kama Mungu ni Baba yako mwaminifu, unaweza kujiaminisha kwake kirahisi na kumbuka alichoahidi, kwamba atawaagiza malaika kukulinda usije ukajikwaa mguu wako jiweni. (Zaburi 91). Kwa hiyo kama kuna Baba aliahidi kuwalinda watu wake dhidi ya kila hatari basi Ibilisi anamdokezea Yesu amtie majaribuni huyo Baba kama kweli yuko. Kumbe, kama mmoja anataka kuhakikisha juu ya uwepo wa Baba yake, basi huko ni kukosa imani juu ya upendo wa Baba. Hivi kama unamwomba Mungu afanye miujiza ili kujisadikisha kama yuko hapo dini inakuwa ni ushirikina na mazingaombwe ya kutumia nguvu zaidi ya zile za kibinadamu ili kuwaaminisha watu juu ya ukuu wake. Hapa ni kukosa imani na tunaalikwa kuangalia kutomweka Mungu katika jaribio hilo. Mapato yake usipotekelezewa unachoomba unaweza kukata tamaa na kuacha kumwomba Mungu asiyesikiliza. Yesu anajibu: “Usimjaribu Bwana Mungu wako.” Kumbe Mungu yuko daima na hamwachi mja wake. Hata bustanini Getsemani Yesu alijaribiwa na kudhani labda ameachwa hadi akafikia kusali: “Mungu wangu Mungu wangu, kwa nini umeniacha?” Lakini akajijibu mwenyewe: “Siyo mimi bali mapenzi yako yatimizwe.”

Jaribio la tatu: linahusu mahusiano yetu na jirani yetu. “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, “Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.” Ibilisi anampendekezea kutawala ulimwengu wote hii ni tofauti kabisa na yule anayetumikia wengine. Suala ni kutumikia au kutumikiwa na mwingine. Pendekezo la kwanza ni la Mungu nalo ni la kutumikia. Kumbe pendekezo la pili la Ibilisi la kutaka kutumikiwa. Yesu anamfukuza Ibilisi: “Nenda zako, shetani! Kwa maana imeandikwa: “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Yesu alichukua uamuzi wa kumfuata Mungu ambaye siyo mtawala bali mtumishi wa upendo kwa watu. Wakati huu wa kwaresima tunaalikwa kujitazama na kutafakari juu ya uso wetu, nafsi yetu kama tunafanana na Yesu, kwani uso wake ni wa upendo wa Baba wa mbinguni.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.