2017-02-25 13:39:00

Askari wawezeshwe kuwa ni mashuhuda wa matumaini ya Kikristo!


Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, daima inaacha chapa ya kudumu katika maisha ya watu: kiroho na kimwili; inaharibu uhusiano na mafungamano ya kidugu, kitaifa na kimataifa, kiasi kwamba, hata askari wa vikosi vya ulinzi na usalama walioko mstari wa mbele wanaathirika vibaya. Kutokana na ukweli huu, Kanisa Katoliki limekuwa daima mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, linawasaidia kiroho, askari wa vikosi vya ulinzi na usalama, kutambua na hatimaye, kuwa kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya binadamu.

Ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Monsinyo Janusz S. Urbanczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirikisho la Ushirikiano wa Maendeleo na Usalama Kimataifa, OSCE katika mkutano wake wa 854 uliokuwa unajadili kuhusu “Viongozi wa kidini katika vikosi vya ulinzi na usalama; uhuru wa kuabudu wakati wa amani na vita”. Kanisa linapenda kuwatuma viongozi washauri wa maisha ya kiroho ili kuwasindikiza askari wa vikozi vya ulinzi na usalama katika kutekeleza dhamana na wajibu wao kila siku, daima wakiwa tayari kutekeleza na kuzima kiu ya maisha ya kiroho ya askari hawa.

Ni wajibu wa viongozi washauri kuwasaidia askari hawa kutambua tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, hasa zaidi utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mambo msingi ambayo pia askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wanapaswa kuyazingatia wanapotekeleza dhamana na wajibu wao wakati wa amani au pale wanapolazimika kwenda mstari wa mbele katika mapambano katika nchi wanamohudumia!

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wanapaswa kuwa wa kwanza kutambua hatari iliyoko mbele yao, ili kusimama kidete kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbali mbali za dunia; kwa kujikita zaidi katika kulinda na kuhudumia tunu msingi kama vile: uhai wa binadamu, haki, msamaha na uhuru. Kanisa kwa kutambua umuhimu wa viongozi washauri wa maisha ya kiroho kwa vikosi vya ulinzi na usalama, lilianzisha Jimbo la Kijeshi, lenye Askofu mwenye dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Askari wa vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na familia zao kwa kuwapatia huduma za kiroho na kichungaji.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna Majimbo 36 ya Kijeshi sehemu mbali mbali za dunia na kati yao Majimbo 17 yako kwenye Nchi wanachama wa OSCE; yanayohudumiwa na viongozi washauri wa maisha ya kiroho wapatao 2, 500; hawa ni mihimili ya uinjilishaji katika ukweli na amani. Kanisa linapania kuwawezesha askari wa vikosi vya ulinzi na usalama kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matumaini ya Kikristo yanayofumbatwa katika ushindi wa upendo dhidi ya chuki na uhasama; amani dhidi vita, kinzani na mipasuko ya kijamii! Monsinyo Janusz S. Urbanczyk, anaendelea kufafanua kwa kusema kwamba, Vatican inakazia pia uhuru wa kuabudu au uhuru wa kidini wakati wa amani na hata wakati wa vita. Hii inatokana na ukweli kwamba, uhuru wa kuabudi ni kati ya haki msingi za binadamu inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na kuridhiwa na OSCE katika Kanuni Msingi za Helsink. Hii ni haki msingi ambayo kila binadamu anapaswa kuifurahia, mahali, wakati na mazingira yoyote yale; iwe ni wakati wa amani au wakati wa vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.