2017-02-20 07:21:00

Ufafanuzi wa kina: Toba ya ndani na kutamani matakatifu!


Baada ya Sinodi maalumu ya Maaskofu kuhusu masuala ya ndoa na familia, iliyofanyika mwezi Oktoba 2015, Baba Mtakatifu Francisko ameandika Wosia wa kitume, Amoris laetitia, Furaha ya upendo ndani ya familia. Wosia huu wa kitume umehitaji kueleweshwa vema juu ya nini kinaelekezwa hasa katika sura ya nane, inayozungumzia mipango ya kichungaji katika kuwasaidia wale wanoishi kinyume na taratibu za ndoa kadiri ya kanuni sheria za Kanisa.

Katika wimbi la maoni na tafsiri mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vigugumizi vingi katika kulishughulikia suala hilo, Kardinali Francesco Coccopalmerio, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Nyaraka za Kisheria, anaandika kitabu kuelezea sura ya nane ya Amoris laetitia. Lengo la mwandishi, sio kuweka maoni yake binafsi, bali mwaliko kwa wasomaji kutotoa majibu ya haraka kabla ya kuelewa kilichoandikwa na namna ya kukishughulikia.

Wosia wa kitume, Amoris laetitia,  yaani Furaha ya upendo ndani ya familia, unaleta upya wa kichungaji unaofumbatwa na tamaduni ya Mafundisho tanzu ya Kanisa, kuendana na hali halisi ya jamii ya leo: misingi ya taalimungu juu ya ndoa na familia imeungana bila kuchangamana na misingi ya taalimungu juu ya maadili; ufahamu wa familia ya kikristo unachambuliwa na kutofautishwa na busara ya kichungaji katika kuwasindikiza kiroho wale ambao kwa namna moja au nyingine ndoa zao zimepata misukosuko ya kushindwa kubaki waaminifu katika misingi ya ndoa na familia. Hii haina maana kunakutengeneza aina za ndoa na familia za kikristo, la hasha, bali ni ulazima wa busara ya kichungaji katika kuhangaikia kila mwana Kanisa katika hali yake, bila kubaguliwa, na bila kuvunja taratibu wala kwenda kinyume na mafundisho ya Kanisa.

Kitabu hicho cha Kardinali Coccopalmerio, katika sura tatu za awali, kinaweka misingi ya ufafanuzi kitaalimgu: anatoa mwanga kwa mihimili isiyotikiswa ya mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia; mwelekeo wa kichungaji kwa wale wanaoishi tofauti na taratibu za Sheria Kanuni za Kanisa; hali za dhamira za waamini hao na changamoto ya kuruhusiwa kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa. Ugumu na mahangaiko ambayo hata mwandishi anakiri wazi uwepo wa ugumu huo, ni suala la kufahamu hali binafsi za dhamira za wahusika na namna ya kuwashirikisha kwenye Sakramenti za Kanisa bila kutimulia mavumbi mafundisho ya Kanisa, na kuwaacha baadhi wakiisoma namba ya “Taxi bubu”. Kinachomfanya mhusika kujifungia mwenyewe ushiriki wa Sakramenti, ni kuwa katika hali ya dhambi ya mauti, na hivyo Kanisa linachukua tahadhari ya kutomuacha mwamini huyo, kutenda jambo lingine linalomuingiza kwenye dhambi nyingine tena.

Waamini wanaoongelewa kuwatazama na kuwasaidia katika kiwango cha Sakramenti za Kanisa, ni wale ambao wanatambua na kukiri wazi kuwa wanaishi katika hali ya dhambi, wanahangaika na changamoto ya kujinasua. Kumbe, wanakuwa na nia ya kujinasua, au walau hamu ya kubadili maishi yao na kumpendeza Mungu. Waamini waliofika katika kilele cha hamu ya kujirekebisha lakini kunakuwa na changamoto ya kuvunja mahusiano yasiyo halali kwa kutengana na wakati huo huo kuhakikisha malezi bora ya watoto, kwa hakika wanahitaji msaada wa kutuliza kiu yao hiyo, lakini kwa namna ambayo wataweza kuendelea kulea na kuwatunza watoto kwa namna stahiki. Mafundisho haya yamekuwapo pia katika Waraka wa Kitume juu Wajibu wa familia za kikristo katika ulimwengu mamboleo, Famliaris consortio, Na. 84, kadiri ya mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, juu ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo, Gaudium et spes, Na. 51.

