2017-02-27 14:06:00

Papa Francisko: Jiaminisheni na kumtumainia Mungu katika maisha yenu!


Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, anayewatunza na kuwategemeza viumbe wake wote, daima anaviangalia kwa jicho la huruma na upendo, bondeni huku kwenye machozi, wasi wasi na mahangaiko ya kila siku, kiasi cha kuwanyima amani na utulivu wa ndani. Yote haya ni bure, kwani kamwe hayawezi kubadilisha matukio ya maisha, ndiyo maana Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kutohangaikia sana maisha ya hapa duniani, kwani yupo Mwenyezi Mungu, anayewapenda, ambaye kamwe hawezi kuwasahau watoto wake. Lakini, ikumbukwe kwamba, kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu si kuyapatia matatizo na changamoto za maisha kisogo! La hasha, bali ni kupambana na changamoto hizi kwa ari na moyo mkuu, kwa ujasiri na kwa kujiaminisha kwa Mungu anayewategemeza, kuwatakia na kuwajalia mema!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 26 Februari 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu yuko kati pamoja na watu wake, ni kimbilio salama, chemchemi ya amani na utulivu kwa waja wake. NiĀ  mwamba wa wokovu ambao mwanadamu anaweza kuukumbatia kwa uhakika bila ya kuporomoka, kwani anayejiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, kamwe hawezi kuanguka!

Mwenyezi Mungu ni ngome ya watu wake, rafiki, mwandani na Baba ambaye, wakati mwingine, waamini wanashindwa kuyatambua yote haya. Ni Mwenyezi Mungu anayewatakia mema, lakini wakati mwingine, waamini wanakengeuka na kumgeuzia Mungu kisogo, kiasi hata cha kukataa na kutema upendo wake wa kibaba, kiasi cha kubaki wakiwa wanajisikia kuwa ni watoto yatima ambao kamwe hawawezi kudeka hata siku moja! Waamini wanakwenda mbali sana na upendo wa Mungu pale ambapo wanamezwa na malimwengu, kwa kutafuta utajiri wa dunia hii, kiasi hata cha kukengeuka.

Tabia hii, anasema Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu ndiyo sababu ya mateso na mahangaiko ya ndani, hapa jambo la msingi ni kuutafuta Ufalme wa Mungu na mengine yote, watapewa kwa ziada. Uhakika wa kujiaminisha kwa Mungu unatolewa na Yesu mwenyewe kwenye hotuba yake ya Mlimani, kwani anayemtumainia Mungu kamwe hawezi kuhadaika, kama inavyojitokeza kwa marafiki ambao, mwishoni wanageuka kuwa ni wasaliti wakubwa. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya wokovu wa watu wake, kumbe, kipaumbele cha kwanza ni Mungu, kwani kwa uhakika mwanadamu hawezi kumtumikia Mungu na mali.

Uchaguzi huu anasema Baba Mtakatifu Francisko ni dhamana ambayo waamini wanapaswa kuifanya kwa moyo mkuu na saburi, dhamana inayopaswa kupyaishwa kila wakati, kwani kuna kishawishi kikubwa kinachoyaweka yote katika uchu wa fedha na mali; madaraka na anasa na matokeo yake, kuna vishwishi kibao vinavyoyazunguka mambo haya. Kwa wale wanaokengeuka na kumezwa na malimwengu, watakiona cha mtema kuni, kwani kwa wale wanaomchagua Mwenyezi Mungu na Ufalme wake unaosimikwa katika haki na amani, hawawezi kuyaona matokeo yake kwa haraka ikilinganishwa na wale waliomezwa na malimwengu. Kipaumbele kwa Mungu ni uamuzi unaofanywa na mwamini kwa kujiaminisha na kumtumainia Mwenyezi Mungu atakayetekeleza mpango wake kwa wakati muafaka. Matumaini ya Kikristo yanafumbatwa katika utekelezaji wa ahadi ya Mungu licha ya magumu na changamoto za maisha, kwani ni matumaini ambayo yanajikita katika uaminifu kwa Mwenyezi Mungu; uaminifu ambao kamwe hauwezi kupungua hata kidogo, kwani Mwenyezi Mungu ni: Baba, rafiki na mwanandani mwaminifu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia kujiaminisha kwa upendo na wema wa Baba wa milele, anayeishi naye milele, hapa mwaliko ni kuvuka changamoto za maisha hata mateso na madhulumu, kwa kuwa na matumaini kama yanavyoshuhudiwa na waamini sehemu mbali mbali za dunia! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee, mahujaji waliofika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Magonjwa Adimu Kitaifa. Amewashukuru wanafamilia kwa yale yote wanaoyotenda na anatumaini kwamba, wagonjwa na familia zao, wataweza kusaidiwa katika safari hii nzito katika masuala ya kitabibu na kisheria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.