2017-03-01 12:35:00

1 Machi ni Siku ya Kimataifa ya kupinga ubaguzi wa kila aina


Tarehe 1 machi  ya kila mwaka ni siku ya kimataifa ya kupinga aina zote za ubaguzi ambapo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Ukimwi, UNAIDS  katika tarehe 1 Machi ya mwaka huu 2017 imesema kuwa, lengo kuu kwa mwaka huu ni kuwataka  kila mtu apaze sauti ili kupinga ubaguzi wa aina zikiwemo zile dhidi ya watu wenye virusi vya Ukimwi, VVU, au Ukimwi.Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé amesema kutokubaguliwa ni  haki ya binadamu na hivyo ni vyema sheria na kanuni na mazingira bora vikawepo ili kundi hilo lipate matibabu bila vikwazo vyovyote.

Ikimbukwe kila mwaka kampeni zimekuwapo za kulenga kutoa wito kwa watu wote popote pale walipo kuendeleza na kutambua haki ya kila mmoja kuishi maisha yenye utu bila kujali muonekano, jinsi, ampendaye na hata uwezo wake wa kiuchumi.Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa Bwana Sidibé amesema wanawake wenye VVU hawapatiwi huduma za afya ya uzazi hali inayosababisha wapate saratani ya mfuko wa uzazi ambao hatimaye hutolewa badala ya kupatiwa huduma, hivyo amesema…"Nadhani nataka nihakikishe tu watu wanasikia ya kwamba tunaweza kushinda, lakini kamwe hatutashinda kwa kubagua watu."Kwa ufafanuzi zaidi anasema kile kinachokwamisha makundi kama vile wanaojidunga madawa ya kulevya, wapenzi wa jinsia moja kukosa huduma."Nadhani tunakabiliwa na tatizo kubwa la desturi na mila na vikwazo vya kitamaduni ambavyo tunapaswa kuondoa. Halikadhalika sheria na sera mbovu ambazo zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa cha kupata huduma."Anasema Sidibe’.

Hata hivyo kutokana na siku ya kimataifa ya kupinga aina zote za ubaguzi ikumbukwe nchini Tanzania uliwekwa muhtasari wa Mkakati wa kitaifa wa kupunguza unyanyapaa wa ubaguzi tangu 2013 -2017.

Katika utangulizi wa mhutasari huo tunasoma yafuatayo: kwamba Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine, watu wanaohusishwa na VVU wanatazamwa vibaya na kufanyiwavitendo viovu vinavyochangia kudhoofisha afya na uwezo wao wa kuishi maisha yenye tija, hali ambayo husababisha kile kinachoitwa unyanyapaa na ubaguzi.Unyanyapaa unahusu imani na mtazamo ambao kwa kiwango kikubwa hudhalilisha utu wa mtu au kikundi cha watu kutokana tu na maumbile yasiyokuwa ya kawaida au kuhusiana na VVU na UKIMWI. Hali hii huweza kusababisha vitendo vyenye kuumiza kama vile ubaguzi dhidi ya mtu huyo au kikundi hicho.

Watu walioathiriwa na unyanyapaa na ubaguzi huweza kupoteza ajira, riziki, mali na marafiki. Wengi wa watu hawa wameacha kutafuta au kuhudhuria huduma za afya kwa sababu tu ya kuhofia kunyanyapaliwa au kubaguliwa. Kwa mtazamo huu, unyanyapaa na ubaguzi vimekuwa ni miongoni mwa vichocheo vya maambukizo ya janga la VVU na UKIMWI kwa kusababisha hofu na usiri miongoni mwa watu juu ya kupima VVU na kuweka wazi hali yao ya afya.Katika juhudi za kushughulikia sababu kuu za unyanyapaa na ubaguzi Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imetengeneza Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Unyanyapaa na Ubaguzi unaohusiana na VVU na UKIMWI wa 2013-2017 kulingana na Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI Tanzania [II & III] na Sheria ya Kuzuia na Kudhibiti VVU na UKIMWI ya Mwaka 2008.

Aidha, Mkakati huu wa Kupunguza Unyanyapaa na Ubaguzi umetolewa katika kipindi mwafaka kuendana na shabaha tatu za Umoja wa Mataifa za kutokuwepo na maambukizo mapya, unyanyapaa na ubaguzi, na vifo vitokanavyo na UKIMWI.Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Unyanyapaa na Ubaguzi unaohusiana na VVU na UKIMWI umeorodhesha maeneo makuu 13 ya kimkakati na kuainisha malengo na viashirio muhimu ili kupata mwitikio wa kuridhisha dhidi ya unyanyapaa na ubaguzi.

 Kwa kuanisha maeneo muhimu ya kipaumbele, mkakati unalenga kuunganisha juhudi za wadau ili kupata matokeo zaidi yanayotazamiwa kutoka kwenye programu zakisekta. Mkakati umetayarishwa kwa kuzingatia mapitio ya kina ya taarifa zilizotokana na mchakato wa mashauriano na wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi kutoka serikalini, asasi za kiraia, na mitandao ya watu wanaoishi na VVU, vyama vya kitaaluma, sekta binafsi na vyuo vikuu. 
Mchakato huu uliongozwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Serikali ya Marekani (USAID) kupitia Mradi wa Kuimarisha Sera za Afya (Health Policy Initiative) unaoendeshwa na Futures Group International, ikiwa ni pamoja na msaada kutoka Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kusaidia Harakati Dhidi ya UKIMWI (PEPFAR).

Visababishi vikuu vya Unyanyapaa na Ubaguzi Unaohusiana na VVU
Watafiti ulimwenguni kote wameainisha aina tatu za vichocheo vikuu vya unyanyapaa vikiwemo ukosefu wa elimu / utambuzi, woga wa kuambukizwa VVU na mtazamo hasi wa jamii kuhusisha maambukizo ya VVU na tabia za aibu. Kukosekana kwa utambuzi kunawafanya watu washindwe kutambua mitazamo, inavyowaathiri wengine. Wakati mwingine VVU vimefikiriwa isivyo kuwa vinaambukiza kwa urahisi sana hivyo kuchukuliwa kama tishio kubwa kwa jamii.
Dhana potofu zinaweza kuifanya jamii kufanya vitendo vya kunyanyapaa wengine. Watu wamedhani kimakosa kwamba VVU vyaweza kuambukizwa katika majumuiko ya kawaida na hivyo kujihalalishia vitendo vya kuwanyanyapaa wale wanaoishi na VVU kama vile kuwanyima pango, ajira n.k. Mara nyingi watu wamehusisha VVU na tabia mbaya ya uasherati hivyo kulifanya suala hilo kama jambo la aibu, shutuma na hukumu. Kwa bahati mbaya, mitazamo hii imejikita kwenye mila na desturi za jamii na kuifanya iwe vigumu kushughulikiwa.

Ni mamilioni ya watu ambao wanaathirika na vitendo hivyo duniani  , ambapo ni changomoto kubwa inayo paswa kutatuliwa katika kukomesha unyanyapaa na ubaguzi.Swali, tangu kuwekwa kwa mhutasari wa 2013 kufikia leo hii 2017 , tunapoadhimisha  siku ya kimataifa ya kupinga aina zote za ubaguzi, je tabia hiyo  nchini Tanzania kama mojawapo ya nchi nyingine duniani imefika hatua zipi za mapambano ?


Sr Angela Rwezaula 
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.