2017-03-04 08:11:00

Mpatieni Yesu nafasi apyaishe ukakasi wa maisha yenu ya kiroho!


Taifa la Mungu Tumsifu Yesu Kristo. Kuanzia jumatano ya majivu tumeanza kipindi cha kwaresma ambacho ni maandalizi ya sikukuu ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni wakati maalum wa kumkaribisha Yesu atembee katika jangwa la kila mmoja wetu sio kwa hizi siku arobaini tu bali katika maisha yetu yote lakini basi hasa hizi siku maalum ambazo mama kanisa anatupatia za kutadhimini jangwa la maisha yetu.  Tukikumbuka wazi kwamba namba arobaini katika Biblia inamaanisha kipindi kirefu na hivyo basi kumaanisha katika maisha yetu yote.

Masomo yetu ya jumapili hii ya kwanza ya kwaresma yanatualika kutafakari kuhusu safari ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Katika somo la kwanza kutoka katika kitabu cha mwanzo Adamu na Hawa wanashindwa kushinda majaribu na matokeo yake wanaanguka katika dhambi. Wanaanguka katika dhambi ya kutofautiana. Adamu na Hawa walikuwa wanaishi pamoja kwa upendo na furaha lakini sasa wanatofautiana. Kila mmoja anamuona mwenzake tofauti, wanajiona wako uchi.  Katika somo la injili Kristo anajaribiwa na tunaona anayashinda majaribu hivyo basi anafanikiwa kumkomboa mwanadamu katika dhambi. Kumbe basi Kristo anachukua nafasi ya Adamu  na anakuwa Adamu mpya.

Katika somo la Injili tumesikia kwamba Kristo aliongozwa na Roho kwenda jangwani ili kujaribiwa na shetani. Ndugu zangu, jangwani/nyikani ni sehemu ambayo hakuna maji, hakuna chakula, hakuna miti na hakuna pa kujificha. Jangwani huwezi kujificha hata kidogo na magumu yaliyopo jangwani yanaweka wazi undani wote wa mwanadamu. Jangwa linamuanika mtu jinsi alivyo. Kumbe kipindi cha kwaresima tunakaribishwa pia kuingia ndani ya jangwa letu na kumruhusu Yesu atembee huko afufue upya imani, matumaini, na mapendo yetu kwa Mungu na kwa jirani zetu. Kumbe, basi hiki ni kipindi tunachoalikwa kuweka mioyo yetu mbele ya kioo na kujiona jinsi tulivyo hivyo basi, kumruhusu Kristo atusafishe kwa neema ya Sakramenti ya Kitubio, ili kuimarisha ile neema ya utakaso tuliyopata wakati wa Ubatizo wetu. Huu sio muda wa kuficha dhambi zetu kwa sababu hatua ya kwanza ya kupambana na dhambi ni kuitambua dhambi ndani yetu, ili kuitubu, kuiungama, kutimiza malipizi na hatimaye kupania kuiacha kabisa!

Kwenye masomo yetu ya leo tunaona anayeshawishi/jaribu ni shetani. Shetani linatokana na neno la Kigiriki Diabolos kumaanisha mtu, watu, taasisi, au kitu chochote kinachotenganisha upendo kati ya Mungu na binadamu au binadamu na binadamu.  Mfano kwenye Injili ya Mathayo 16:23 Petro anaitwa shetani/ibilisi kwasababu anataka kumsimamisha Kristo katika safari yake ya ukombozi ndio maana Mungu anamkanya haraka sana. Kwa mara nyingi tumekuwa na picha ya shetani kama kitu kinachoogopesha sana ambacho mtu ukikiona lazima akimbie. Sasa ingekuwa kweli shetani yupo hivi nani angekubali kusubiri ashawishike? Kumbe, shetani anavaa ngozi ya malaika. Shetani anatujia kwa ujanja wa hali ya juu, anakudanganya anakupenda, anakujali na anakutakia mema kwa lengo la kukurubuni. Mfano katika kitabu cha Mwanzo shetani anavalishwa sura ya nyoka.  Kwa hali ya kawaida wote tunamwogopa nyoka. Nyoka ni mbaya, ni hatari kwa maisha.

Nyoka katika kitabu cha Mwanzo anatumika kama alama iliyo na maana mbili tofauti ambazo pia zinaonyesha maana mbili za vishawishi.  Shetani wa ahadi anayeahidi kukupa maisha, furaha, kujitambua nk, mfano kama tulivyosikia katika kitabu cha Mwanzo shetani anawaambia Adamu na Hawa kwamba nanyi mtakuwa kama Mungu. Alama nyingine ni ya shetani mwongo, mzushi anayetaka kukupoteza, kukuharibia maisha. Shetani anamshawishi mwanadamu anamwambia usikubali kuamuliwa kila kitu na Mungu, amua mwenyewe, kuwa mungu wewe. Kwa hiyo, hapa shetani anamdanganya mwanadamu atumbukie kwenye shimo la kujiamulia yeye kipi kizuri na kipi kibaya.  Kumbe, shetani anashawishi uende njia tofauti, upotee njia. 

