2017-02-18 17:31:00

Jifunzeni kupenda na kusamehe bureeeee kabisa ili muwe wakamilifu!


Huluka ya kibinadamu inatutuma kurudishiana wema tunaotendeana. Unapomtendea mtu  wema hata kama ni kidogo, unategemea afurahi, ashukuru au walau ajali na kutambua wema uliomtendea. Kwa hiyo ni sawa na kuwekeza upendo tukitegemea kurudishiwa upendo. Haki ya mahusiano ulimwenguni imelala katika  nipe nikupe au mkono kwa mkono. Wakati mwingine mantiki hii ya kufikiri tunampandikizia Mungu kwani hata katekismo inasema: “Mungu ni mwema kwa wanyofu na anawaadhibu wabaya.”

Juma lililopita tulimsikia Yesu akisema: “Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” Huu ufalme wa mbinguni haimaanishi paradisini, bali ni ulimwengu wa haki mpya aliyotuletea Yesu Kristu. Hatari iliyoko kwetu ni kule kubaki katika haki tunayoifikiria sisi na kujidanganya kwamba tuko katika ulimwengu unaotakiwa. Katika fasuli ya Injili ya leo Yesu anatutaka tufuate haki mpya anayotupendekezea yaani ile ya kutenda wema na kufanya ukarimu wa bure, usiohesabu gharama, usiotegemea kurudishiwa chochote, usiojali mahusiano gani yapo kati yako na yule unayemtendea wema. Lengo la kutenda wema ni kumtakia mwingine kuishi vyema na kuwa na furaha. Haki hiyo unaitenda kwa kusukumwa na roho ya kimungu iliyowekwa ndani ya mioyo yetu na Mungu mwenyewe. Haki hiyo ni huluka iliyoko ndani mwetu inayofanana na ua linalotoa harufu inayonukia vizuri bila kutegemea kurudishiwa shukrani hata kama likikanyagwa linaendelea tu kunukia vizuri. Mwanafunzi wa Yesu ni yule anayesukumwa na haki hii mpya.

Baada ya kuona maana hii ya haki na asili yake, leo tunaendelea kuona mfano miwili ya mwisho inayotuonesha kwamba Yesu amefika kukamilisha Torati na Manabii. Mosi, Yesu anasema: “Mmesikia kwamba imenenwa: Jicho kwa jicho, na jino kwa jino.” Sheria hii inayo bado uzito wake katika ulimwengu wa leo. Hata hivyo, budi ieleweke kwamba hadi hapo sheria hiyo imeshapiga hatua kubwa sana. Kabla yake mtu akikosewa haki, aliokosea aliadhibiwa vikali sana na alilipwa kisasi karibu mara sabini na zaidi. Mathalani, kama mtoto amekurushia jiwe unaweza hata kulipiza kisasi cha kumwua. Kumbe Jicho kwa jicho na jino kwa jino, ilikuwa ni adhabu ya haki, kwani analipa kile alichokosea tu basi. Hii ilikuwa ni haki ya ulimwengu yenye kuhesabu ovu.

Kumbe, Yesu anasema: “Msishindane na mtu mwovu;” Hapa Yesu anatupendekezea siyo tu kujitoa kutoka katika mantiki hiyo ya kulipa kisasi, bali tusirudishiane uovu kwa uovu au kutendeana wema kwa wema yaani  kuhesabiana mambo. Kinachotakiwa ni kutoa bure, kama Mungu anavyotupenda watu wote bure. Kutoka katika uelewa huo tunaletewa  mifano minne ya mtu mwenye hadhi ya kuwa mwana wa Mungu, yaani yule anayesukumwa na upendo wa bure, na jinsi anavyotakiwa ayatoe majibu ya haki na upendo kwa mtu awaye yeyote:

Kwanza Yesu anasema: “lakini mtu akupigaye shavu la kuume.” Hapa anataka kuzungumzia juu ya uharibifu mkubwa wa kimwili, yaani jinsi ya kumjibu mtu anayekuzaba kofi. Ni kwamba hadi sasa inaeleweka kwamba mmoja akikupiga kofi shavu la kulia maana yake ametumia upande wa nje ya mkono kukuzaba kofi. Wengine waliita hilo kuwa ni kofi la kumakava.

Kofi hilo ni la kumdhalilisha mwingine. Yesu anatuonesha jinsi ya kujiweka mbele ya uonevu wa kimwili. Hapo mkristu inambidi apige hatua mbele zaidi ya kutofanya chochote isipokuwa: “mgeuzie na la pili.”  Yaani kutofanya ubaya mwingine zaidi badala yake kufanya maamuzi magumu zaidi ya kugeuza shavu jingine kusudi nalo lizabwe. Hapa unaalikwa kujihoji, uchukue hatua gani unapokosewa haki. Hapo kama unao msukumo wa kulipa kisasi hutaweza kugeuza shavu. Lakini kama unasukumwa na upendo utaamua kumgeuzia shavu la pili. Pili Yesu anasema: “Mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.” Yaani anayekudhalilisha na kukukosea haki kiuchumi. Joho lilikuwa ni kitu cha mtu binafsi. Mmoja anakushtaki mahakamani na kukuchukulia mali ambayo ni haki yako. Hapo Yesu anasema wewe mwachie hata joho lako pia, kwamba, penye tatizo la kiuchumi, wewe uongozwe na upendo.

