2017-03-03 17:42:00

Dhambi ni janga la maisha ya binadamu!


Mtakatifu Yohane Chrysostom anasema lipo janga moja tu duniani, nalo ni janga la dhambi. Ndugu zangu kipindi cha kwaresima huanza siku ya jumatano, inayoitwa jumatano ya majivu. Katika ibada hiyo tunapakwa majivu utosini au kisogoni. Maana yake nini? Alama hii yatukumbusha kuwa mwili wa mwanadamu u katika hali ya uharibifu na ukomo – alama hii ikituelekeza kwenye matumaini makuu. Tunaishi tukitambua kuwa sisi si kitu na ulimwengu huu ni mahali pa kupita tu. Tunakiri na kukubali waziwazi mbele ya Mungu Baba Muumba wetu na mbele ya wenzetu kuwa sisi tumepungukiwa. Ni majivu tu. Lakini huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Tunakiri dhambi zetu. Kumbe, hata baada ya kupata neema ya Mungu, mwanadamu bado anaweza kutenda dhambi. Hatari kweli.

Katika KKK na. 397 tunasoma hivi – Mtu akishawishiwa na ibilisi, aliliachilia tumaini alilokuwa nalo kwa Muumba wake life moyoni mwake, na kwa kutumia vibaya uhuru wake akakaidi Amri ya Mungu. Hiyo ndiyo dhambi ya kwanza ya mtu. Tangu hapo, kila dhambi itakuwa ni kumkaidi Mungu na kukosa kutumainia wema wake. Kipindi cha Kwaresima hutupatia muda wa kujikarabati kiroho na kimwili ili tusherehekee pamoja  na Kristo ufufuko. Ni nafasi tunayopata ili tuweze kufufuka kimwili na kiroho, kiakili, katika namna yetu ya kutenda, namna ya kufanya shughuli zetu, kufanya mabadiliko katika mitizamo yetu, mawazo yetu, maneno na matendo yetu, katika mahusiano yetu. Ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na kusameheana makosa tayari kuanza upya katika mwanga wa Injili.

Sisi tunaalikwa kujitafakari tena tunapooanza kipindi kingine cha Kwaresima. Maswali machache ya tafakari. Je, ni yupi ibilisi wako anayekuamrisha umpigie magoti? Ni mambo yepi tunayaamini mno na kuona kuwa  ya maana zaidi na kuyapigia magoti ingawa yanapingana na mapenzi ya Mungu? Je, tunafanya matumizi mazuri ya akili, uhuru, utashi na neema aliyotujalia Mwenyezi Mungu? Tuombe sana neema na baraka yake Mungu ili kipindi hiki cha toba na mwito tena wa kuiamini Injili kizae matunda ya kimungu katika maisha yetu.

Tunapoangalia Liturujia yetu ya leo na Neno la Mungu tunajiuliza maswali mengi. Mojawapo ni hili. Kwa nini Yesu alishawishiwa? Mbona alikuwa na uwezo wa kumkataza shetani mara moja? Mwinjili Mathayo na Luka wanamwona Yesu akimshinda shetani na nguvu zake zote. Katika Mt. 3:17 mara tu baada ya Ubatizo wa Yesu, tunasikia sauti ikisema ‘huyu ni Mwanangu Mpendwa, ninayependezwa naye’. Matayo anaandika juu ya kushawishiwa Yesu mara tu baada ya ubatizo wake. Mwandishi wa YBS 2:1 anaandika hivi – ‘mwanangu, kama ukija kumtumikia Bwana, weka tayari roho yako kujaribiwa’. Tunaambiwa kuwa hakuna mwana wa Mungu atakayeepuka vishawishi sababu hii ndiyo njia ya kutofuatisha mfuasi halisi na mwongo. Mwandishi mmoja anasema tendo la kishawishi kwa Yesu, ni utangulizi wa ushindi utakaonekana pale Msalabani. Sisi waamini tunashiriki ushindi huu. Vinginevyo Injili isingeandikwa, kutangazwa na kushuhudiwa ulimwenguni.

Ila pamoja na maelezo/majibu hayo machache bado swali linabaki. Ni kwa nini Yesu ashawishiwe? Somo la kwanza leo laongea juu ya uumbaji wa mtu, wa miti bustanini, Amri ya Mungu kwa wazazi wa kwanza, juu ya ushawishi wa shetani na habari ya dhambi ya asili.  Kwa hali hii Yesu alishawishiwa kama tuonavyo katika Kitabu cha Mwanzo, tangu mwanzo mwanamme na mwanamke walishawishiwa na wakapotea. Kwa upande mwingine Yesu angejuaje hali yetu kama asingeshawishiwa? Pia angekuwaje Mkombozi wetu kama asingeshinda vishawishi? Katika Ebr. 2:16-18, twaona kuwa Yesu alishawishiwa. Hali hii inamfanya atusaidie zaidi. Alifanana na ndugu zake ili awe mwenye huruma na mwaminifu kwa Mungu Baba, kwa ajili yetu. Alijua hali yetu na ndiyo maana ni mwaminifu. Katika fundisho hili twaona kuwa Yesu alichukua mwili ili ashiriki mateso yetu.

