2017-03-04 13:56:00

Papa Francisko asema: muhimu kushiriki kikamilifu na kuelewa


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Machi 2017 amekutana na kuzungumza na washiriki wa  kongamano la muziki mtakatifu kimataifa, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Muziki na Kanisa: Ibada na tamaduni katika kipindi cha Miaka 50 ya Mwongozo wa Muziki Mtakatifu”. Hili ni tukio ambalo limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni, Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki pamoja na Taasisi ya Kipapa ya Liturujia katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselmi, kilichoko mjini Roma.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mang’amuzi na majadiliano waliyoshirikishana wakati wa kongamano hili mintarafu tafakari juu ya muziki mtakatifu, mambo ya kitamaduni na kisanaa yatazisaidia Jumuiya za Kikanisa kuboresha Ibada na kuendeleza mchakato wa utamadunisho sanjari na majadiliano ya kiekumene. Imekwisha kugota miaka 50 tangu Mwongozo wa Muziki Mtakatifu ulipochapishwa na kwamba, kongamano hili limekuwa ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana kuhusu uhusiano wa kiekumene; mwingiliano wa Muziki mtakatifu na tamaduni mamboleo; muziki unaotumiwa na Jumuiya za Kikristo na maelekeo ya muziki kwa nyakati hizi. Kongamano limetoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya majiundo endelevu kwa wakleri na watawa kuhusiana na mambo ya muziki mtakatifu, ili kuboresha huduma za kichungaji, hasa kwa kwaya za Makanisa.

 

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao wa “Sacrosanctum Concilium”, kuhusu “Liturujia” waling’amua ugumu uliojitokeza kwa waamini kuweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia kwani hawakutambua kwa ukamilifu: lugha, maneno na alama zilizokuwa zinatumiwa. Kutokana na changamoto hii, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakachapisha Mwongozo kuhusu Muziki Mtakatifu na viongozi mbali mbali wa Kanisa wameendelea kujadili umuhimu wa Muziki mtakatifu katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji. Mkazo ni ushiriki mkamilifu wa waamini katika Liturujia, kama kielelezo cha furaha inayoshuhudiwa na familia ya Mungu katika ujumla wake. Waamini wanapaswa kulinganisha akili na nyoyo zao ili kumtukuza Mwenyezi Mungu, kama ile Liturujia inayoadhimishwa kwenye Yerusalemu ya mbinguni!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa kuhusiana na Muziki mtakatifu linahimiza kwa namna ya pekee: ushiriki mkamilifu; uelewa wa kile kinachoadhimishwa na utimilifu wake ili kufaidika na matunda ya maadhimisho ya Liturujia. Lengo ni kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo miongoni mwa watu wake; Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kuwakomboa watu wake. Ushiriki mkamilifu na uelewa makini unawasaidia waamini kuzama katika Mafumbo ya Kanisa kwa kutambua na kuyatafakari; kwa kuabudu na kuyakumbatia, ili kutambua maana yake ya ndani hata katika ukimya na lugha ya muziki inayotumiwa na Kristo Yesu. Huu ndio mwelekeo unaopania kupyaisha Muziki mtakatifu ili kudumisha thamani yake.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa lina dhamana ya kuhakikisha kwamba, linawafuatilia kwa karibu wale wenye dhamana katika masuala ya Muziki mtakatifu ili kuweza kulinda na kuthaminisha amana na urithi wa Muziki mtakatifu katika historia iliyopita, kwa kuutumia kwa umakini mkubwa bila kuubeza au kuutupa kapuni! Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na mchakato wa utamadunisho wa lugha ya wasanii, ili kweli Neno la Mungu liweze kusikika katika nyimbo ili kuburudisha mioyo ya waamini, kwa kuwatengenezea mazingira ya imani, ili kupokea na kushiriki kikamilifu katika mafumbo yanayoadhimishwa.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, katika mabadiliko ya Liturujia, kwa kuingiza lugha mbali mbali kumekuwepo na matatizo na changamoto katika mtindo na muundo wa muziki wenyewe, kiasi hata cha kudhalilisha Liturujia inayoadhimishwa! Kumbe, wadau mbali mbali wa Muziki mtakatifu wanaweza kuchangia katika maboresho ya Muziki mtakatifu na nyimbo zinazotumika katika Liturujia. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya wadau mbali mbali kupata majiundo makini, bila ya kuwasahau Majandokasisi wanaojiandaa kuwa Mapadre; kukuza na kuendeleza majadiliano katika mifumo ya muziki wa kisasa mintarafu tamaduni za watu na majadiliano ya kiekumene.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawatakia heri na baraka katika maisha yao, daima wasindikizwe kwa maombezi ya Bikira Maria, ambaye kwenye Utenzi wa “Magnificat” ameimba utakatifu wa huruma ya Mungu. Wajitahidi kuwasaidia watu wa Mungu kufahamu na kushiriki kikamilifu katika Fumbo la maisha ya Mungu. Muziki mtakatifu na nyimbo za ibada zina dhamana ya kuwapatia waamini maana ya utukufu, uzuri na utakatifu wa Mungu unaowafunika na kuwajaza watu wake kwa wingu la mwanga angavu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.