2017-02-22 15:21:00

Tunzeni na kuendeleza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi!


Sera na mikakati ya kimataifa, kikanda na kitaifa ni mambo msingi ambayo ujumbe wa Vatican umeyapatia kipaumbele cha pekee kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira ya bahari, rasilimali pamoja na utajiri wake ili visiharibiwe kwa shughuli zinazofanywa na binadamu! Ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani wakati akichangia mada kuhusu lengo la kumi na nne la maendeleo endelevu linaloitaka Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika kulinda na kutumia kwa makini bahari, rasilimali na utajiri uliomo humo kwa busara zaidi.

Askofu mkuu Bernadito Auza anakaza kusema, sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote vimepembuliwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto kubwa zinazoendelea kutishia usalama na maisha ya binadamu katika ulimwengu mamboleo. Hii inatokana na uchafuzi mkubwa unaofanywa kwenye bahari, kuongezeka kwa acidi baharini, kupungua kwa viumbe hai baharini bila kusahau uharibifu mkubwa unaofanywa na binadamu katika fukwe za bahari.

Changamoto zote hizi anasema Askofu mkuu Auza, zinahitaji Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa majadiliano utakaosaidia kulinda na kudumisha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kusimama kidete kwa ajili ya kulinda mafao ya wengi; haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Majadiliano haya yasaidie kuibua sera na mbinu mkakati wa pamoja utakaotumika katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera hizi kwa ajili ya mafao ya wengi.

Haya ni majadiliano yanayowahusisha watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha, yaani: wanasiasa, viongozi wa kidini, wataalam, wanafalsafa; wachumi na watunga sera bila kuwasahau watu wa kawaida ambao kimsingi ndio waathirika wakubwa! Kumbe, ujumbe wa Vatican katika maandalizi ya utekelezaji lengo la 14 katika Malengo ya Maendeleo Endelevu unapenda kukazia kwa namna ya pekee ushirikishwaji wa viongozi wa kidini kwani, athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema, kumbe, haya pia ni mapambano ya kimaadili na maisha ya kiroho dhidi ya mifumo ya maisha inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, nyumba ya wote.

Askofu mkuu Bernardito Auza anahitimisha mchango wake katika mkutano wa maandalizi ya utekelezaji wa lengo la 14 la Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwashirikisha watu wengi zaidi pamoja na na kufanya uragibishaji wa kimataifa, ili kulinda na kudumisha mazingira, rasilimali na utajiri unaopatikana baharini, ili kweli uweze kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi! Yote haya yanawezekana, ikiwa kama kutakuwepo na sera makini ya uvuvi salama na endelevu; udhibiti wa uchafuzi wa mazingira nyumba ya yote pamoja na kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na maboresho ya maisha ya wavuvi wadogo wadogo pamoja na familia zao; bila kuwasahau maskini ambao kimsingi ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Sheria za kimataifa, kikanda na kitaifa zisaidie katika mchakato wa utekelezaji wa lengo la 14 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, ifikapo mwaka 2030; utekelezaji unaohitaji majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi kwa kuwahusisha wadau wengi zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.