2017-02-23 11:47:00

Maendeleo ya watu yaboreshe maendeleo ya umoja na mshikamano wa watu


Ilikuwa ni tarehe 26 Machi 1967, Miaka 50 iliyopita, Mwenyeheri Paulo VI alipoandika Waraka wa Kitume, “Populorum progressio” yaani “Maendeleo ya watu” akakaza kusema, maendeleo ni jina jipya la amani. Waraka huu ni mwendelezo wa mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican; Kanisa katika ulimwengu mamboleo, unaofumbata kwa namna ya pekee masuala ya kiuchumi na kijamii. Anagusia maendeleo endelevu ya binadamu; mshikamano unaofumbatwa katika kanuni ya auni, ili kulinda, kudumisha na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mwenyeheri Paulo VI anasema, maendeleo ya sayansi na teknolojia, yasaidie mchakato wa maboresho ya maisha na utu wa binadamu sanjari na kutambua uwepo endelevu wa Mungu katika historia na maisha ya binadamu. Maendeleo ya kweli yanajikita katika mchakato wa kukata kiu ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati, ili kufikia utimilifu wa mwanadamu, unaoongozwa na tunu msingi za maisha ya kiroho!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma, ili kujenga na kuimarisha maendeleo ya watu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji, kwa kusoma alama za nyakati ili kujibu changamoto zinazoendelea kujitokeza wanasema, sasa kuna haja ya kusonga mbele zaidi kwa kutoka katika maendeleo ya watu na kujikita katika umoja wa watu “Populorum communio”.

Hiki ndicho kiini cha Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwenye Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji kwa Mwaka 2017. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu kuweza kujizatiti kikamilifu kubainisha malengo, kutoa nyenzo za utekelezaji wa majibu muafaka ili kuzima kiu ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo! Changamoto kubwa ni ukosefu wa misingi ya haki, amani na mshikamano kati ya watu; mambo ambayo yamepelekea dunia kuwa ni uwanja wa fujo, vurugu, vita na kinzani za kila aina, kama inavyojionesha kwa namna ya pekee huko Mashariki ya Kati.

Kumekuwepo na mashambulizi ya kigaidi yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu, bila kusahau wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, lakini kwa bahati mbaya, ni watu wanaokabiliana uso kwa uso na kifo, kiasi kwamba, Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi la wazi, lisiokuwa na alama kwa wale wote wanaomezwa tumboni mwake! Hii ni changamoto inayogusa maisha na utume wa Kanisa, linalopaswa kuwa kweli ni Sakramenti ya wokovu na matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha! Huu ni wakati muafaka wanasema Maaskofu Katoliki kutoka Ubelgiji wa kuhakikisha kwamba, Kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa zinamwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kujibu kilio cha watu wanaoteseka na kukata tamaa ya maisha.

Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia; maendeleo haya yanapaswa sasa kutafsiriwa na kuwekwa katika mchakato wa kuimarisha maendeleo ya umoja wa familia ya Mungu duniani; kwa kukazia: haki, amani na mshikamano wa upendo unaoongozwa na kanuni auni. Hii ndiyo dira na mwelekeo unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kulitaka Kanisa kuwa kweli ni Sakramenti ya huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi; kwa kuwajali na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji; kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wote hawa waonjeshwe huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani wala ubaguzi!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji, linawataka waamini kuwa mstari wa mbele katika kusongezesha mbele mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; kwa njia ya huduma makini inayopania kugusa, kuganga na kuwaponya watu: kiroho na kimwili; sanjari na kuwapatia huduma makini inayotolewa na Kanisa katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu! Maendeleo ya umoja wa watu yawasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua na kuthamini utu na heshima ya binadamu wote; kwa kutubu na kumwongokea Kristo Yesu kama mtu binafsi pamoja na Jumuiya ya waamini na kijamii katika ujumla wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ubelgiji linakiri kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu mamboleo yamekuwa na mafao makubwa sana kwa binadamu, lakini pia yamechangia kwa baadhi ya watu kujikuta wakiwa wametelekezwa pembezoni mwa maendeleo haya kama “magari mabovu”. Maendeleo makubwa katika tasnia ya habari na mawasiliano yamepelekea mabadiliko makubwa hata katika mfumo wa maisha ya binadamu. Umefika wakati kwa familia ya Mungu kujikita katika kukuza na kudumisha haki jamii, ili kweli sera na mikakati ya kiuchumi iweze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi.

Haki jamii na mshikamano wa kiinjili ni nyenzo msingi na chachu ya mabadiliko katika masuala ya uongozi wa Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni ufahamu wa kijamii kimataifa unaopania kudhibiti ukosefu wa haki msingi za binadamu unaozalishwa na uchumi huria usioguswa na mahangaiko ya watu wengine katika jamii pamoja na vita ambavyo kimsingi ni kielelezo cha ubinafsi, uchu wa mali na madaraka! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti katika kutatua kinzani na migogoro ya kitaifa na kimataifa kwa njia ya majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi. Rasilimali na utajiri wa nchi viwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Rushwa ni adui wa haki, watu wajenge utamaduni wa kuridhika na maisha yao, tayari kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa na kwamba, hakuna njia ya mkato kwa ajili ya kujipatia maendeleo ya kweli! Kuna haja ya kujenga na kudumisha utandawazi wa mshikamano ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji; kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya watu. Maendeleo ya umoja wa watu, yakifumbatwa katika huruma ya Mungu; amani itaweza kutawala tena duniani na hivyo kuwa ni kichocheo cha maendeleo endelevu ya binadamu! Watu wasimame kidete kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote sanjari na kuondokana na utamaduni wa kifo. Maendeleo ya kweli yanafumbatwa katika umoja wa watu na msingi wake ni haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.