2017-03-02 15:15:00

Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na changamoto ya wote!


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, Jumatano ya Majivu, tarehe 1 Machi 2017 limezindua Kampeni ya 54 ya Kwaresima kwa Mwaka 2017 inayoongozwa na kauli mbiu “Udugu: baianuai ya Brazil na ulinzi wa maisha”. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Mwanzo “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil katika uzinduzi wa kampeni ya udugu nchini humo anasema hii ni changamoto kubwa ambayo binadamu anakabiliana kwa wakati huu. Hii ni changamoto inayohitaji ushiriki wa watu mbali mbali, ili kuweza kufikia malengo yanayokusudiwa.

Baba Mtakatifu anasema, amefafanua changamoto ya utunzaji bora wa mazingira katika Waraka wake wa kitume “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote! Mwenyezi Mungu amekuwa mkarimu sana kwa Brazil kwa kuipatia utajiri mkubwa wa maliasili unaoipambana kwa uzuri wa kuvutia. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kuna vitendo vinavyochangia uharibifu mkubwa wa mazingira. Kanisa, daima limekuwa mstari wa mbele kama sauti ya kinabii kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira sanjari na kuwasaidia maskini ambao ni waathirika wakuu wa vitendo vya uchafuzi wa mazingira.

Changamoto kubwa iliyoko mbele ya wananchi wa Brazil ni kuwataka kuangalia kwa makini matatizo ya ekolojia, lakini zaidi kufahamu chanzo cha matatizo haya na mbinu za kuweza kukabiliana nayo ili kuboresha mazingira, nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, kunako mwaka 1979, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil liliendesha Kampeni ya Kwaresima iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya ulimwengu ambao ni wa kibinadamu zaidi”. Hapa waamini na watu wote wenye mapenzi mema walikuwa wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanalinda na kutunza mazingira kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, tangu wakati ule, kwa kusoma alama za nyakati liliwaonya wananchi wote kuhusu athari za uharibifu wa mazingira kutokana na kazi za binadamu. Kumbe, familia ya Mungu nchini Brazil inapaswa kusimama kidete kulinda na kudumisha mazingira bora, nyumba ya wote, kwani wamekabidhiwa na Mwenyezi Mungu kulima na kuitunza ardhi ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu sanjari na udumishaji wa udugu, kwa kulinda na kutetea maisha ya binadamu na tamaduni zake kwa mwanga wa Injili.

Uharibifu wa mazingira, nyumba ya wote anasema Baba Mtakatifu, unachangiwa kwa kiasi kikubwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Kumbe, Kampeni hii ya Kwaresima inapania pamoja na mambo mengine kuwasaidia wananchi wa Brazil kusimama kidete katika kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote! Waoneshe moyo wa shukrani kutokana na baianuai mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu ameijalia nchi ya Brazil na watu wake. Lakini, ikumbukwe kwamba, hii ni changamoto kwa watu wote duniani, kwani uharibifu mkubwa wa mazingira matokeo yake ni ukosefu wa haki msingi za kijamii. Watu asilia mara nyingi wamekuwa ni mfano bora zaidi wa kuishi na kutunza mazingira nyumba ya wote, kama kielelezo cha utimilifu wa huruma ya Mungu kwa binadamu!

Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wa Brazil kujitaabisha kuwafahamu watu hawa na kujifunza kutoka kwao katika mchakato wa kudumisha uhusiano mwema na mazingira, nyumba ya wote. Pale inapowezekana, Brazil iangalie sera na mikakati mbadala ya maendeleo ya binadamu kwa kuwa na matumizi bora ya rasilimali na utajiri wa nchi kuliko hali ilivyo kwa sasa, ambamo, kumekuwepo na matumizi makubwa ya rasilimali za dunia, kiasi kwamba, utu na heshima ya maskini vinawekwa rehani. Kila mwaka kampeni ya udugu wakati wa Kwaresima ni mwaliko na changamoto kwa waamini kukiishi kipindi hiki kwa manga wa Fumbo la Pasaka, tayari kutubu na kumwongokea Mungu.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ilikuwa ni changamoto ya kuwarejeshea tena maskini utu na hadhi yao kama binadamu. Mwamini anayeadhimisha Fumbo la Pasaka kwa kusherehekea ushindi wa maisha dhidi ya nguvu ya kifo na mauti anapaswa kuwa makini katika kutunza mazingira nyumba ya wote, Brazil nayo inapaswa kujenga na kudumisha mwelekeo huu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anaitakia heri na baraka familia ya Mungu nchini Brazil. Ni matumaini yake kwamba, kampeni ya Kwaresima itaweza kufanikisha malengo yake. Anawaweka wananchi wote wa Brazil chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria  Mama Yetu wa Aparecida, kwa namna ya pekee kabisa wanapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.