2017-02-24 12:03:00

Papa Francisko na wasaidizi wake "kujichimbia mlimani" kwa tafakari!


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, maarufu kama “Curia Roma” kuanzia tarehe 5 -10 Machi 2017 watapanda kwenda “Mlimani” Ariccia, nje kidogo ya mji wa Roma kwa ajili ya Mafungo ya kiroho yatakayoongozwa na Padre Giulio Michelini. Tema iliyochaguliwa ni “Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kadiri ya Injili ilivyoandikwa na Mtakatifu Mathayo.”  Tema hii ni muhimu sana kwa ajili ya kuwaandaa Wakristo kwa maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima ambacho kilele chake ni Juma kuu, Kanisa linapoadhimisha: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo.

Hii ni tafakari ambayo itagusia hali halisi ya maisha ya mwanadamu kadiri ya mwanga wa Injili ya Mathayo: familia, maskini, watu wanaoteseka na kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia; nao pia watapata nafasi katika tafakari hii ambayo Padre Michelini anasema, imemchukua siku kumi kuweza kuiandaa akiwa “amejichimbia” mjini Galilaya, hasa kule Kapernaumu, mahali ambako Yesu alianza maisha yake ya hadhara! Anataka kuwashirikisha wasikilizaji wake Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kadiri ya Mwinjili Mathayo ili kugusa msingi wa maisha ya kiroho kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu!

Padre Giulio Michelini anasema, ameamua kutumia mfumo wa mahubiri tofauti sana na watangulizi wake kama akina Padre Bruno Secondin aliyetafakari kuhusu “Nabii Eliya” pamoja na Padre Ermes Ronchi aliyejikita katika “Maswali wazi ya Injili”. Katika tafakari yake atawashirikisha wanandoa Mariateresa Zattoni na Gilberto Gillini, watakaoshirikisha furaha ya Injili ya familia, katika ushauri. Hawa watazungumzia kuhusu ushwishi wa mke wa Ponsio Pilato aliyetaka mme wake amwachie huru Yesu, lakini kwa bahati mbaya, ushauri huu ukagonga mwamba, Yesu akahukumiwa kuteswa, akafa Msalabani, lakini akafufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa.

Mtawa wa ndani kutoka Gubio, atasimulia jinsi Maria kule Bethania kwenye nyumba ya Simoni mkoma, alivyommiminia Yesu marhamu safi, kama sehemu ya mchakato wa kumwandaa Kristo Yesu kwa Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake! Padre Giulio Michelini anasema mtawa huyu atatumia tafakari iliyotolewa na Mtakatifu Clara, kwa kuwakumbusha umuhimu wa kuuandaa mwili wa Yesu kwa maziko, kwani maskini watakuwa nao daima! Anakumbusha kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, chanzo na lengo la Uinjilishaji.

Kunako mwezi Oktoba 2013, Padre Giulio Michelini anasema, Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea mjini Assisi, baada ya kuchagua jina la Mtakatifu Francisko kuwa msimamizi wake, ili aweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa “Laudato si” yaani utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; aweze kuwa mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya amani pamoja na kuendelea kuwa ni sauti ya maskini na “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi” alibahatika kumpatia nakala ya kazi yake kuhusu uchambuzi wa Injili ya Mathayo. Padre Giulio Michelini anasema ameguswa sana na ujasiri wa Baba Mtakatifu Francisko kumteua binafsi, ili kuwasindikiza “Jangwani” ili kujichotea nguvu ya maisha ya kiroho, tayari kupambana na maisha pamoja na utume wao kwa mwanga wa Fumbo la Pasaka! Kabla ya kukubali kupokea dhamana hii nzito, ilimbidi kwanza kuzungumza na Padre wake mshauri wa maisha ya kiroho kwa ushauri zaidi.

Katika tafakari yake kuhusu Ufufuko wa Kristo Yesu, atagusia mateso, changamoto na matumaini ya Wakristo huko Mashariki ya Kati; mambo ambayo yako mbele ya walimwengu. Mafungo haya yanalenga kuwasaidia washiriki wote kupokea na hatimaye kumwilisha maneno yaliyosemwa na Yesu mwishoni mwa maisha yake hapa duniani, ili hatimaye, kujiandaa kuadhimisha Fumbo la Pasaka, kwa kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu! Anataka wasikilizaji wake wawe karibu sana na Yesu pamoja na kumsikiliza kwa makini Mtakatifu Petro, ili kulisaidia Kanisa kujenga utamaduni wa kuwa karibu sana na familia ya Mungu wakati wote, ili kuionjesha uwepo endelevu wa Kristo katika maisha yake! Kanisa linapaswa kutangaza na kushuhudia Injili likiwa kati pamoja na watu wa Mungu!

Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 ni “Neno ni zawadi; jirani yako ni zawadi pia”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujitahidi kumwilisha ile sehemu ya Injili ya Lazaro Maskini na tajiri asiyejali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.