2017-03-03 10:32:00

Adhabu ya kifo imepitwa na wakati ni kinyume cha haki msingi!


Hakuna uhakika unaosadifu kwamba hukumu ya kifo imekuwa na mafanikio makubwa katika kudhibiti makosa ya jinai sehemu mbali mbali za dunia. Hukumu ya kifo imepitwa na wakati na kwamba, ni adhabu inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu! Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inafutulia mbali adhabu ya kifo kwani maisha ya binadamu awaye yote ni matakatifu na yanapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake!

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, Uswiss, wakati alipokuwa anashiriki katika mkutano wa 43 wa Baraza la Haki Msingi za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Anaendelea kusema, hata mkosaji anayetuhumiwa kwa mauaji ana haki ya kuishi kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Wakati mwingine haki ya binadamu inaweza kurekebishwa kutokana na sababu mbali mbali, lakini adhabu ya kifo ikishakutolewa na kutekelezwa, hata kama imekosewa haki haiwezi kupatikana tena!

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna watu waliowahi kuhukumiwa adhabu ya kifo na baadaye ikadhihirika kwamba, hawakuhusika na makossa yale, lakini tayari walikuwa wamekwisha kunyongwa! Hukumu ya kifo ni kielelezo cha serikali kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa raia na matokeo yake inalazimika kuua kwa kisingizio cha haki! Lakini, hakuna haki inayoweza kutendwa kwa njia ya mauaji.

Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu unakaza kusema, kuna mbinu nyingi zinazoweza kutumiwa kudhibiti makosa ya jinai, kwa kuhakikisha kwamba, hata watuhumiwa wanapata haki na nafasi ya kuweza kujirekebisha hatimaye, kurejea tena katika jamii ili kuchangia mustakabali wa maendeleo ya jamii zao, wakiwa watu wapya, huku utu na heshima yao ikiheshimiwa kama binadamu! Askofu mkuu Ivan Jurkovic  anasema, Vatican imedhamiria kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutokomeza adhabu ya kifo kama ilivyoamriwa kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye Azimio la mwaka 2014. Vatican inapenda kuzihamasisha nchi mbali mbali dunia kufanya maamuzi machungu ya kufuta adhabu ya kifo ili kulinda utu wa watu wote na kutoa nafasi kwa watuhumiwa kuhukumiwa kwa haki zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.