2017-02-18 16:11:00

Wafanyakazi katika sekta ya haki zingatieni ukweli na utu wema!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 18 Februari 2017 amezindua Mwaka wa Mahakama mjini Vatican kwa Ibada ya Misa Takatifu, ili kumwomba Roho Mtakatifu awasaidie wahusika wote kutekeleza vyema wajibu wao wa kuhudumia vyema haki ya binadamu, katika msingi wa amani, utulivu ili kuokoa na kudumisha mahusiano mema; mambo ambayo ni matunda ya hekima ya binadamu ambayo kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu.

Kardinali Parolin, amekita mahubiri yake kwenye tukio la Yesu Kugeuka Sura mbele ya wafuasi wake, ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, tayari kupokea kashfa ya Msalaba, kielelezo cha utii kwa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni na wokovu wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kung’arisha maisha yao kwa njia ya mwanga wa ufufuko wake. Hili ni tukio ambamo Yesu anatangaza pia Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Ubinadamu wa Yesu unauficha Umungu wake; kielelezo makini cha upendo wa Mungu katika historia ya mwanadamu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, Tukio la Yesu kugeuka Sura pale Mlimani Tabor, linaonesha mwanga wa Kristo unaofukuzia mbali giza la maisha ya binadamu; mateso na hata kifo chake. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, maisha yao yanaangazwa na mwanga wa Kristo Mfufuka hatua kwa hatua katika maisha yao, ili kuwawezesha hata wao pia kuwa ni mwanga angavu!

Hii ni changamoto ya kupambana na chuki ili kujenga fadhila ya upendo; kuondokana na hali ya kutowajali wengine ili kuambata wema na huruma ya Mungu; kuwa kweli ni watu wa ibada na msamaha, ili kupambana na ukosefu wa haki ili kuwatendea watu wote haki, yaani kile wanachostahili, kwa uaminifu, ukweli, uwazi na uhuru kamili. Hapa jambo la msingi ni kuzingatia sheria asilia ambayo imechapwa katika sakafu ya moyo wa mwanadamu inayomwelekeza kutenda mema.

Wafanyakazi katika sekta ya haki wanapaswa kuwa makini kwa kuzingatia ukweli na wala si maoni ya wengi; kwa kutekeleza dhamana na wajibu wao katika hali ya unyenyekevu na utu wema, hasa pale Mahakimu wanapotoa hukumu zao. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hukumu ya kifo imepitwa na wakati na kwamba, kifungo cha maisha ni hukumu isiyokuwa na matumaini tena kwani haimpatii mhusika nafasi ya kujirekebisha na kuanza tena kuandika historia ya maisha yake kwa wema. Haki ni jambo ambalo linawasaidia binadamu kudumisha amani, itakayofikia utimilifu wake mwisho wa nyakati. Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Professa Gian Pietro Milano alitoa hotuba elekezi mintarafu shughuli za Mahakama zilizotekelezwa mjini Vatican kwa mwaka 2016 na matarajio yao kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.