Tatu Yesu anasema: “Mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.” Yaani kunyanyaswa na kunyimwa uhuru wa maamuzi. Hapa kulazimisha kwa kigiriki ni (aggareusei) kama vile Simoni wa kirene alivyolazimishwa kubeba msalaba wa Yesu. Wanakijiji walikuwa mara nyingi wanalazimishwa kuwatumikia maaskari. Katika mazingira kama hayo, Wazeloti walisema kwamba, kama askari au mtu yeyote akikulazimisha kumbebea mzigo wake, wewe mwitikie tu kinafiki, lakini ukifika pahali penye gema we msukumie bondeni akafie mbali huko. Namna nyingine ya kufanya walisema kama wakikulazimisha kuwapatia punda wako, wewe usibishane nao, kwa sababu usipowapatia, watakutwanga mangumi kisha wanakunyang’anya punda wako. Kumbe, Yesu hachukui maamuzi hayo, bali anachukua huluka ya mwana wa Mungu anayesukumwa na upendo tu.

Nne Yesu anasema: “Akuombaye mpe” yaani masuala ya kukopa na kukopeshwa. Yesu anasema, “Anayetaka kukukopa kitu, usimpe kisogo.” Unapomwona anayehitaji msaada wako, hapo huluka yako ya umwana wa Mungu anayependa tu basi haifanyi mahesabu, kwamba labda atanirudishia au la. Wewe toa tu ulicho nacho  kwa upendo. Kwa jumla mapendekezo haya aliyofanya Yesu yamekuwa na matatizo makubwa katika kuyatafsiri, sanasana kutoka kwa wale ambao wanachagua haki ya ulimwengu huu. Mkristu hataki kufanyiana ukatili wala kuoneana kwa sababu palipo na uonevu hapo hapana ufalme wa Mungu. Ufalme wa Mungu upo pale ambapo pana haki na kuna kupendana.

Wayahudi wa karne ya kwanza waliwapinga wakristu kwamba: “Masiha Yesu hajatimiliza Maandiko Matakatifu, kwa sababu katika Maandiko Isaya, anasema: “Dubu (chui) atakaa pamoja na kondoo; mapanga na silaha za vita zitayeyushwa kuwa majembe ya kulimia, na hivi hakutakuwa na vita tena. Lakini kumbe vita vipo bado hadi sasa hapa duniani.” Wakristo wakawajibu: “Ni kweli duniani vita zinaendelea kuwepo, lakini kuna jumuia iliyo kinyume cha maisha hayo nayo ni jumuia ya wakristu ambayo silaha hizo kwao hazipo kabisa. Huo ndiyo ufalme wa Mungu unaoweza kuenea ulimwenguni kote.” Kwa hiyo palipo na vita na uonevu hapo ufalme wa Mungu haujafika bado.

Mfano wa mwisho, unaohusu kutoikana tora bali ni kuimarisha zaidi Yesu alisema: “Mmesikia kwamba imenenwa: Umpende jirani yako, na umchukie adui yako.” Sehemu ya kwanza ya fasuli iko katika tora. “Upende jirani yako,” Lakini sehemu ya pili “umchukie adui yako” haipo kabisa katika agano la kale. Lakini hivi ndivyo ilivyokuwa fikra za watu wa ulimwengu wa kulipana wema kwa wema na ubaya kwa ubaya.  Hata watawa wa Kumrani walisema: “Wapendeni wana wa mwanga na wachukieni wana wa giza.” Kumbe, hata huko  hakukuwa kna mantiki ya kupenda bure kadiri ya Yesu wa Nazareti. Lakini Yesu anasema: “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi.”

Neno hili kupenda kwa kigiriki agapan, halikuwa linatumika sana katika lugha ya kawaida, bali lilitumika zaidi na wakristu ili kuonesha upendo wa Baba wa mbinguni unaotakiwa uwe katika moyo wa kila mwana wa Mungu. Ili kuwa na upendo kama huo yabidi kusali ili kuudumisha. Ukweli ni kwamba tabia ya kurudishiana ufadhili ilizaliwa katika ukristu, kutokana na ubinafsi wa kiroho ya mahusiano ya nipe nikupe na Mungu. Mmoja alitenda jema akitumaini kutuzwa na Mungu. Anayefikiri hivyo, bado hajaingia katika ufalme wa Mungu anayependa bure. Motisha anayotoa Yesu hadi upendo uweze kumfikia hata adui, bila kupata faida kwa sababu u mwana wa Mungu, kwa sababu:“Mungu anawaangazia jua lake waovu na wema, na kuwanyeshea mvua wene haki na wasio na haki.” Kwamba, Mungu ni mwema kwako unapokuwa mwema, hata pale unapokuwa mbaya kwa sababu Mungu ni upendo tu basi.

Kwa hiyo Yesu anaagiza: “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Kadhalika hapa tusielewe kwamba sasa tutende mema ili tuweze kuwa kama Baba wa mbinguni, bali Yesu anasema: kwa vile wewe sasa unayo huluka na hadhi ya Baba wa mbinguni aliye mkamilifu, mwenye upendo usio na mwisho, basi na wewe sasa uanze kuwajibika katika huluka yako hii mpya. Kama mama anavyotakiwa awe na huluka ya kumpenda mtoto wake nawe pia uwe na huluka ya kupenda.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.