Swali lingine linalofuata ni hili. Kwa nini mtu ashawishiwe au akubali kushawishiwa? Katika KKK na. 396 tunasoma hivi – Mungu alimwumba mtu  kwa sura yake na akamfanya rafiki yake. Kama kiumbe cha kiroho, mtu hawezi kuuishi urafiki huu bila kujinyeyekea kwa hiari mbele ya Mungu. Hiyo ndiyo maana ya amri aliyopewa mtu asile matunda ya Mti wa Ujuzi wa Mema na Mabaya. ‘Kwa maana siku utakapokula, hakika utakufa’. Mti wa ujuzi wa mema na mabaya huonesha kwa mifano mipaka ambayo mtu, kwa vile ni kiumbe, amewekewa asiivuke. Tena aikubali mipaka hiyo kwa hiari na aiheshimu kwa ujasiri. Mtu anamtegemea Muumbaji wake, na yuko chini ya sheria za uumbaji na taratibu za maadili zinazoratibu matumizi ya uhuru.

Jibu ni moja tu na ndilo linalowezekana. Mungu alitaka watu huru na si “matoyi”. Uwezekano wa kushinda vishawishi hudhihirisha kweli uhuru wetu. Yesu amefanya hilo. Nasi tumfuate. Tunakumbushwa kuwa kishawishi ni kipimo cha uhuru wa mtu na kwamba mateso huwa ni kipimo cha jinsi ya kufanya maamuzi.  Mtu huru hufanya uamuzi sahihi na baada ya uamuzi sahihi hufuata majukumu. Mtumwa hushurutishwa. Kwa hakika akili, uhuru, utashi na neema ya Mungu vikitumika vizuri kinachofuata ni majukumu. Tumeona Yesu akisimamia hilo. Neno la Mungu leo latupa changamoto ya matumizi sahihi ya akili, uhuru, utashi na neema yake Mungu. Ni katika uhuru huu, tunabeba majukumu na katika kutimiza mapenzi yake Mungu tunapat wokovu. Tunaimarishwa na neno la Mungu toka Ebr. 4:15, – ‘maana hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuonea huruma udhaifu wetu, kwani yeye alijaribiwa kama sisi katika mambo yote, ila hakutenda dhambi’. Kumbe tukimfuata yeye tutashinda.

Swali lingine linalofuata ni hili. Vishawishi vyatoka wapi? Kwanza vyatoka kwa shetani. Kama ilivyo katika Injili ya leo. Na pia kishawishi chatoka ndani yetu. Katika waraka wa Yakobo 1:12 -15 – tunasoma hivi; mwenye heri mtu avumiliaye kishawishi, kwa maana akiwa amekishinda atapata taji la uzima alilowaahidia Mungu wenye kumpenda. Mtu anaposhawishiwa asiseme ‘ninashawishiwa na Mungu’. Maana Mungu hawezi kushawishi kutenda mabaya, wala yeye mwenyewe hamshawishi mtu. Kila mtu anashawishiwa akivutwa na kubembelezwa na tamaa yake mwenyewe. Na baada ya kuchukua mimba, tamaa inazaa dhambi, na dhambi inapokomaa inazaa mauti. Kwa hiyo kishawishi chatoka kwa shetani na pia kutoka kwenye hali yetu iliyoyanguka dhambini. Waswahili husema ‘ ibilisi wa mtu ni mtu’.

Twawezaje kuepuka vishawishi? Walimu wa kale watuambia hata ikibidi tukimbie mazingira. Mtakatifu Agustino anasema wazi kuhusu jambo hili. Katika injili ya  Mt. 5:29-30 tunasoma hivi – jicho lako la kulia likikukosesha, uling’oe na kulitupilia mbali, kwa maana yakufaa zaidi kupotewa na kiungo kimoja kuliko kutupwa mwili wako mzima Jehenamu. Na mkono wako wa kulia ukikukosesha, uukate na kuutupilia mbali. Afadhali upotewe na kiungo kimoja kuliko kutupwa mwili wako mzima Jehenamu.

Majibu ya Yesu dhidi ya shetani hutupa mwongozo wa namna ya kusimama imara dhidi ya vishawishi na shetani. Jibu la Yesu katika kishawishi cha kwanza linatupa  changamoto juu ya namna tunavyopaswa kutumia vizuri vipaji alivyotupatia Mungu. Yesu alikuwa na uwezo wa kugeuza mawe kuwa mkate, lakini hakufanya hivyo. Katika kishawishi cha pili twapata changamoto namna ya kutambua na kuishi imani. Ingawa Yesu anamwamini Mungu na hakuwa na shaka, hakuwa tayari kumjaribu Mungu Baba.Katika kiswawishi cha tatu, ingawa Yesu anataka ulimwengu utambue ukuu na uwezo wake Mungu, hayuko tayari kufanya hivyo kwa kumtii mungu wa uongo. Hakika namna ya kushinda vishawishi ni kuishi maagizo ya Kwaresima yaani maisha ya sala, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, kufunga na kutenda matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini!

Tumsifu Yesu Kristo.  Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.