2017-02-21 10:43:00

Miaka 60 ya uhuru, Ghana kuwekwa wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Giuseppe Bertello, Rais wa Serikali ya mji wa Vatican, kuwa mwakilishi wake maalum katika kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 40 tangu Serikali ya Ghana ilipoanzisha uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican, sanjari na kumbu kumbu ya miaka 60 tangu Ghana ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingireza. Maadhimisho haya yataanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 3 Machi na kufikia kilele chake hapo tarehe 6 Machi 2017.

Kunako tarehe 6 Machi 1957, Ghana iliyokuwa inajipatia uhuru wake, ikawekwa wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ndiyo maana, kuanzia tarehe 23 Februari 2017, hadi tarehe 3 Machi 2017, Familia ya Mungu nchini Ghana inaadhimisha Novena maalum kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kujiweka tena wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Askofu mkuu Chrales G. Palmer-Buckle, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana ndiye anayeratibu zoezi zima la maadhimisho haya kiroho! Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma na neema ya Mungu; msamaha na upendo; unyenyekevu, upole na maisha mapya.

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kiini cha Sakramenti za Kanisa, Moyo Mtakatifu uliotobolewa kwa mkuki, humo yalitoka Maji na Damu: alama ya Sakramenti ya Ubatizo na Ekaristi Takatifu; mwanzo na hatima ya maisha na utume wa Kanisa, ni chemchemi ya utakatifu na ukamilifu wa maisha ya Kikristo! Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana kwa kutambua utajiri unaofumbatwa katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, linataka tena kuiweka wakfu familia ya Mungu nchini humo tarehe 4 Machi 2017 katika Ibada ya Kiekumene itakayoongozwa na Askofu mkuu Jean-Marie Speich, Balozi wa Vatican nchini Ghana akisaidiana na Askofu mkuu Philip Naameh, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana. Ibada hii inatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Nana Dankwa Akufo Addo wa Ghana, atakayewawakilisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.