Katika jaribu la kwanza tunaona shetani anakubali kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu na ili kudhibitisha hilo anamshawishi aonyeshe huo umungu. Ili aweze kuonyesha huo umungu anamshawishi aamuru mawe yawe mkate. Shetani anamwambia Yesu kama unataka kufanana na Mungu Baba fanya nikuambiavyo. Shetani haonyeshi sura halisi ya Mungu. Huyu ni mungu sanamu anayeabudiwa na watu wanaoabudu vitu na mali za ulimwengu huu. Katika huu ulimwengu ubora/ ukuu/ uweza wa mtu unapimwa kwa mali alizo nazo…Akaunti ya benki, magari, nyumba, viwanja, simu ya bei mbaya, kubwa utadhani daftari,nk,  kinachotiliwa mkazo hapa ni kuwa na mali nyingi iwezekanavyo… “Super man”, kuwa mungu wa vitu, huyu ni mungu wa dunia. Yesu anajibu kwamba ni kweli mwanadamu anahitaji mkate kuishi ila hatoshelezwi kamwe kwa mkate tu bali anahitaji pia Neno la Mungu. Mwanadamu ni tofauti na mnyama, hatoshelezwi tu kwa vitu vya kidunia,  bali ana maisha ya kiroho ambayo yanalishwa kwa Mkate utokao mbinguni.  Ni wazi kwamba vitu vya dunia hii sio vibaya lakini basi havitakiwi kuchukua nafasi ya Mungu au kututenganisha na Mungu.

Jaribu la pili linazungumzia mahusiano yetu na Mungu. Shetani anaonyesha mungu feki mbele ya Yesu. Shetani anacheza na taswira ya yesu..kama wewe ni mwana wa mungu jitupe chini malaika watakuokoa kama ilivyoandikwa katika Zaburi 91.  Swali la kujiuliza  hapa ni; mwana wa Mungu ni nani? Kupitia ubatizo tumekuwa wana wa nani? Mungu wangu ni nani? Mimi ni mwana wa mungu yupi? Mungu vitu wa huu ulimwengu au wa ufalme wa Mungu? Ibilisi anamwambia Yesu usijali Mungu ameahidi kukulinda. Ndugu zangu, kama una imani unayo kuna haja gani ya kuijaribu/kuihakikisha? Ukiijaribu maana yake huamini kama ipo. Ni kama wanawali wawili wawekane majaribuni siku moja kabla ya ndoa yao kuhakikisha kama wanapendana.  Hapo kutakuwa na shida kwasababu kama upendo upo kwanini waufanyie majaribio? Shetani anataka tufikiri ya ulimwengu huu tu. Anataka kutuweka mbali na Mungu. Yesu anamjibu, usimjaribu Bwana Mungu wako. Yesu anajibu kwa upendo mkuu.

Katika jaribu la tatu shetani anaahidi utawala wote wa ulimwengu huu. Hili jaribu linazungumzia mahusiano yaliyopo kati ya watu wa ulimwengu huu.  Mahusiano katika ulimwengu huu yanaweza kuwa yale ya kutumikia au kutumikiwa. Hapa kuna mapendekezo mawili; pendekezo la kwanza ni lile la Mungu kwamba anayetaka kuwa mwanadamu kamili lazima awe mtumishi wa wote. Pendekezo la pili ni lile la shetani la kuwa (super man), kutaka kutumikiwa, kutawala wengine, kuabudiwa. Yesu anajibu kwmaba anayetakiwa kuabudiwa ni Mungu pekee.  Kumuabudu shetani inaamanisha kujiweka chini ya utawala wake. Utawala wa  kunyanyasa, na sio wa upendo na huduma.

Ndugu zangu haya ni majaribu tunayokumbana nayo kila siku katika maisha yetu. Kumbe basi, tujitahidi kumruhusu Kristo atembee katika Jangwa la maisha yetu ya kiroho ili tuweze kuwa na mabadiliko ya kweli yanayoendana na tunu msingi za Kiinjili. Tujichotee neema za hiki kipindi cha Kwaresima ili tuimarike katika ukristo wetu, tayari kuadhimisha Fumbo la Imani, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Amina.

Na Padre Honesti Mapendo Lyimo.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.