2017-02-22 14:39:00

Watu milioni 17 wanahofiwa kukumbwa na baa la njaa Pembe ya Afrika!


Watu zaidi ya milioni kumi na saba wanatishiwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kwenye Nchi zilizoko kwenye Pembe ya Afrika kutokana na ukame wa muda mrefu. Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Matiafa, UNICEF linasema, zaidi ya watu millioni tano kwenye mikoa miwili iliyoko Sudan ya Kusini wanakabiliwa na uhaba mkubwa sana wa chakula; hawa ni sawa na asilimia 50% ya idadi ya watu wote wa Sudan ya Kusini. Hali hii inaendelea kugumishwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyojitokeza tangu kunako mwaka 2013, kiasi cha kuathiri uzalishaji wa chakula hadi kufikia mwaka 2016.

Mashirika ya misaada ya kiutu yanaendelea kujipanga kwa ajili ya kutoa huduma maeneo ya Upper Nile, Jonglei, Magharibi na Mashariki mwa Sudan ya Kusini. Wachunguzi wa masuala ya kijamii wanakaza kusema, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii nchini Sudan ya Kusini ni chanzo kikuu cha maafa kwa raia; hali inayokuza pia baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kwa watoto wengi vijijini! Bwana Serge Tissot, mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa  Mataifa nchini Sudan ya Kusini katika taarifa yake anasema baa la njaa kwa sasa linaendelea kupanuka na kuongezeka maradufu nchini Sudan ya Kusini.

FAO inakumbusha kwamba, kunako mwaka 1998, Sudan wakati ule, ilikuwa kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe, kiasi kwamba baa la njaa liliwatikisa watu wengi sana. Hali hii inaweza kujirudia tena, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitajizatiti kikamilifu kutafuta chakula cha msaada kwa ajili ya wananchi wa Sudan ya Kusini. Watu milioni kumi na saba wanatishiwa na baa la njaa huko Gjibouti, Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan, Uganda na Kenya na hata Tanzania.

Baa la njaa linaendelea kuhatarisha maisha ya wakimbizi wanaoishi kwenye kambi za wakimbizi Afrika Mashariki, watu ambao wamekimbia nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi, sasa wako hatarini kutoweka kwenye uso wa dunia kutokana na baa la njaa. Vita, kinzani za kijamii pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya mambo yanayoendelea kuchangia kupanuka kwa baa la njaa katika nchi za Pembe ya Afrika na kwamba, idadi hii inaweza kuongezeka maradufu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.