2017-02-20 14:33:00

Hospitali ya Rufaa ya Haydom, Dayosisi ya Mbulu kupandishwa hadhi!


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali haina kipingamizi na wazo la kuifanya hospitali ya rufaa ya Haydom kuwa ya kanda kwani hatua hiyo itaupunguzia mzigo Serikali. “Serikali hii ni sikivu, na kuifanya hospitali hii kuwa ya kanda ni kazi ndogo. Kwa hiyo nitamleta Waziri wa Afya aje awaongoze kusimamia vigezo vya kuifanya hospitali hii iwe ya kanda,” amesema. Ametoa kauli hiyo leo mchana Jumatatu, Februari 20, 2017 wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Haydom kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kata.

"Serikali haina kipingamizi na wazo lenu, cha msingi ni vigezo muhimu vifuatwe. Kwa hiyo, nitamleta Waziri wa Afya awasaidie kuangalia vigezo," amesisitiza. “Kama vigezo havipo, tushirikiane kuvikamilisha kwa sababu uwepo wa hospitali hii kwa hadhi ya kanda kunaisadia Serikali kutokana na nafasi yake kijiografia,” amesema Waziri Mkuu  “Nia yetu ni kupunguza gharama kwa mgonjwa anayelazimika kutoka Simiyu hadi Bugando (Mwanza) au kutoka Arusha hadi Muhimbili (Dar es Salaam). Hapa ni katikati na nimearifiwa kuwa wagonjwa kutoka mikoa mitano ya Tabora, Simiyu, Arusha, Singida na Manyara wanafika hapa kupatiwa matibabu,” amesema.

Amesema Serikali imepokea maombi kwa ajili ya watumishi wanaotakiwa kwenye hospitali hiyo na kwamba hivi karibuni itaajiri watumishi kati ya 5,000 hadi 6,000 wa sekta ya afya peke yake. “Tumekwishaanza kuajiri, tumeanza na sekta ya elimu kwa kuajiri walimu 4,693 ambao wote ni wa fani ya sayansi. Na sekta inayofuata ni ya afya, kwa hiyo hao watumishi 90 wanaohitajika watapatikana kwenye kundi hilo hilo,” amesema.Hospitali hiyo inahudumia wananchi kutoka wilaya nane za Mbulu, Hanang, Babati, Karatu, Mkalama, Iramba, Kondoa na Meatu.

Wakati huohuo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bibi Hannamarie Kaarstad ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, alisema amefarijika na mchango unaotolewa na Serikali ya Tanzania kusaidia juhudi zinazofanywa na marafiki wa hospitali walioko Norway. “Hospitali ya Haydom ni mahali thabiti ambapo mshikamano baina ya Tanzania na Norway unaweza kuonekana kwa dhahiri. Nawashukuru watumishi wa hospitali kwa moyo wao wa kujitoa kuwahudumia wananchi wa wilaya ya Mbulu na maeneo ya jirani,” amesema.

Hospitali hiyo ambayo inaendeshwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu kwa ufadhili kutoka Serikali za Tanzania na Norway, ilianzishwa mwaka 1955 ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50. Hivi sasa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 420 kwa wakati mmoja. Pia inatoa huduma za upasuaji, magonjwa ya macho, tiba ya mifupa na mazoezi ya viungo. Ilipandishwa hadhi kuwa ya rufaa baada ya mkoa wa Manyara kuanzishwa.

Mapema, akisoma taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba wa hospitali hiyo, Dk. Emanuel Q. Nuwass alisema wameomba kibali cha ajira kwa watumishi 90 kupitia bajeti ya mwaka 2016/2017. “Tumeomba pia hospitali ipandishwe hadhi na kuwa ya rufaa ya kanda (Kaskazini kati au Kanda maalum) ili iweze kutoa huduma bora kwa mkoa wa Manyara na mikoa jirani kwani wahisani wa maendeleo wako tayari kuchangia ujenzi wa miundombinu,” alisema. Pia aliomba waongezewe ruzuku ya dawa ikilinganishwa na ya sasa hivi ambayo ni asilimia 15 na pia waongezwe malipo ya on call allowance kwa ajili ya madaktari na watumishi wengine wa hospitali hiyo.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.