2017-02-20 10:31:00

Maswali ya watoto wadogo kwa Baba Mtakatifu Fransicko!


Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume kwenye Parokia ya Mtakatifu Maria Josefa wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Kuu la Roma, Jumapili tarehe 19 Februari 2017, alipata nafasi ya kukutana na makundi mbali mbali ya waamini Parokiani hapo pamoja na kujibu maswali kadhaa. Parokiani hapo, Baba Mtakatifu alipokelewa na Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, Askofu msaidizi Giuseppe Marciante pamoja na Paroko Francesco Rondinelli. Amewaungamisha waamini wanne waliokuwa wamejiandaa pamoja na kuzungumza na watoto Parokiani hapo!

Baba Mtakatifu anasema, alichaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika mkutano wa Makardinali 115, waliosali, wakatafakari kwa kina na mapana na hatimaye, wakamwomba Roho Mtakatifu aliyewasaidia kumchagua. Mchakato huu unaongozwa kwa kiasi kikubwa na sala pamoja na tafakari. Kumbe, ni Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa kupitia kura za Makardinali anayemchagua Mashemasi mmoja kuwa Papa kadiri ya mahitaji ya Kanisa kwa wakati huo! Kama ilivyo kwa wote, Papa pia atafariki dunia au atalazimika kung’atuka kutoka madarakani kama alivyofanya Papa Mstaafu Benedikto XVI, baada ya kuona kwamba, afya yake ilikuwa haimpatii nafasi ya kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kila Papa ana karama na mchango wake maalum kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Baba Mtakatifu amewaambia watoto wanaojindaa kupokea Sakramenti ya Kipaimara kwamba, alipokuwa mtoto mdogo alitamani sana kuwa “Muuza nyama” kwani alikuwa anafurahia sana kazi ya muuza nyama ambaye alikuwa ni jirani yake. Ili kuweza kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro sharti la kwanza ni kuwa Mkristo mwema, Padre na Askofu. Katika historia ya Kanisa kuna baadhi ya Mapapa walikuwa ni Makardinali waliochaguliwa na watu kuliongoza Kanisa. Lakini kwa sasa Sheria za Kanisa zinatoa ruhusa kwa Makardinali wenye umri chini ya miaka 80 kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata yeye katika maisha ameguswa na kutikishwa sana katika masuala ya afya, tangu bado akiwa ni kijana mwenye umri wa miaka 20, lakini Mwenyezi Mungu amemsaidia kwani maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu; matatizo na changamoto za maisha zinakuja na kupita na maisha yanasonga mbele. Anasema, kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki ni dhamana na wajibu mkubwa, kwani ni Khalifa wa Mtakatifu Petro, kumbe, anawajibika kufanya vyema zaidi kama Askofu wa Jimbo kuu la Roma na Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano ndiyo makao makuu ya Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu amewafafanulia watoto kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu yaani: Mungu mmoja mwenye Nafsi Tatu: Mungu Baba ni Muumbaji; Mungu mwana ni Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ndiye anayeliongoza na kulitakatifuza Kanisa. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa na Mtakatifu Yosefu mtu mwenye haki ni Baba mlishi wa Yesu.

Baba Mtakatifu alipata pia nafasi ya kuzungumza na wagonjwa na kusali pamoja nao katika hali ya faragha. Amewashukuru wanafamilia wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Amewataka kutambua uwepo wa Kristo kati yao kwa njia ya maskini na wale wote wanaohitaji msaada! Kwa njia ya sala, majitoleo na ushuhuda wao wanasaidia kulitangaza Neno la Mungu. Anawaomba kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya Sala na Sadaka zao! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia wote heri na baraka katika maisha yao na hata wale ambao hawakubahatika kufika kutokana na sababu mbali mbali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.