2017-02-18 15:18:00

Mwilisheni ushuhuda wenu katika matendo ya huruma lugha inayoeleweka!


Shirika la Mapadre wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili linajizatiti katika huduma kwa Kristo na Kanisa lake katika nchi ishirini, sehemu mbali mbali za dunia. Kwa sasa Mapadre hawa wanaadhimisha mkutano mkuu wa Shirika ambao pamoja na mambo mengine unapembua kwa kina na mapana Sheria za Shirika, Sera na Taratibu za maisha, ili kurejea tena katika misingi ya hija ya maisha ya Shirika mintarafu Karama yao ambayo kimsingi ni zawadi kwa Kanisa. Mapadre hawa wanapaswa kufanya tafakari hii kwa uaminifu kwa karama ya Mwanzilishi wao wa Shirika pamoja na kuzingatia amana ya maisha ya kiroho inayofumbatwa katika Shirika lao, sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati, kwa kuwa na akili na moyo wazi!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 18 Februari 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Mapadre wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kuhakikisha kwamba, wanafuata mfano wa Mtakatifu Stanislao wa Yesu na Maria, aliyemtangaza kuwa Mtakatifu kunako Mwaka 2016, ili kweli aweze kuwa ni mwanga na dira katika hija ya maisha na utume wao.

Mtakatifu Stanislao alijitambua kuwa ni Mfuasi wa Kristo Yesu na kumweka kuwa ni kiini cha upendo wake, kiasi kwamba, hakuna jambo lolote ambalo lingeweza kufua dafu ili kumtenganisha ni Kristo Yesu, kwani aliweza hata kumuunganisha katika huruma yake isiyokuwa na kifani! Hata katika mapungufu yake ya kibinadamu alitambua kwamba, wema wa Kristo ungeweza kumwambata. Ndiyo maana hata katika udogo wake, aliweza kuteseka kama sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo unaoteseka.

Kutokana na mwelekeo huu, Baba Mtakatifu Francisko anawataka Watawa hawa kutoa huduma ya Neno inayoshuhudia Ufufuko wa Kristo Yesu, waliyebahatika kukutana naye katika hija ya maisha yao na kwamba, kutokana na mtindo wao wa maisha, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanampeleka Kristo Yesu, sehemu mbali mbali za dunia. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unafumbatwa katika mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, asili ya Shirika hili la kitawa.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kuwahudumia maskini na wanyonge kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu katika lugha inayoeleweka kwa walengwa, yaani ushuhuda unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na sala kwa ajili ya kuwaombea waamini marehemu! Mwenyeheri  Giorgio Matulaitis amewaachia amana kubwa ya maisha ya kiroho, kwani maisha yake yote ni ushuhuda unaomwonesha jinsi alivyojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, akalipigania Kanisa na kwenda pale kulipokuwa na mahitaji, changamoto kwa watawa hawa kueneza karama ya Shirika katika nchi maskini hasa zile zilizoko Barani Afrika na Asia. 

Hapa changamoto kubwa anasema Baba Mtakatifu ni mchakato mzima wa utamadunisho unaokabiliwa na mabadiliko makubwa na ya haraka kijamii na kitamaduni. Lakini, Shirika hili linamshukuru Mungu kwa kuwa na mashuhuda jasiri wa Kristo na Injili yake, mwaliko wa kutembea katika ari iliyopyaisha; kwa uhuru wa kinabii, mang’amuzi ya hekima katika barabara za utume na maeneo ya kimissionari; kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Maaskofu mahalia pamoja na mihimi mingine ya Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre hawa watawa kushuhudia ujumbe wa Injili kwa watu wote pasi na ubaguzi pamoja na kuendelea kupanua wigo wa utume wao, kwani kuna umati mkubwa wa watu wenye hamu ya kutaka kumfahamu Kristo Yesu, Mkombozi pekee wa binadamu; ili kuwaokomboa kutoka katika hali ya ukosefu wa haki, mmong’onyoko wa kimaadili; pamoja na umaskini wa hali na kipato unaowashambulia waamini wengi. Utume na dhamana hii unahitaji kwa namna ya pekee toba na wongofu wa ndani unaotekelezwa katika ngazi ya mtu binafsi na jumuiya katika ujumla wake. Wajitahidi kuwa wazi kwa neema ya Mungu tayari kusoma alama za nyakati, ili kuzima kiu ya binadamu anayehitaji matumaini na amani.

Baba Mtakatifu anawataka Mapadre hawa kuwa na ujasiri katika huduma kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kujizatiti kikamilifu ili kukabiliana na changamoto mamboleo ambazo wakati mwingine ni hatari sana, lakini watambue kwamba, katika vinasaba vya maisha na utume wao wako tayari kupambana na vikwazo pasi na kukata wala kukatishwa tamaa. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaweka Mapadre hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ili daima waweze kuungana na Kristo Yesu pamoja na Roho Mtakatifu anayewawezesha kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Mfufuka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.