2017-02-24 15:23:00

Umoja wa Mataifa: Bilioni 4 zinahitajika haraka kupambana na njaa


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antònio Guterres anasema, zinahitaji zaidi ya bilioni nne za kimarekani kwa ajili ya kupambana na baa la njaa nchini Yemen, Nigeria, Sudan ya Kusini na Somalia, ili kuokoa zaidi ya watu milioni 20 wanateseka kwa baa la njaa. Kiasi hiki cha fedha hakina budi kupatikana kabla ya mwisho wa mwezi Machi, 2017, vinginevyo, watu wengi watakufa kwa baa la njaa katika maeneo haya. Hadi sasa Umoja wa Mataifa umefanikiwa kukusanya kiasi cha dola za kimarekani milioni 90. Sababu kubwa ya njaa katika maeneo haya ni ukame wa kutisha, lakini pia vita pamoja na vitendo vya kigaidi. Watu katika maeneo haya pia wanatishiwa kushambuliwa kwa magonjwa ya mlipuko. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anakaza kusema kwamba, hali ni mbaya sana nchini Yemen kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo na watoto na wanawake ndio waathirika wakubwa. Watu nchini Yemen wanahitaji msaada wa haraka wa chakula.

Takwimu zinaonesha kwamba, watu zaidi ya milioni 2 wanahitaji haraka chakula cha msaada na wengine zaidi ya milioni 14 wanashambuliwa na utapiamlo wa kutisha, ambao ni sawa na asilimia 63% ya idadi ya watoto wote nchini Yemen. Huduma za afya zinaendelea kusua sua kutokana na vituo vingi vya huduma ya afya kushambuliwa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anaendelea kukaza akisema kwmaba, hali ni mbaya pia nchini Sudan ya Kusini. Watu zaidi ya milioni 5 na nusu wanakabiliwa na baa la njaa. Maeneo mengine yaliyokumbwa na ukame wa kutisha kiasi hata cha kuhitaji chakula cha msaada ni Gjibouti, Eitrea, Ethiopia, Somalia Sudan, Uganda na Kenya. Kambi za wakimbizi zinaendelea kufurika kwa watu wanaohitaji msaada wa chakula kutokana na baa la njaa, magonjwa; vita, mipasuko ya kijamii na kisiasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.