2017-02-22 09:56:00

Majadiliano ya kidini kati ya Vatican na Chuo Kikuu cha Al-Azhar


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini akiwa ameambatana na Askofu Miguel Angel Ayuso Giuxot, Katibu mkuu wa Baraza, kuanzia tarehe 22- 23 Februari 2017 wako mjini Cairo, Misri ili kushiriki katika semina iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Al-Azhar. Semina hii inaongozwa na kauli mbiu “Mchango wa Al-Azhar al Sharif na Vatican katika mapambano dhidi ya misimamo mikali ya kidini, kiimani na vita kwa jina la dini". Askofu mkuu Bruno Musarò, Balozi wa Vatican nchini Misri ana ambatana na wageni wake kutoka Vatican.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 23 Mei 2016, Baba Mtakatifu Francisko alibahatika kukutana na kuzungumza na Imam Mkuu wa Al-Azhar, Sheikh Ahmad Al Tayyib. Tangu wakati huo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini amefanya ziara kadhaa nchini Misri ili kukutana na kuandaa mpango mkakati wa ushirikiano kati ya Vatican na Chuo kikuu cha Al-Azhar. Majadiliano haya ni sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya tarehe 24 Februari 2000, Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Taasisi ya Dini ya Kiislam yenye madhehebu ya  Kisunnita. Huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kidini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.