2017-02-22 16:33:00

Kardinali Desmond Connell Askofu mkuu mstaafu wa Dublini kuaga dunia


Kardinali Desmond Connell, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland ameaga Dunia mara baada ya kuugua kwa muda mrefu akiwa anakaribia miaka 91 usiku wa kuamkia tarehe 21 Februari 2017. Kufuatia kifo cha Kardinali Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dublin, naye Baba Mtakatifu Francisko akiwa na huzuni ,ametuma salama za rambirambi  kwa viongozi wa dini , watawa , na waamini walei  wa Jimbo Kuu kupitia kwa Askofu Mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo Kuu la Dublin.

Baba Mtakatifu anasema kuwa anakumbuka utume wake kama Padre na askofu Mkuu wa Dublin na mchango wake kwa Kanisa la Ireland , hasa katika kitengo cha mafunzo ya falsafa; anamwombea roho yake iungane na kupata huruma ya Mwenyezi Mungu. Na kwamba katika matumaini na hakika ya ufufuo,anatuma Baraka zake za kitume kwa wote wanao omboleza kifo cha marehemu Kardinali Connell  ili wapate  faraja na amani katika Bwana Yesu.
Kardinali Desmond Connell alizaliwa mji mkuu wa Ireland tarehe 24 Machi 1926.Alipata daraja la upadre tarehe 19 Mei 1951,na kuteuliwa kuwa askofu Mkuu wa Jimbo kuu katoliki  la Dublin tarehe 21 Januari 1988 .Aliteuliwa kuwa Kardinali na Mtakatifu Yohane Paulo wa II tarehe 21 Februari 2001, na alikuwa amestaafu utume wake wa Jimbo kuu tangu tarehe 26 Aprili 2001. 

Kardinali Connell amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Kanisa kama vile kuwa mmoja wa Kamati ya kitaalimungu ya Baraza la Maaskofu wa Ireland; kuongoza jumuiya tatu za watawa wa ndani. Halikadhalika amewahi kuwa Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland pia kamati ya mafundisho ya kitaalimungu na ya kiekumene. Mwishoni, Kardinali Connel amewahi kuwa rais wa kamati ya Chuo Kikuu cha falsafa.

Sr Angela Rwezaula 

Idhaa ya kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.