2017-03-02 15:54:00

Imani kwa Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo iguse madonda ya watu


Wakristo katika maisha yao wanapaswa kumfuasa Yesu Kristo aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye Umungu mmoja sawa na Baba, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Huyu ndiye Yesu ambaye Madonda yake Matakatifu bado yanaendelea kutoka damu miongoni mwa ndugu zake wadogo, yaani maskini na wale wote wanaonyanyaswa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii! Hii sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 2 Machi 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, mwanzoni mwa Kipindi cha Kwaresima, mwaliko kwa waamini ni kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu; kwa kuchagua mema na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Mwenyezi Mungu amewapatia waja wake, Amri zake ili ziweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha. Haikuwa rahisi sana kwa Mitume wa Yesu kutambua Njia ya Msalaba, kama kiini cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Hiki ni kielelezo cha unyenyekevu wa Mungu aliyejifanya mtu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi!

Hakuna Mungu pasi na Kristo, kwani Yesu ni ufunuo wa Mungu, aliyekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ni Mungu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Ukweli wa Mungu anasema Baba Mtakatifu, unafumbatwa katika huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, chimbuko la matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hapa waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa binadamu wanaoendelea kuteseka kutokana na sababu mbali mbali. Hiki ndicho kiini cha maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima, yaani kutubu na kumwongokea Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu anawahamasisha wale wote wanaotaka kujisadaka na kumfuasa katika maisha yao, lazima kwanza wajikane wenyewe na kuchukua Msalaba wao, tayari kumfuasa Kristo Yesu, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha! Kumfuasa Kristo si kwa ajili ya mtu kutenda anavyotaka, lakini kile ambacho Yesu anapenda katika maisha ya mwamini wake. Hii ndiyo njia inayomwezesha mwamini kupata furaha ya kweli na hatimaye, maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe tayari kuachana na malimwengu, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji. Mwenyezi Mungu anapaswa kuabudiwa, kutukuzwa na kuheshimiwa na wote. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumfuasa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hii ndiyo dira na mwongozo wa maisha ya wakristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.