Kardinali Coccopalmerio, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Nyaraka za Kisheria anasema katika kitabu chake, "mkanganyo, dukuduku, kigugumizi na hofu ya kukosea" kuhusu nini Baba Mtakatifu Francisko amemaanisha katika Wosia wa Kitume, Amoris laetitia, vinapaswa vieleweke kwamba: Wanaoishi mahusiano yasiyo halali kisheria ndani ya Kanisa, wanaweza kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kitubio na Ekaristi Takatifu kwa kuzingatia masharti mawili; kwanza wawe wanajitambua kosa lao na wanayo nia ya dhati ya kubadili mwenendo wao wa maisha, pili kufuatana na sababu za msingi kama malezi bora ya watoto, hawawezi kuifikia nia hiyo kwa kutengana au kufunga ndoa sababu ya vizuizi vya kisheria vya ndoa ya awali. Masharti haya mawili, yanapaswa yachambuliwe na kutathiminiwa kwa umakini mkubwa na viongozi wa Kanisa, kwa kila familia, sababu wahusika wanapaswa kutoendelea na tendo la ndoa, na siyo kutoa rukhusa kiholela ya kushiriki Sakramenti "kama ugawaji wa njugu".

Ieleweke tangu awali, na kila wakati ambapo tathimini hiyo inafanyika ili kutoa rukhusa hiyo maalumu kwamba, mafundisho msingi ya Kanisa yanabaki katika upamoja wake kwenye hili suala. Kwanza kabisa, mafundisho juu ya ndoa ya kikristo ya mke mmoja, mme mmoja, iliyo halali na isiyovunjika kamwe. Pili mafundisho juu ya majuto ya dhambi na kunuia kutotenda tena dhambi hiyo, ingawa sasa kwa wakati huu kukamilisha majuto hayo kwa kutengana kabisa kunakuwa na kikwazo kikubwa kisichovukika bila kusababisha madhara mengine hatarishi na pengine makubwa zaidi.

Tatu ni Mafundisho juu ya Neema ya Utakaso, ambayo inamruhusu mtu kushiriki Sakramenti za Upatanisho na Ekaristi Takatifu, iwapo mhusika anakuwa amefanya majuto ya rohoni na ya kweli ili kubadilika. Hali hii ya majuto, ndiyo inayomsogeza mwamini katika Sakramenti. Hata hivyo, izingatiwe sana, tena sana, kwamba, ni katika ile tu hali ambayo inashindikana kabisa kufanya mabadiliko ya maisha ghafla, bila madhara makubwa zaidi.

Kardinali Gerhard Müller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, katika mahojiano na gazeti la “Rheinische Post” la Ujerumani hivi karibuni, anasisitiza kwamba Sharti la toba ya dhati, kwa wahusika kuachana kabisa na tendo la ndoa, ni la lazima kuzingatiwa kabla ya kuwaruhusu kushiriki Sakramenti, na kwamba wasiendelee tena kuhusika nalo baada ya hapo.

Mtakatifu Yohane Paulo II anafundisha kwamba, Mapadri waungamishaji wanapaswa kuwa wanakumbuka kila wakati katika huduma hiyo, kuwa uwezekano wa mwanadamu kuanguka tena dhambini, siyo hukumu ya kutilia shaka nia thabiti ya muungamaji kubadili maisha yake. Mwanadamu akumbuke katika nia yake njema ya majuto na kubadili maisha, kwamba anahitaji pia msaada wa Neema ya Kristo hasa katika sala ili adumu katika mwenendo bora.

Kuanzia sura ya nne hadi ya sita, Kardinali Coccopalmerio anadadavua mahusiano yaliyopo kati ya mafundisho na sheria kanuni za Kanisa kwa kuzingatia uhalisia wa mwanadamu alivyoumbwa. Kuna zile sifa na taratibu za jumla na zile binafsi. Hivyo katika baadhi ya mahangaiko ya maisha ya mwanadamu, ni muhimu kumzingatia kila mmoja kwa hali yake, uwezo wake, udhaifu wake, mazingira yake na namna ya kumsaidia abaki na kujisikia sehemu ya Kanisa kwa kutumia huduma mbali mbali za Kanisa na Ukarimu wa kidugu. Katika sura ya saba na ya mwisho, Kardinali Coccopalmerio anadadavua tathimini ya uhalisia wa mambo kwa kupitia mtu. Hii ndiyo namna ya Utume wa Baba Mtakatifu Francisko, anazingatiwa mtu kwanza katika kuchambua na kutathimini hali halisi inayokabiriwa. Kumbe, mafundisho ya Kanisa yanabaki kusimamiwa katika misingi yake yote, na kuhakikisha kondoo aliyepotea anatafutwa na kurudishwa kundini kadiri ya taratibu.

Kardinali Müller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anatoa angalisho kwamba maaskofu waepuke kutoa tafsiri huria za Nyaraka za Kanisa, badala yake waendelee kufundisha na kutoa huduma za kichungaji kadiri ya maelekezo na tafsiri rasmi zinazotolewa na vyombo rasmi kwa ajili ya hayo kadiri ya itifaki ya Kanisa.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.