2017-02-24 15:00:00

Lindeni miundo mbinu dhidi ya mashambulizi ya kigaidi!


Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni alipokuwa akichangia mjadala wa wazi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa miundo mbinu nyeti dhidi ya mashambulizi ya kigaidi alisikika akisema, leo hii dunia inaonekana iko kwenye mapambano ya Vita Kuu ya Tatu ya Duniani, inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, sehemu mbali mbali za dunia.

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kusimama kidete kupinga biashara haramu ya silaha duniani inayoendelea kupandikiza kifo na kusababisha hofu kutokana na kushamiri kwa vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa anasema Askofu mkuu Auza kupambana vikali na vitendo vya kigaidi vinavyopandikiza hofu na mashaka pamoja na kuwatumia watu kushambulia miundo mbinu nyeti, kwa ajili ya mafao yao binafsi pamoja na kujijenga kisiasa na kitamaduni. Askofu mkuu Auza ameyapeleka mawazo yake huko Mashariki ya Kati ambako vita inaendelea kusababisha uharibifu mkubwa wa urithi na amana ya maisha ya kiroho na kitamaduni.

Maeneo ambayo kwa miaka mingi yalihesabiwa kuwa ni urithi wa utamaduni na maendeleo ya binadamu huko Mashariki ya Kati yameharibiwa vibaya sana na vitendo vya kigaidi katika miaka ya hivi karibuni. Licha ya maeneo haya ya kitamaduni, lakini pia kumekuwepo na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya shule, hospitali na kwenye vyanzo vya maji pamoja na maeneo ya ibada kama ilivyojitokeza hivi karibuni sehemu mbali mbali za dunia!

Askofu Mkuu Auza anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba inawalinda raia na mali zao kama inavyobainishwa kwenye Katiba ya Umoja wa Mataifa dhidi ya mashambulizi ya kigaidi. Miundombinu nyeti inapaswa kulindwa kikamilifu dhidi ya mashambulizi ya kigaidi, ili kuepuka maafa makubwa kwa maisha ya watu pamoja na ukosefu wa huduma msingi kama vile elimu, afya na maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya raia. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kupinga sera na mbinu mkakati unaotaka kuwanufaisha watu wachache wanaojihusisha na biashara haramu ya silaha inayoendelea kunuka damu ya watu wasiokuwa na hatia! Hiki ni kielelezo cha ubinafsi wa hali ya juu, ambao unaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao!

Ujumbe wa Vatican umetumia fursa hii kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba, linadhibiti kwa kiasi kikubwa biashara ya silaha duniani: kwa kuzuia utengenezaji, usambazaji na matumizi yake, hasa katika maeneo ambamo kuna vita, migogoro na mipasuko ya kijamii. Pale inapofaa zaidi, biashara ya silaha ipigwe rufuku ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia! Lengo hili linaweza kufikiwa ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itaonesha ushirikiano na mshikamano wa dhati kwa ajili ya amani, usalama, ustawi na mafao ya wengi. Sera na mikakati ya udhibiti wa silaha mipakani uimarishwe zaidi sanjari na kudhibiti magenge ya uhalifu kimataifa, yanayotumia vita, kinzani na mipasuko ya kijamii kwa ajili ya kujinufaisha kwa kutumia biashara haramu ya silaha. Makundi ya kigaidi yanaendelea kupandikiza maafa, hofu na mashaka kwa watu sehemu mbali mbali za dunia! Hapa, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa karibu zaidi kwa njia ya kubadilisha uzoefu, taarifa na mbinu za kupambana na vitendo vya kigaidi.

Ikumbukwe kwamba, vitendo vya kigaidi vinavuka mipaka ya nchi, kumbe, kuna haja pia ya kudhibiti waandaaji watakaotumiwa kujitoa mhanga kwa ajili ya mashambulizi ya kigaidi; kwa kudhibiti pia vyanzo vyao vya fedha zinazogharimia vitendo vya kigaidi pamoja kuratibu mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi, kitaifa, kikanda na kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.