2017-02-22 15:03:00

Iweni ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili ndani ya familia


Baraza la Maaskofu Katoliki India, CCBI baada ya maadhimisho ya mkutano wake mkuu wa 29 uliohitimishwa hivi karibuni huko Bhopal, Madhya Pradesh, linaitaka familia ya Mungu nchini India kuhakikisha kwamba, inajenga na kudumisha Injili dhidi ya utamaduni wa kifo; wanandoa watarajiwa wanapewa majiundo awali na endelevu ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia; tayari kutangaza na kushuhudia: ukuu, wema na utakatifu wa Sakramenti ya Ndoa katika maisha ya kifamilia. Wanandoa wapya wanapaswa kusindikizwa katika maisha na utume wao, ili kuweza kupata ukomavu katika maisha ya ndoa, tayari kusimama kidete kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza katika hija ya maisha yao ya kila siku, mintarafu mwanga wa Injili!

Kanisa linapaswa kuwa karibu sana na wanandoa waliotengana na baadaye wakaamua kuoa au kuoana, ili kuwasaidia kuonja Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika safari ya maisha yao ya kiroho, kwa kuwashirikisha katika maisna na utume wa Kanisa! Haya ni mambo msingi yaliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki India katika ujumbe wake kwa familia ya Mungu nchini humo! Maaskofu wanakazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa majiundo awali na endelevu kwa mihimili ya utume wa familia, ili kutambua changamoto, matatizo, kinzani na fursa zinazopatikana katika kukuza na kudumisha Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai wa maisha ya binadamu! Umaskini wa hali na kipato; magonjwa, njaa na umaskini ni kati ya changamoto kubwa za kifamilia nchini India!

Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki India imekuwa ni fursa ya kupembua kwa kina na mapana Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”, kwa kuongozwa na kaulimbiu “Ukuzaji wa furaha ya upendo ndani ya familia zetu. Maaskofu wanasea, familia ni kiini cha jamii, shule ya utakatifu, haki, amani upendo na mshikamano wa dhati. Zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anaikirimia jamii na Kanisa katika ujumla wake. Wanafamilia kutoka majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini India, walipata nafasi ya kutolea ushuhuda wa tunu msingi za Injili ya familia, changamoto, matatizo na fursa walizo nazo katika maisha na utume wa Kanisa.

Baraza la Maaskofu Katoliki India linakaza kusema, kuna watu milioni 300 wanaoishi katika hali ya umaskini, hasa katika maeneo ya vijijini. Wanakabiliwa na huduma hafifu za afya na elimu, kiasi cha kushindwa kuchangamkia fursa za ajira kwa ajili ya kuziwezesha familia zao. Waathirika wakuu ni watoto, wasichana na wanawake. Licha ya kiwango hiki cha umaskini nchini India, lakini familia nyingi hata katika umaskini wake, zimekuwa ni chemchemi na vitalu vya miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Kuna umati mkubwa wa Wakleri na Watawa kutoka India wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za dunia.

Maaskofu 138 kutoka katika Majimbo 132 ya Kanisa Katoliki nchini India wameshiriki katika mkutano huu. Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu ndiye aliyekuwa mwezeshaji mkuu kuhusu Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Katika hotuba yake elekezi amekazia kwa namna ya pekee kuhusu Utenzi wa Upendo kama unavyofafanuliwa na Mtume Paulo (1Kor. 13: 4-7). Mwaliko kwa waamini kurejea tena na tena katika utenzi wa upendo ili kukuza na kudumisha furaha ya upendo ndani ya familia; furaha inayomwilishwa siku kwa siku. Takwimu zinaonesha kwamba, waamini wa Kanisa Katoliki nchini India ni takribani milioni 28, sawa na asilimia 3% ya wananchi wote wa India.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.