2017-02-28 09:25:00

Papa Francisko kuongoza maandamano na Ibada ya Toba!


Mwenyezi Mungu kila mwaka anawajalia waamini kungojea kwa moyo wa toba, wongofu wa ndani na furaha ya kweli, maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Waamini wakifuata kwa bidii mambo ya: Ibada na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa zinazowaletea nguvu ya maisha ya kiroho, tafakari ya kina ya Neno la Mungu linalopaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha unaomwilishwa katika vipaumbele vyao kama kielelezo cha imani tendaji,  watakuwa kweli ni watoto wa Mungu waliozaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya Majivu, tarehe Mosi Machi 2017 majira ya Saa 10:30 Jioni kwa Saa za Ulaya, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu ya Jumatano ya Majivu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina, Jimbo kuu la Roma. Ibada hii ya Misa Takatifu itatanguliwa na Maandamano ya toba kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina. Wakati wote wa maandamano, waamini watasindikizwa na litania ya watakatifu pamoja na nyimbo za toba, mwaliko wa kufunga na kurekebisha vilema, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka kwa ari na moyo mkuu!

Mwanzoni mwa Kipindi cha Kwaresima, Mama Kanisa kwa namna ya pekee kabisa, anawataka watoto wake kuimarisha imani yao inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili; kielelezo makini cha imani tendaji. Ni kipindi cha kujikita katika fadhila ya matumaini, hekima, haki na nguvu inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka, ili iweze kutia shime na kuwategemeza Wakristo ambao wanaoteswa na kunyanyaswa sehemu mbali mbali za dunia. Changamoto kubwa wakati wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 ni kujitahidi kumwilisha sehemu ya Injili la Lazaro maskini na tajiri asiyejali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zake. “Neno ni zawadi; jirani yako ni zawadi pia”. Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.